Thursday, November 10, 2016

SHINDANO LA KUTAFUTA MBADALA WA MKAA LAANDALIWA,MSHINDI WA KWANZA KUIBUKA NA KITITA CHA SHILINGI MILIONI MIA TATU

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- uungano na Mazingira Mheshimiwa January Makamba akiongea na Wandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya shindano la kutafuta mbadala wa mkaa,   lilioandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.



KUHUSU SHINDANO LA KUTAFUTA MBADALA WA MKAA 

Nchi yetu iko njia panda. Tuna nchi nzuri yenye bioanuai za wanyama na mimea ambazo haziwezi kufananishwa na nchi nyingine yeyote. Takriban asilimia 40 ya eneo lote la nchi limehifadhiwa kwa ajili ya misitu na wanyamapori. Hata hivyo, uharibifu wa misitu unafanyika kwa kasi ya kutisha. Takriban ekari milioni moja za misitu zinateketezwa kwa mwaka. Karibu mabonde na mifumo yote ya mito mikuu hapa nchini inaanzia kwenye misitu ambayo sasa tunaiharibu kwa kasi ya kutisha.

 Kuna mambo kadhaa yanayochangia kasi hii kubwa ya uteketezaji wa misitu hapa nchini, ikiwemo ufyekaji wa maeneo kwa ajili ya kilimo, mifugo, uchomaji wa mkaa na biashara ya kuni. Hakuna shaka kwamba mahitaji ya mkaa na kuni yanazidi uwezo wa misitu yetu ya asili kukukidhi mahitaji hayo. Mahitaji haya yataendelea kuongezeka kwa kasi kwa miaka inayokuja kutokana na ukuaji wa miji na ongezeko la idadi ya watu, kwani inaaminika kwamba ongezeko la asilimia moja ya ukuaji wa miji linasababisha ongezeko la asilimia 14 la matumizi ya mkaa.

Ikizingatia kwamba, Tanzania ni moja ya nchi zinazoongoza duniani kwa kasi ya ukuaji wa miji, kiasi kwamba ifikapo mwaka 2027 zaidi ya nusu ya Watanzania watakuwa wanaishi mijini, mahitaji na matumizi ya mkaa yatakuwa maradufu kuliko ilivyo sasa. Hivyo, ni muhimu sana hatua za haraka ni muhimu zichukuliewe sasa ili mahitaji haya ya makubwa ya mkaa yasipelekee kuangamizwa kwa misitu yetu. 

Kuwa na uzalishaji endelevu wa  mkaa, au kuifanya biashara ya mkaa isiwe na tija, au mbadala wa mkaa kuwa na faida zaidi kibiashara, ni jambo la msingi kwa usalama wa nishati kitaifa, kwa kupunguza ukataji misitu na kulinda huduma zitokanazo na mifumo-ikolojia nchini, ikiwemo ulinzi wa vyanzo vya maji, utiririkaji wa maji katika mito na hivyo upatikanaji wa maji nchini.

Naamini kuwa moja ya njia za kuokoa mazingira yetu, kulinda urithi adhimu uliomo katika Hifadhi zetu, na kurejesha thamani ya maliasili yetu ni kwa kupunguza ukataji wa misitu kwa ajili ya mkaa. Njia bora ya kufanya hivyo ni kwa kupunguza matumizi ya mkaa kupitia  ubunifu wa teknolojia za nishati nafuu na zenye ufanisi zaidi na endelevu; na vyanzo nafuu vya nishati mbadala katika ngazi ya kaya. 

Lakini leo tunaweza kuanza safari ya kuondokana kabisa na matumizi ya mkaa kupitia ubunifu katika ujasiriamali wa nishati za kupikia - hasa ubunifu kwa upande wa uzalishaji na usambazaji wa nishati mbadala wa mkaa, na katika kuufanya mkaa kupata ushindani mkubwa katika soko la nishati za kupikia au ubunifu katika kufanya uzalishaji na matumizi ya mkaa kuwa endelevu (kutoharibu mazingira). Naamini kwamba inawezekana kabisa kuanzisha na kuendeleza mifumo mipya ya uzalishaji, usambazaji na uuzaji wa nishati ya kupikia ambayo itapunguza kasi ya ukataji miti na kupunguza athari kwa mazingira nchini.

Ninazindua kwa mara ya kwanza Shindano la Kitaifa la Kutafuta Mbadala wa Mkaa. Madhumuni ya msingi ya Shindano hili ni kuwatambua, kuwatuza, kuwawezesha na kuwaendeleza wabunifu na wajasiriamali wanaojihusisha na mbinu na jitihada za uzalishaji, usambazaji na matumizi ya nishati endelevu za kupikia. Natoa wito kwa wadau wote: watu binafsi, wabunifu, makampuni binafsi, wajasiriamali, asasi za kiraia na kijamii, taasisi zisizokuwa za Kiserikali, Taasisi za Elimu ya Juu, na Taasisi za Utafiti, kushiriki katika changamoto hii.

Moja ya madhumuni ya ziada ya shindano hili ni kuwaleta pamoja wadau na wabunifu wanaojishughulisha na harakati za kutafuta na kutumia nishati mbadala wa mkaa. Kama sehemu ya mchakato huu, na hasa baada ya shindano, kutakuwa na warsha, semina, mafunzo ambazo zitawaleta pamoja wadau wote kuendelea kutafakari jitihada za ziada za kupata nishati mbadala wa mkaa. 
Aidha, mafanikio mengine tunayoyatarajia ni kama  yafuatayo:-
§  Kuinua uelewa juu ya suala la ukataji miti na umaskini wa nishati kwa mapana zaidi miongoni mwa watu wa kawaida;
§  Kuvutia na kuhamasisha ujasiriamali na uwekezaji miongoni mwa wananchi katika sekta ya nishati ya kupikia; 
§  Kuwezesha kuonekana kwa mawazo na fikra mpya za watu wengi wanaojishughulisha na kupunguza matumizi ya mkaa;
§  Kuweza kubaini makundi yanayojihusisha na ubunifu/ufumbuzi wa nishati endelevu ya kupikia na iwapo yanaweza kuunganishwa, kuwezeshwa au kuwekwa pamoja mnyororo wa thamani ya uzalishaji, usambazaji, uuzaji wa rejareja / jumla wa nishati ya kupikia.

Mshindi wa kwanza atapokea tuzo ya fedha ya shilingi Milioni Mia Tatu (300,000,000), mshindi wa pili atapokea Shilingi Milioni Mia Mbili (200,000,000) na mshindi wa tatu atapokea Shilingi Milioni Mia Moja (100,000,000). Zawadi hizo za fedha zitatumika tu kwa ajili ya kukuza na kuendeleza mtaji wa miradi/ufumbuzi iliyoshinda. Vilevile, washindi hawa watatu wa kwanza watapatiwa mafunzo ya biashara na uwekezaji kulingana na uvumbuzi wao na watatambulishwa kwa wawekezaji na/au kupelekwa zilipo fursa zaidi za uwekezaji au ubia, ndani na nje ya nchi, kwa ajili ya kupanua  na kuupeleka sokoni ubunifu wao. Mategemeo ni kwamba njia moja au njia zote zilizoshinda zitakuwa zimetoa ufumbuzi wa nishati mbadala ya kupikia nchini.

