Friday, November 25, 2016

SERIKALI YASHAURIWA KUANDAA SERA BORA KUKUZA UJASIRIAMALI NA UBUNIFU

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Uwekezaji,Profesa Adolf Mkenda (kushoto) akibadilishana mawazo na Meneja Mradi wa BEST-DIALOGUE, Bw.Hans Determeyer (katikati) wakati wa majadiliano yaliyohusu kuongeza kasi ya ubunifu na ukuaji wa wajasiriamali kupitia sera wezeshi zenye kutekelezeka na (kulia) ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF),Bw. Godfrey Simbeye. Picha na Mpiga picha wetu,Dar es Salaam.
Wadau wa masuala ya biashara wa ndani na nje ya nchi wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa majadiliano iliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Uwekezaji ,Profesa Adolf Mkenda (hayupo pichani), wakati wa majadiliano yaliyohusu kuongeza kasi ya ubunifu na ukuaji wa wajasiriamali kupitia sera wezeshi zenye kutekelezeka.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF),Bw. Godfrey Simbeye (kulia) akitoa taarifa juu ya maendeleo ya sekta binafsi nchini, wakati wa majadiliano yaliyohusu kuongeza kasi ya ubunifu na ukuaji wa wajasiriamali kupitia sera wezeshi zenye kutekelezeka, wa pili kulia Meneja Mradi wa BEST-DIALOGUE, Bw.Hans Determeyer , katikati ni Mkurugenzi wa Program ya Kimataifa ya SEPT,Profesa Utz Donberger, (wa pili kushoto) ni Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Uwekezaji ,Profesa Adolf Mkenda na kushoto ni Mkuu wa Kitivo cha Biashara Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS) ,Dk. Ulingeta Mbamba.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda (kulia) akifungua majadiliano yaliyohusu kuongeza kasi ya ubunifu na ukuaji wa wajasiriamali kupitia sera wezeshi zenye kutekelezeka, (wa pili kulia) Meneja Mradi wa BEST-DIALOGUE, Bw.Hans Determeyer , (katikati) ni Mkurugenzi wa Program ya Kimataifa ya SEPT, Profesa Utz Donberger, (wa pili kushoto) ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF),Bw. Godfrey Simbeye na (kushoto) ni Mkuu wa Kitivo cha Biashara Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS),Dk. Ulingeta Mbamba.


SERIKALI imeshauriwa kuweka  mazingira ambayo yatasaidia kuwa na sera bora na mifumo mizuri ya kisheria inayochangia kukuza sekta ya Ujasiriamali (SME) ambayo pia itaongeza  ajira, vipato vya wajasiriamali na taifa ili kupunguza umasikini katika jamii.

Akizungumza hayo jijini Dar es salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF),Bw. Godfrey Simbeye amesema kuwa serikali inahitajika kuweka mazingira yatakayo changia kuwa na sera ambayo inayolenga kukuza  kwa haraka sekta ya wajasirimali ili kukuza ajira, vipato vya wajasiriamali na pato la taifa na kupunguza umasikini katika jamii.

“Sera iliyopo ya mwaka 2003 ya kuendeleza ujasiriamali inahitaji kuboreshwa zaidi ili kwenda na wakati ili kukuza na kuimarisha maendeleo ya sekta hii” alisema Bw. Simbeye.

Aidha Bw. Simbeye alisema kwamba majadiliano hayo yaliwaleta wadau wa masuala ya biashara wa ndani na nje ya nchi  kama Kenya,Ghana, Uganda, Ujerumani, Uingereza,Ethiopia, Rwanda, Uholanzi, Taasisi za Biashara, wasomi na wajasirimali na wawakilishi kutoka UN kujadili namna ya kuwa na sera hiyo wezeshi.

Bw. Simbeye aliongeza kuwa Tanzania imejikiwekea mikakati ya kuelekea katika uchumi wa viwanda, hivyo serikali itambue kukuza vipaji vya wabunifu katika sekta ya uzalishaji na ujasiriamali wadogo na wa kati kwa kupewa motisha  ili waweze kuhamasika kuibua mawazo mapya.

 Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Uwekezaji Prof. Adolf Mkenda alisema  kuwa sekta ya ujasirimali ina mchango mkubwa kwa taifa, na serikali imekuwa karibu katika kuhakikisha inazidi kuimarika  na kutoa mchango mkubwa.

“Pamoja na mchango huu wa sekta hii pia tunatambua kuna changamoto mbalimbali ambazo kwa kushirikiana na wadau wa biashara tunaweza kuifanya sekta hii kuimarika zaidi na kuwa na mchango mkubwa kuliko ilivyo hivi sasa,” alisema Prof. Mkenda
Aidha Prof. Mkenda alisema serikali imeweka mazingira ambayo yanasaidia kukuza sekta hiyo ikiwemo  taasisi zote zinazohusika na masuala ya biashara zinafanya kazi ipasavyo kusaidia wajasiriamali wadogo na wakati kuzidi kukua.

Prof. Mkenda alisitiza kuwa serikali itaendelea kushishirikisha sekta hiyo ili kuhakikisha inafanya kazi kwa karibu kwani ndio injini ya uchumi wa nchi.

Naye Meneja Mradi wa BEST DIALOGUE,Bw. Hans Determeyer alisema maendeleo katika nchi yanakuja kwa sekta binafsi kuwa na nguvupamoja na kuweka mazingira wezeshi kati ya serikali na wafanyabiashara wenyewe.

“Majadiliano haya ni chachu kwa mataifa mbalimbali yaliyoshiriki katika kuweka mikakati inayowezesha kufikia malengo ya kiuchumi,” na kwa kufanya hivyo ni kusaidia kupunguza hali duni za vipato kwa wananchi na nchi kwa ujumla” alisema Bw.  Determeyer.

Kwa upande wake  Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Wakatoliki nchini Ghana,George Kafui Agbozo alisema nchi za Afrika ili ziweze kupiga hatua kiuchumi zinahitaji kuweka mazingira ya kukuza wajasiriamali wadogo na wakati.

“Changamoto za ukuzaji ujasirimali kwa nchi hizi za Afrika zinafanana hivyo ukikuza ujasiriamali kuna nafasi kubwa na kupunguza umasikini,”alisema Bw. Agbozo.

Majadiliano hayo yaliandaliwa na TPSF, Kituo cha Utafiti wa Sera na Utetezi (CPRA),Chuo Kikuu cha Dar es Salam Kitivo cha Biashara (UDBS),kwa kushirikiana na Mtandao wa Maarifa na Ubunifu Afrika (iN4iN) kwa ajili ya kupata njia bora za kuendesha ujasiriamali nchini.

No comments: