Vyama vya Ushirika vimetakiwa kushiriki katika kuanzisha viwanda vidogovidogo ambavyo vitawezesha uchakataji wa mazao ya wakulima, wavuvi na wafugaji, kuweka kwenye madaraja na kufungasha tayari kwa ajili ya mauzo.
Wito huo umetolewa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini Bw. Tito Haule katika Ufunguzi wa Kikao Kazi cha Warajis Wasaidizi Wa Vyama Vya Ushirika Wa Mikoa kilichofanyika leo mjini Dodoma Novemba 15, 2016.
“Sekta ya Ushirika ina mchango mkubwa katika kuwezesha kutimia kwa azma ya Serikali ya kukuza uchumi, hivyo kila mmoja wetu katika eneo lake tuweke msukumo katika vyama vya ushirika ili viweze kuwa sehemu ya utekelezaji wa azma hii ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuipeleka nchi yetu katika uchumi wa viwanda ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza kasi ya kufikia lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025,” alisema Mrajis.
Viwanda vinavyomaanishwa siyo lazima viwe viwanda vyenye kuhitaji mitambo mikubwa bali vinaweza kuanzishwa viwanda vidogovidogo ambavyo vitawezesha uchakataji wa mazao.
Bw. Haule akizungumzia kuhusu majukumu yatakayopewa kipaumbele na Tume ya Maendeleo ya Ushirika alisema ni kusimamia na kudhibiti badala ya kuwa wasuluhishi wa migogoro katika Vyama vya Ushirika.
“Sote tunafahamu kwamba kuna udhaifu mkubwa katika eneo la usimamizi na udhibiti wa vyama vya ushirika na hivyo kusababisha utii wa sheria kutozingatiwa katika uendeshaji wa shughuli za vyama vya ushirika. Hivyo, kipaumbele changu cha kwanza ni Usimamizi, cha pili ni Usimamizi na cha tatu ni Usimamizi”, alisema Bw. Haule.
No comments:
Post a Comment