Tuzo zitatolewa kupitia mchakato wa wazi kwa tathmini mahiri ya jopo la wadau wa nishati, mazingira na wataalamu wa biashara kwa kipindi cha miezi sita. 
Kuhusu ubunifu unaohusisha matumizi endelevu ya mkaa, masuala yafuatayo yanaweza kuangaliwa, katika kuamua mshindi:
§  Usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu na upandaji miti;
§  Teknolojia bora za uzalishaji wa mkaa;
§  Vyanzo mbadala vya mkaa kama vile briketi,  au mkaa wa taka, nk.
§  Ubunifu katika mnyororo wa thamani ya mkaa, na
§  Utengenezaji na usambazaji wa majiko banifu na biashara ya mkaa.
Ubunifu/ufumbuzi utakaopokelewa kwa ajili ya kushindanishwa ni ule ambao tayari unatekelezwa au ambao upo kwenye majaribio kwa muda usiopungua miezi sita kuanzia tarehe ya kuwasilisha maombi ya kuingia kwenye shindano. Andiko/pendekezo, wazo au dhana ambayo bado iko kwenye makaratasi (paper proposal) haitafikiriwa kuingizwa kwenye shindano.
Wakati wa mchakato wa tathmini, jopo la thathmini linaweza kutembelea maeneo ubunifu unapotumika, kuomba vifaa vinavyotumika, kuhitaji kufanyika majaribio mara kadhaa, na kuhitaji maelezo mengine yoyote ya ziada kwa ajili ya kufanya tathmini kamili na sahihi na ya haki. 
Jinsi ya kushiriki: Waombaji watatakiwa kujaza fomu zitakazopatikana katika Ofisi ya Makamu wa Rais, iliyopo Mtaa wa Luthuli, jijini Dar es Salaam, au kupakuliwa kutoka tovuti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (www.vpo.go.tz) kuanzia tarehe 15 Disemba 2016. Vilevile, watatakiwa kuwasilisha andiko la ubunifu/ufumbuzi wao lenye kujibu maswali yafuatayo:-

    • Je, ubunifu/ufumbuzi huu unaweza kupanuliwa (scalability) na kutekelezwa, kuzalishwa na kuigwa katika maeneo mengi nchini? 
    • Je, ubunifu/ufumbuzi huu utaweza kuwa  endelevu na kutekelezwa kwa muda mrefu bila ukomo (sustainability)?
    • Je, ubunifu/ufumbuzi huu utaweza kutekelezwa/kupatikana nchi nzima, hasa kwa watu wa kipato cha chini?
    • Je, ubunifu/ufumbuzi huu utatoa unafuu wa gharama ya nishati ya kupikia kuliko mkaa? 
    • Je, ubunifu/ufumbuzi huu ni kwa namna gani unaweza kuwa biashara yenye faida (commercially viable) kwa mbunifu na mwekezaji?
    • Je, ubunifu/ufumbuzi huu utaweza kuwa na faida gani na kwa kiasi gani kwa mazingira na kijamii?
Imani yangu ni kwamba shindano hili litaendana na hatua nyingine za kisera za kudhibiti ukataji wa misitu, kulinda vyanzo vya maji, kuondoa umaskini wa nishati, na kuifanya bei ya mkaa itokane na thamani halisi ya miti iliyotumika kutengeneza mkaa huo.
Uchukuaji na urudishaji fomu za kushirikiki kwenye shindano, pamoja na mawasilisho ya maandiko, yatapokelewa kuanzia tarehe 15 Desemba 2016 hadi tarehe 31 Januari 2017. Tuzo kwa washindi zitatolewa mwezi Juni 2017. Mawasilisho yanaweza kuwa kwa lugha ya Kiingereza au Kiswahili na hakutatozwa ada kwa ajili ya fomu na mawasilisho.
Maelezo ya ziada ya shindano hili nitayatoa tarehe 29 Novemba 2016, katika kikao cha wadau wa mkaa nilichokiitisha siku hiyo. Katika kikao hicho pia nitatangaza Mshirika wa Sekta Binafsi katika shindano hili. 
Kwa ufanunuzi wa ziada, unaweza kuwasiliana nami kupitia:

Facebook: Ofisi ya Makamu wa Rais
Instagram: VPOTanzania
Twitter: VPOTanzania
Simu: 0685 333 444

January Makamba (MB.)
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira

10 Novemba 2016

No comments: