Friday, November 25, 2016

WAFANYABIASHARA MKOANI SINGIDA WAJIPATIA BILIONI 1.8 KWA MAUZO YA KUKU.

Mwenyekiti wa Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew John Mtigumwe akiongoza kikao hicho, kushoto kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dokta Angelina Mageni Lutambi, wa kwanza kulia ni Waziri wa Mambo ya ndani Mwigulu Lameck Nchemba na anayefuata ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida Mhe. Martha Mlata.
Mbunge wa Viti maalum CCM Singida Aisharose Matembe akichangia hoja katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Singida (RCC). 
Meneja wa SIDO Mkoa wa Singida Shoma Kibende akichangia hoja katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Singida (RCC).

Na Nathaniel Limu-Singida
Wafanyabiashara wa kuku wa asili/kienyeji mkoani Singida wamejipatia mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 1.8, baada ya kuuza kuku 151,242 katika kipindi cha mwaka jana hadi sasa.

Hayo yamesemwa juzi na kaimu Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Beatus Choaji wakati akitoa taarifa ya uendelezaji wa kuku wa asili, kwenye kikao cha kamati ya ushauri mkoa (RCC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano uliopo kwenye jengo la ofisi ya mkuu wa mkoa mjini hapa.

Chowaji amesema mapato hayo yamepatikana baada ya kuku hao 151,242 kusafirishwa  na kuuzwa nje ya mkoa ikiwemo jijini Dar-es-salaam.

“Kuku wa asili wakifungwa vizuri kwa kudhibiti ugonjwa wa mdondo na kuzingatia kanuni za ufugaji bora wanaweza kuleta mabadiliko makubwa na ya haraka ya kipato. Kuku wa asili pia ni lishe bora hususani kwa watoto na akina mama”, ameongeza Choaji.

Ili kuimarisha ufugaji kuku wa asili amesema imependekezwa halmashauri zote zitekeleze mkakati wa kuchanja kuku kwa wakati moja mara tatu kwa mwaka kwa kutumia watoa chanjo wasiokuwa wataalam wa mifugo.

Akisisitiza amesema “Mkakati huu unatarajiwa kuanza mara halmashauri zitakazokamilisha utoaji wa mafunzo kwa watoa chanjo hao. Halmashauri zimesisitizwa kushiriki kikamilifu kutekeleza mkakati huo ili kuinua kipato cha wananchi kwa haraka zaidi”.

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Singida na mwenyekiti wa kikao hicho, Mhandisi Mathew John Mtigumwe, akifungua kikao hicho ameagiza kuwa wananchi wahamasishwe, ili wasiendelee kuuza chakula walichovuna msimu uliopita kiweze kuwafikisha msimu ujao wa mavuno.

Mhandisi Mitugumwe amesema kwa mujibu wa mamlaka ya hali ya hewa nchini (TMA) mvua za msimu huu zinatarajiwa kunyesha kwa kiwango cha chini ya wastani.

“Hivyo ni jukumu letu sote kuhimiza na kushauri wananchi kufuata kanuni bora za kilimo na kupanda mazo ya kipaumbele yanayostahimili ukame, na yanayokomaa mwa muda mfupi.

Wakati huo huo Mkuu huyo wa mkoa, ametumia fursa hiyo kutoa shukrani zake za dhati kwa wananchi wadau wa elimu, wafanyabiashara, kampuni za simu za viganjani na mashirika ya umma na binafsi, kwa kushiriki kutekeleza agizo la rais Magufuli la kumaliza uhaba wa madawati mashuleni.

No comments: