Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akiwa anatoka kwenye Wodi ya Sewahaji katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kurejea nyumbani mara baada ya kuruhusiwa baada ya kupata nafuu. Mama Janeth Magufuli alikuwa amelazwa hospitalini hapo tangu tarehe 9 Novemba 2016.
.................................................................................
Na.Alex Mathias.
Katika kipindi cha mwaka mmoja ambao serikali ya awamu ya tano chini ya mhe, Dr. John Pombe Magufuli imekaa madarakani, kuna mengi yaliyofanyika au yaliyowekewa mipango ya kufanyika hapo mbeleni na wananchi wengi kuonyesha kuridhishwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kwa ujumla wake.
Moja kati ya mambo ambayo yamewafanya wananchi wengi kufurahia na kujenga imani juu ya serikali ni uboreshaji wa hospitali ya rufaa ya Muhimbili ambayo imekuwa ni moja kati ya kero kubwa kwa miongo mingi na ilionekana kama vile ni jambo lisilowezekana kutatua kero hiyo.
Zipo kero ambazo zilihitaji serikali kuingilia kati kwa kuwa ziligusa bajeti kuu kwa mfano upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, fedha kwa ajili ya utafiti wa magonjwa mbalimbali na hata maslahi ya waganga na wauguzi pamoja na wafanyakazi wote wa taasisi hiyo ya afya.
Itakumbukwa kuwa kulikuwa na sakata la mashine za “MRI” na CIT Scan hii ikiwa ni siku chache tu baada ya Mhe, Rais kuingia madarakani, kama haitoshi suala la ununuzi na ufungaji wa vitanda katika hospitali hiyo kutokana na fedha zilizokuwa zitumike kwenye tafrija ya ufunguzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni baadhi ya hatua za mapema zilizochukuliwa kuboresha hospitali hiyo.
Lakini ni ukweli usiopingika kwamba vipo baadhi ya vitu ambavyo havihitaji serikali kuingilia kati ni suala la ubunifu na usimamizi wa uongozi wa hospitali hiyo na kila mmoja kutimiza majukumu yake katika kulijenga taifa kupitia maeneo yetu ya uwajibikaji.
Juma lililopita mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Janeth Magufuli alilazwa katika hospitali hiyo ya Rufaa na ilikuwa ni moja kati ya masuala yaliyogonga vichwa vya habari hapa nchini na kuzua mijadala mbalimbali ikiwemo kutozoeleka kwa viongozi wetu na familia zao kutibiwa katika hospitali za umma hapa nchini.
Lakini ninachotaka kukijadili hapa siyo suala la Mama Janeth kulazwa katika hospitali ya Rufaa Muhimbili, bali ni kile nilichokiona katika picha wakati Mama Janet Magufuli akitoka wodini baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini hapo ilinipa maswali mengi na muhimu yanayoanzisha majadala juu ya hatima yetu kama taifa kuufikia ustawi wetu.
Ukiangalia kwa makini katika picha ile inaonesha baadhi ya maeneo kama milango,madirisha, samani nk vikiwa vimeharibika bila ya kufanyiwa ukarabati wowote na hili linaleta shaka juu ya nani anapaswa kusimamia? Je! uongozi wa Muhimbili haujaona kama sisi wengine tunavyoona katika hii picha ? Au, hili nalo linahitaji Mhe, Rais na Waziri Mkuu ama Mawaziri wa wizara husika waingilie kati?
Hili ni suala ambalo halihitaji fedha za kigeni wala uchumi wa kati kwa kuwa ninaamini kipo kitengo cha ukarabati ambacho kina wafanyakazi wanaolipwa mshahara na serikali tena kuna wasimamizi walio juu yao ambao haya wanapaswa kuyaona na kuyafanyia kazi bila ya kuhitaji kusukumwa.
Kinachohitajika ni moyo wa kizalendo na kujituma huku tukiwa na mawazo ya kuijenga nchi yetu kwa kufanya tunayopaswa kufanya bila ya kuwa na shinikizo kutoka kwa walio juu yetu au manung’uniko kutoka kwa watumiaji wa huduma zetu, na hiyo itakuwa ni ishara ya kupenda tunachokifanya na zaidi kuipenda nchi nchi yetu.
Ili taifa lolote liweze kujengwa na kukua hadi kufikia malengo yaliyowekwa kunahitajika kuwe na moyo wa kujituma lakini pia kuwa na moyo wa kutimiza wajibu kila mtu mahali pake pa kazi pamoja na ubunifu huku kila mmoja akichukulia yote kama sehemu ya maisha yetu ya kila siku.
Hospitali ya taifa ya Muhimbili licha ya kuwa ni hospitali ya Rufaa lakini pia inatarajiwa kuwa mfano kwa hospitali zote nchini kwakuwa hii ndiyo kioo cha afya na utendaji wa viongozi katika sekta hiyo muhimu katika taifa letu. Hatupaswi kabisa kupuuzia hata kitu kidogo tu chenye viashiria vya uzembe kwakuwa chanzo cha madhara yoyote kwa kiasi kikubwa huwa ni uzembe.
Hapa kiukweli Uongozi wa Muhimbili haujawajibika vya kutosha kwani vitu vidogo kama hivi ambavyo vinatakiwa kukarabatiwa tu navyo mpaka Mh.Rais Dk. John Pombe Magufuli aje ?Mimi naamini kwamba kazi ya kuitunza Hospitali ya muhimbili kwa masuala ya ukarabati mdogomdogo sio jukumu la Serikali kuu bali ni Uongozi wa Hospitali hiyo.
Uongozi wa taasisi hii unapaswa kuliangalia hili kwa makini ili lisije likaharibu taswira ya mambo mema wanayoyafanya madaktari na watumishi wengine , lakini pia lisije likawa chanzo cha kuondoa uaminifu na weledi wao katika mambo mbalimbali wanayokusudia kuyafanya. Wakumbuke tu kwamba "Hiari Yashinda Utumwa"
No comments:
Post a Comment