Shughuli ya uchimbaji na upakiaji wa makaa ya mawe
ikifanyika katika Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka uliopo kata ya Ruanda mkoani Ruvuma. Mgodi huo una
mashapo ya makaa ya mawe tani milioni
400.
|
Na Teresia Mhagama
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameendelea kusisitiza kuwa
Serikali haitatoa vibali kwa Viwanda nchini kununua madini ya Jasi na Makaa ya
Mawe nje ya nchi wakati Tanzania ina mashapo ya kutosha kukidhi mahitaji
wa viwanda hivyo.
Aliyaeleza
hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ya
makaa ya mawe katika mgodi wa Ngaka unaomilikiwa na kampuni ya TANCOAL
katika Kata ya Ruanda mkoani Ruvuma. 30
Katika
ziara hiyo Profesa Muhongo aliambatana na watendaji mbalimbali kutoka viwanda
vya simenti vinavyotumia makaa hayo ya mawe, Chama cha Wamiliki wa Malori
(TATOA), Wazalishaji wa Makaa ya Mawe, Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini
na viongozi kutoka Mkoa wa Ruvuma, wilaya ya Mbinga na Songea.
“Baadhi
viwanda vya simenti vimelalamika kuwa kuna upungufu wa makaa ya mawe, ndio
maana wadau wote tuko hapa ili kuhakiki je ni kweli kuna upungufu wa makaa ya
mawe au la,” alisema Profesa Muhongo.
Akijibu
suala la upungufu wa makaa wa mawe, Meneja wa TANCOAL, David Kamenya alisema
kuwa katika mgodi huo wa Ngaka, Makaa ya mawe yapo ya kutosha na kuna mashapo
Tani milioni 400 ambazo uchimbaji wake utafanyika kwa muda wa miaka 40.
Aliongeza
kuwa Mgodi huo pia una vifaa vya kutosha vya kuchimba madini hayo ili kuweza
kukidhi mahitaji ya wateja na kwa siku wanaweza kuzalisha makaa ya mawe tani
1200 hadi 1500 kulingana na mahitaji wanayopata ila kampuni ina uwezo wa
kuzalisha hadi tani 3000 siku.
Kuhusu
ubora wa makaa ya mawe, TANCOAL ilieleza kuwa makaa hayo yana ubora unaotakiwa
sawa na makaa ya mawe ambayo viwanda mbalimbali nchini vimekuwa vikiagiza
kutoka Afrika Kusini.
Katika
ziara hiyo kampuni za simenti za Tanga, Rhino na Lake zilikiri kuwa kuna
mashapo ya kutosha ya makaa ya mawe lakini changamoto iliyopo ni uwepo wa
magari ya kutosha na yanayofaa kusafirisha makaa hayo.
Kuhusu
Changamoto hiyo Profesa Muhongo alimtaka Mwenyekiti wa TATOA pamoja na
wanachama wake wenye magari yenye uwezo wa kusafirisha makaa hayo,
kukutana na watendaji wa viwanda vya Simenti, tarehe 15 Novemba, 2016 jijini
Dar es Salaam ili wenye viwanda hao wakague magari hayo na kuweza kufanya
maamuzi ya kuingia mikataba ya kutumia magari husika.
Aidha,
Profesa Muhongo alisema kuwa, lazima kuwe na mikataba kati ya
TANCOAL na viwanda vinavyohitaji makaa hayo ya mawe na endapo kampuni ya
TANCOAL itashindwa kuzalisha makaa ya mawe ya kutosha, kampuni hiyo ndiyo
itakayobeba lawama ya kushindwa kutekeleza mkataba wa kazi husika.
“Hivyo
hapa tumeshahitimisha kuwa makaa ya mawe yapo ya kutosha, hivyo mtu asithubutu
kuomba kibali cha kuagiza madini haya nje ya nchi, narudia uamuzi wa Serikali
ni kwamba, ruhusa haitatolewa kabisa, mtatumia makaa yanayozalishwa hapa
Tanzania,” alisema Profesa Muhongo.
Akitoa
uamuzi wa Serikali wa kuzuia uagizaji wa madini hayo nje ya nchi mwezi Agosti
mwaka huu, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani alisema kuwa
Hazina ya madini ya Jasi nchini ni zaidi ya Tani 300,000 na kuna tani zaidi ya
milioni 5 za makaa ya mawe ambazo zinatosheleza mahitaji ya nchi.
No comments:
Post a Comment