Tuesday, November 1, 2016

Utaratibu wa ajira kwa watanzania wanaofanya kazi za ndani katika nchi za Mashariki ya Kati kuangaliwa upya

Na. Immaculate Makilika- MAELEZO

Watanzania 5600 wanakadiriwa kufanya kazi katika kada za madaktari, walimu, wauguzi, wahadhiri, wapishi, wahudumu wa mashambani na bustani na watumishi wa nyumbani, na kati ya hao karibu watanzania 200 ndio wanaofanya kazi za ndani katika nchi za Mashariki ya Kati.

Kada inayofanya kazi za ndani ndio inayopata changamoto nyingi huko ugenini ikiwemo ujira mdogo na vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji. Jambo hili halipaswi kufumbiwa macho. Hata hivyo zipo jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo zimefanyika kupunguza ama kuondoa hali hii.

Kufanya kazi nje ya nchi bila mateso au manyanyaso ni haki ya binadamu kama inavyoainishwa katika mikataba ya kimataifa. Katika makala hii utaweza kuona baadhi ya vipengele vya mikataba hiyo.

Mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na kisiasa wa mwaka 1966, unataja haki mbalimbali za kiraia zinazolindwa na mkataba huo ikiwa ni pamoja na haki ya kutopewa mateso au kufanyiwa ukatili au vitendo vya kikatili na udhalilishaji ikiwemo hukumu za kikatili katika ibara ya 7. Uhuru wa mtu na usalama wake katika ibara ya 9 na uhuru wa mtu kwenda atakako na kuchagua mahala pa kuishi katika ibara 12.

Katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 17 Kifungu cha (1) kinampa haki raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kwenda kokote ndani na nje ya nchi bila kuvunja sheria za nchi. Kwa misingi hiyo watanzania wanapata fursa za kwenda nje ya nchi, hususani nchi za kiarabu kwa lengo la kufanya kazi za ndani ili kujiongezea kipato na kuweza kuinua uchumi wa familia zao na pamoja na taifa kwa ujumla.

Lakini jambo linalovutia idadi kubwa ya watanzania kwenda kufanya kazi katika nchi za Mashariki ya Kati ambazo ni Omani, Saudi Arabia, Qatar, Bahrain, Kuwait, Lebanon, Syria, Iran, Iraq na Yemen pamoja na nchi zinazounda Falme za kiarabu ambazo ni Abu dhabi, Dubai, Ajman, Al Ain, Fujuirah, Ras al Khaimah na Sharjah ni uhusiano wa karibu sana ambao ni wa kihistoria na kidamu, ambapo nusu ya familia za Oman asili yake ni Tanzania na hivyo kufanya kuwa na mwingiliano wa karibu.

Lakini pia, nchi hizi kwa kiasi kikubwa ni tegemezi ya nguvu kazi kutoka nje ya eneo hilo na hivyo kusababisha soko kubwa la ajira katika maeneo mbalimbali kama vile madaktari, wauguzi, madereva, wapishi, wahudumu wa saluni, watumishi wa shambani na hasa watumishi wa nyumbani(house maids).

Asha Abdallah (si jina halisi) mwenye umri wa miaka 25, aliacha familia yake ya mume na mtoto mmoja, na kwenda kufanyakazi za ndani nchini Omani akiamini kuwa atapata kipato kitakachosaidia kuitunza familia yake nchini Tanzania.Hata hivyo, maisha yake ya nchini Omani yameififisha ndoto yake, kwa vile imemlazimu kurudi nchini Tanzania kwa visa vilivyomkumba nchini humo.

“Nilinyanyasika mno, kazi zilikua nyingi sana, sikuwa napata muda wa kupumzika, hata chakula nilikula kwa uoga, nilipoona siwezi kuvumilia zaidi baada ya kukaa mwaka mmoja ilinilazimu kusema nimefiwa na muwe wangu ili mradi nirudi nchini Tanzania”, anasema Asha. Hadi kufikia Januari mwaka huu karibu watanzania 200 wameajiriwa katika kazi za utumishi wa nyumbani nchini Omani.

Naye, mwanamke mmoja mwenye asili ya Tanzania (jina limehifadhiwa) aliyekuwa akifanya kazi ya uwakala wa kusafirisha wasichana kutoka Tanzania kwenda kufanya kazi za ndani nchini Omani, anasema ni kweli kumekuwepo na changamoto nyingi katika kazi hiyo, na wakati mwingine changamoto hizo si za kweli ama zinakuzwa.

“Nilifanyakazi hii kwa miaka 10, nimeacha hivi karibuni baada ya kuona inakabiliwa na changamoto nyingi, baadhi ya wasichana wanasafirishwa hadi Omani na wanapofika huku wanakua hawako tayari kufanya kazi kulingana na makubaliano ya kazi yenyewe”.

Anaongeza kuwa,“Wengine wanajisahau kama huku si Tanzania na hivyo lazima waendane na maisha ya huku, hata hivyo naishauri Serikali ya Tanzania na Omani kupatia ufumbuzi changamoto zenye ukweli kwa vile hivi karibuni kumekuwepo na visa vingi kuhusu wasichana wa kazi hapa Omani”, anasema wakala huyo.

Licha ya kuwa ni kazi inayowapatia kipato watanzania hao, kumekuwepo na  malalamiko kadhaa ikiwemo mazingira magumu ya kufanyia kazi, kufanyakazi masaa mengi, kukosa mapumziko, mshahara mdogo, kufanyishwa kazi za ziada ya makubaliano pamoja na kunyanyaswa kijinsia.

Katika kupambana na hali hii Serikali imeandelea na utaratibu wake wa kawaida pamoja na kuanzisha utaratibu mpya ambao utasaidia kudhibiti changamoto mbalimbali zinazowakumba watanzania wanaokwenda kufanyakazi za utumishi wa ndani nchini Omani pamoja na nchi nyingine za Mashariki ya Kati.

Hivi karibuni Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima anasema Ubalozi kwa kushirikiana na wadau wengine kama Uhamiaji, Wizara ya Kazi, Wakala wa huduma za ajira Tanzania (TAESA), Kamisheni ya kazi Zanzibar, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Jeshi la Polisi pamoja na Idara ya Usalama wa Taifa wamekua wakifanya kazi kwa karibu ya kufuatilia watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi na hasa nchini Omani.

“Watanzania wanatakiwa kufahamu na kufuata utaratibu ambao unamtaka raia wa Omani mwenye nia ya kumwajiri mtanzania kuwa anatakiwa kwenda katika Ubalozi wa Tanzania na kujaza fomu ya maombi ya kumwajiri mtanzania na baada ya fomu yake kuridhiwa na Ubalozi, basi atapewa mkataba ambao atajaza na kuurudisha Ubalozi”, anasema Balozi Kilima.

Balozi Kilima anaongeza kuwa, “Mhusika anaporudisha fomu hiyo anatakiwa kuambatisha nakala ya kitambulisho cha utaifa, uthibitisho wa makazi, nakala ya pasi ya kusafiria ya mfanyakazi, hati ya kiapo na dhamana ya fedha za Omani kiasi cha rial 100”.

Baada ya Ubalozi kuridhika na vielelezo vyake, ubalozi utapitisha mkataba wa kumtaka mwajiri husika kuuwasilisha nchini Tanzania kwa mtumishi husika ambae atauwasilisha TAESA au Kamisheni ya kazi ambao nao watamhoji mhusika pamoja na kujidhihirisha kama ameuelewa mkataba na kazi atakayofanya na baada ya hapo mwajiri huyo wa kitanzania ataruhusiwa kwa kupewa kibali ambacho ni barua ya kumuomba Kamishna wa Uhamiaji kutoa ruhusa ya kwenda kufanya kazi nje ya nchi baada ya kufuata utaratibu uliowekwa.

Aidha, Serikali imeweka mkazo katika hatua kadhaa katika kutatua tatizo hili, ambapo imeanza kutumia wakala rasmi wa ajira ambao wameandikishwa na mamlaka husika.Kutumia mkataba wa ajira na kuhakikisha kila Ubalozi wa Tanzania katika nchi za Mashariki ya Kati unandaa mikataba ya kazi kutokana na muongozo uliokubaliwa na wadau wote.

Vilevile, Serikali inaandaa mtaala wa kuongeza ustadi na ujuzi kwa watanzania wanaofanya kazi za ndani katika nchi za Mashariki ya Kati.Aidha, Balozi huyo amesisitiza kuwa nia ya Serikali ya kuanzisha mtaala huo ni katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakumba nazo watanzania wanaofanyakazi za ndani nchini Omani.

“Serikali imeazimia kutumia Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) ili kuwa na mtaala utakaosaidia kutoa mafunzo mbalimbali ikiwemo utaratibu na utamaduni wa nchi mbalimbali wanazokwenda kufanya kazi, ili kusaidia watanzania kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu kazi husika na changamoto zake kabla ya kukubali kufanya kazi hizo,” anasema Balozi Kilima

Sambamba na hilo, Serikali imeendelea kuwataka watanzania kufuata utaratibu kabla ya kwenda kufanya kazi katika nchi hizo kwa kutumia wakala rasmi wa ajira walioandikishwa na mamlaka husika pamoja na kuwepo mkataba wa ajira unaotambuliwa na Mamlaka za nchi wanazookwenda ili kuepuka usumbufu na changamoto wanazoweza kuzipata ikiwemo kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na ukatili.




Balozi Kilima ameongoza kuwa katika kupata suluhisho la kudumu katika kuwasaidia watanzania kupata fursa za ajira nje ya nchi,Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea kufanya jitihada za kusaini Mikataba ya Ushirikiano katika Sekta ya ajira na kazi baina ya Serikali ya Tanzania na nchi mbalimbali.

No comments: