Tuesday, November 1, 2016

MWAKA MMOJA WA JPM, TRA YAVUKA LENGO LA MAKUSANYO YA MAPATO.


 YAKUSANYA WASTANI WA TRILIONI 1.1 KILA MWEZI
Na JOVINA BUJULU- MAELEZO.


Novemba Tano mwaka huu ni mwaka mmoja tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alipoapishwa kuwa kiongozi na Amri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Nchi hii.

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake, Watanzania wameshuhudia  mafanikio makubwa katika katika sekta ya ukusanyaji kodi kupitia vyanzo mbali mbali vya mapato. Hatua hii inatokana na kuwa Rais Magufuli alipoingia madarakani amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha hakuna mfanyabiashara anayekwepa ulipaji kodi na kuwahimiza wananchi kuhakikisha wanadai risiti kwa kila bidhaa au huduma wanayolipia.

Hivyo Serikali hii tangu ianze kazi rasmi imekuwa ikitilia mkazo ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kubuni vyanzo vipya ili kuongeza makusanyo ya Serikali.Juhudi hizi za Rais Magufuli za kuongeza mapato na kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali zimejionyesha katika mikutano yake mingi ambapo mara nyingi amekuwa akisema “Ukinunua bidhaa dai risiti na ukiuza bidhaa toa risiti”.

Jitihada hizo za wa ukusanyaji wa kodi kwa ajili ya kuongeza mapato ya Serikali kwa manufaa zitatekelezwa na uongozi wa Rais Magufuli zinaunga mkono wosia aliwahi kuutoa Baba wa Taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo alisema kuwa “Serikali yeyote isiyokusanya kodi ni “corrupt”.

Hatua hiyo ya kutoa na kudai risiti ina mchango mkubwa kwa serikali katika  kukusanya kodi ambazo zitasaidia katika kuboresha huduma za jamii kama vile elimu, afya, maji, umeme, usafirishaji, ujenzi na uendeshaji wa serikali kwa ujumla kutokana na mapato yanayopatikana.

Hapa nchini, Mamlaka ya Mapato (TRA) ndicho chombo chenye jukumu la kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Taifa na imekuwa ikitimiza lengo hilo kwa kutekeleza mikakati mbalimbali kama ilivyoainishwa katika mpango mkuu wa miaka mitano.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi Bw. Richard Kayombo, katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wa Rais Magufuli kumekuwepo na ongezeko la makusanyo ya mapato ya serikali yatokanayo na kodi.

Anasema kuwa katika kipindi hiki, TRA inakusanya wastani wa trillion 1.1 kila mwezi kuanzia mwezi Novemba, 2015 hadi Septemba 2016.
“Hili ni ongezeko la asilimia 28.1 kutoka kwenye kukusanya wastani wa shilingi bilioni 867 kwa mwezi katika kipindi cha mwezi Novemba, 2014 hadi Septemba 2015” anasema Bw. Kayombo.

Makusanyo ya mapato katika kipindi cha utawala wa Rais Magufuli kuanzia mwezi Novemba 2015 yamekuwa yakiongezeka ikilinganishwa na miaka iliyotangulia kwa mfano mwaka wa fedha 2015/2016 mapato yaliyokusanywa yalikuwa shillingi trilioni 12.5 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26.4 ya makusanyo ya mwaka 2014/2015. Aidha TRA imekwisha kusanya kodi kiasi cha shilingi trilioni 3.5 kufikia mwezi Septemba 2016, ikiwa ni ongezeko la asilimia 23.4 ikilinganishwa na kipindi kama hiki cha robo mwaka 2015/16.

Bw. Kayombo anaongeza kuwa kwa sasa TRA inatekeleza mpango mkakati wa nne wa ukusanyaji kodi wenye dhamira ya kuongeza makusanyo ya kodi za ndani kwa kuongeza ulipaji kodi wa hiari.

“Jitihada mojawapo zinazofanywa na TRA ni pamoja na kuboresha mifumo ya makusanyo inayoendana na mazingira ya sasa ya ukuaji wa teknolojia ili kuhakikisha walipa kodi wanalipa kwa urahisi kama ilivyo dhamira yake ya kurahisisha ulipaji kodi na kufanya mazingira yawe bora” anasema Bw. Kayombo. Katika kipindi cha mwaka mmoja ambao Rais Magufuli amekuwa madarakani, juhudi mbalimbali zimefanyika ili kuhakikisha matarajio ya Rais ya kuimarisha makusanyo ya kodi na kudhibiti mianya ya rushwa yanafanikiwa.

Mafanikio hayo yatamuwezesha Rais Magufuli kutimiza ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni zikiwemo kuboresha afya, upatikanaji wa maji, umeme, kutoa elimu bure, ujenzi wa miundombinu kama vile viwanja vya ndege, reli na barabara. Aidha makusanyo hayo yatawezesha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda ambavyo vitatoa ajira kwa wananchi na serikali kuweza kujitegemea na hivyo kupunguza utegemezi wa misaada kutoka kwa wafadhili.

Bw.Kayombo anataja kiini cha ongezeko la kukusanya kodi kuwa ni matumizi ya mashine za kielektroniki (EFD) ambazo zinatumika zaidi badala ya stakabadhi zinazoandikwa kwa mkono. “Matumizi ya stakabadhi zinazoandikwa kwa mkono hayakuwa na ubora mzuri wa kukusanya na kuongeza mapato na kutunza kumbukumbu sahihi ambayo yaliifanya serikali ipoteze mapato mengi” anaongeza.

Katika hatua nyingine TRA ilitoa mashine za EFDs 130 bure kwa makatibu wakuu wa Wizara mbali mbali kwa ajili ya taasisi za serikali ambazo zinakusanya maduhuli ya serikali kwa nia ya kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali.


Katika kuhakikisha makusanyo ya kodi yanaongezeka TRA imeendelea kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi, kufichua wakwepa kodi, kupambana na rushwa na kupanua wigo wa kodi kwa kusajili wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa sambamba na kuendesha zoezi la kuhakiki namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN) linaloendelea jijini Dar es Salaam kwa sasa ili kuboresha daftari la walipa kodi.

Pamoja na mafanikio hayo Kayombo alizitaja changamoto wanazokutana nazo katika ukusanyaji kodi kuwa ni pamoja na taarifa za kodi kutowafikia wananchi wote ili kujenga uhiari wa kulipa kodi na uwepo wa ukanda mrefu wa Pwani unaosababisha kuwepo mianya mingi ya ukwepaji kodi ambapo bidhaa huingizwa nchini kwa njia za panya.

Pamoja na changamoto hizo, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imeendelea kubuni mikakati mbali mbali ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ili kuendana na kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano isemayo “HAPA KAZI TU” ili kutimiza na kuvuka lengo la kukusanya shilingi trilioni 15.1 kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2016/17.

No comments: