Thursday, November 10, 2016

Serikali yateuwa waratibu uwezeshaji wa wizara


Serekali imewataka Waratibu wa Uwezeshaji wa Wizara walioteuliwa kuwa watendaji makini ili kusaidia kamati zao za uwezeshaji wananchi kufuatilia kwa ukamilifu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya Mwaka 2004 na kuchangia kuandaa takwimu za uchumi wa taifa.
Akifungua mafunzo ya siku tatu ya Wenyeviti wa Kamati za Uwezeshaji na Waratibu wa Uwezeshaji, mjini hapa jana, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Anthony Mavunde, amesema kuwa sababu ya serekali kuwa na kamati na waratibu hao ni kupata watendaji wa kutumikia Watanzania kwa kuwawezesha, kuwasaidia kumiliki kikamilifu na kunufaika na uchumi wa taifa katika mazingira ya sasa.
Waziri huyo ameliita suala la uwezeshaji wananchi kuwa ni ajenda muhimu ya taifa na kutaka zikusanywe takwimu za kuridhisha juu ya ukuwaji wa uchumi katika miaka na jinsi wananchi wanavyonufaika na ukuwaji huo. Amesisitiza “..haitakuwa na maana kama ukuwaji wa uchumi hauwanufaishi  wananchi walio wengi na (pia kama) hazipo takwimu za kuridhisha za ukuaji wa chumi.”
Akisisitiza umuhimu wa ufuatiliaji, waziri amesema maeneo ya kupwewa kipaumbele ni kujua ni kiasi gani Watanzania wanashiriki na kunufaika kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa hapa nchini na makampuni ya kigeni katika sekta mbali mbali.
Amewataka watendaji kulisaidia taifa “kubainisha vikwazo au sababu zinazokwamisha Watanzania kushiriki katika uwekezaji, ikiwa ni pamoja kupata zabuni za kutoa huduma mbali mbali katika makampuni hayo na pia kupata nafasi za ajira.”
Bw Mavunde amesema serekali inafanya kazi kwa bidii kuleta maendeleo ya haraka kwa Watanzania. Na kuongeza kuwa kwa vile utekelezaji wa majukumu ya uwezeshaji unafanyawa na wadau wa sekta za umma na binafsi, matarajio ya serekali ni kuona kamati za uwezeshaji na madawati ya uwezeshaji katika wizara, idara, taasisi za serekali, mikoa na halmashauri zinafanya kazi kwa karibu na kila mudau.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bi. Beng’i Issa, amesema baraza linatarajia kila wizara, idara na taasisi ya serikali kutoa mchango wake katika kutekeleza sera ya uwezeshaji wananchi.
Amesema mafunzo yameandaliwa ili kuliwezesha baraza kupata maoni juu ya mambo wa msingi kwani washiriki watagusia makujumu na programu zinazotekelezwa na NEEC, mkakati wa uwezeshaji na mwongozo wa utekelezaji wake, wajibu na majukumu ya kamati na waratibu wa madawai ya uwezeshaji, miongozo ya kuwasilisha taarifa za uwezeshaji, mifuko ya uwezeshaji na programu za mitaji, ushiriki wa Watanzania kwenye uwekezaji (local content) na rasimu ya mapitio ya sera ya taifa ya uwezeshaji.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Elisante ole Gabriel, ambaye ni mshiriki amesema mafunzo yatawapa uwelewa mpana wa namna ya kuwahudumia wananchi katika wizara, hasa katika kutekeleza sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Mwenyewe, ameongeza, “nimejifunza mambo mengi sana leo. Nimefahamu kwa undani majukumu ya baraza na muundo wake.”

Baadhi ya Wenyeviti wa Kamati za Uwezeshaji na Waratibu wa Uwezeshaji wakifuatilia mafunzo ya siku tatu ya Wenyeviti wa Kamati za Uwezeshaji na Waratibu wa Uwezeshaji, mafunzo yenye lengo la kuwajengea uwezo wa uwelewa na wajibu wao katika Wizara, Idara na Taasisi wanazotoka, mafunzo hayo yalifunguliwa jana Mkoani Morogoro na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mh. Anthony Mavunde.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mh. Anthony Mavunde ((katikati) akisisitiza jambo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya Wenyeviti wa Kamati za Uwezeshaji na Waratibu wa Uwezeshaji, mafunzo yenye lengo la kuwajengea uwezo wa uwelewa na wajibu wao katika Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali wanazotoka (kulia) ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel, (kushoto) ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ( NEEC) Bi. Beng’i Issa.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mh. Anthony Mavunde (kushoto) akimsikiliza kwa makini ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel ( kulia) muda mfupi mara baada Naibu Waziri huyo fungua mafunzo ya siku tatu ya Wenyeviti wa Kamati za Uwezeshaji na Waratibu wa Uwezeshaji, mafunzo yenye lengo la kuwajengea uwezo wa uwelewa na wajibu wao katika Wizara, Idara na Taasisi wanazotoka, Morogoro jana, (katikati) ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ( NEEC) Bi. Beng’i Issa.

No comments: