Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo (aliyesimama) akiongea na madereva wa boda boda kuwaelezea mpango wa Serikali wa kuwapatia Pikipiki 200.
Nteghenjwa Hosseah
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo amekutana na waendesha
bodaboda wa Jiji la Arusha na kuwajulisha kuhusu mpango wa Serikali wa kuwakwamua
kiuchumi kwa kuwawezesha kupata Pikipiki bila Riba wala dhamana.
Rc Gambo amekuja na Mpango huu wa Kuinua uchumi wa Vijana kwa kuwapatia Pikipiki
baada ya kukutana na kundi hili la waendesha boda boda kwa mara na kusikiliza
malalamiko yao huku miongoni mwa kero yao kubwa ni kutozwa fedha nyingi na wamiliki
wa boda boda hizo.
Akiongea na waendesha boda boda Rc Gambo alisema ninaona jinsi mnavyojituma katika
kujitafutia riziki lakini hamthaminiki na kazi hii imekua ikidharaulika, sasa muda umefika
kwa kazi hii kuwa ya heshima mbele ya Jamii, kila kijana aliyepo katika biashara hii
ataweza kumiliki Pikipiki yake na sio kuendesha Pikipiki za watu ambao wamekuwa
wakiwanyonya kila siku kwa kuwatoza Fedha nyingi na wao kuzidi kuneemeka wakati
ninyi mnazidi kuwa masikini.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo (Katikati) akiwasili kwenye Kikao na waendesha bodaboda wa Jiji la Arusha.
“Kundi hili limekuwa likitumiwa kwa maslahi ya watu wachache kwa kuwa wamekuwa
wakipewa Pikipiki hizo kwa faidi kubwa na mmiliki anapokea Fedha zaidi yya mara mbili
ya bei ya kununulia Pikipiki hiyo ndipo aamue kummilikisha kijana pikipiki hiyo au aamue
kuendelea kupokea Fedha kwa kipindi chote wakati ninyi mnapata tabu barabarani huko
na mnaambulia Fedha kidogo kiasi ambacho hamuwezi fikia hatua ya kumiliki Pikipiki
zenu” Alisema Gambo.
Aliongeza kuwa Serikali ya Mkoa wa Arusha imeona ni vyema ikawajengea uwezo vijana
waliopo katika kazi hii kwa kuwapa mafunzo na kuwapatia Pikipiki ambazo mtatakiwa
kurejesha kiasi cha Fedha halali iliyonunuliwa Pikipiki hiyo kisha kumilikishwa chombo
bila ya riba yeyote wala dhamana.
Lucas Malusu ni dereva wa boda boda Kutoka Kata ya Elerai (aliyesimama katikati) akitoa maoni yake katika kikao chao na Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Aliendelea kusema utoaji wa Pikipiki hizi utazingatia Kata zote zilizopo katika Jiji la Arusha
ili Pikipiki ziweze kuwafikia walengwa na zoezi hili litaendelea kwa vijana wengine kadiri
ya mahitaji; Tutaongeza usimamizi kwa wote watakaopata Pikipiki hizi ili waweze
kurejesha Fedha kama inavyotakiwa na tuweze kuwanunulia vijana wengine hatimaye
tuwafikie vijana wote wenye uhitaji wa kumiliki na kufanya biashara ya bodaboda.
Serafini Shirima ni dereva wa boda boda Kata ya Levolosi akizungumza katika Kikao
hicho alisema kwa mara ya kwanza Katika Mkoa huu wamepata mlezi anayetambua na
kuthamini kazi ya boda boda na aliyethubutu kuwatafutia Pikipiki za bei nafuu ili kuongeza
kipato cha vijana wa Arusha.
Shirima alishauri kuundwa kwa kamati ya mpito itakayosimamia na kuratibu mchakato
mzima wa vijana watakaoanza kupewa Pikipiki hizo na kukamilisha taratibu zote za
uanzishaji wa umoja wa wandesha Boda boda utakaofahamika kwa jina la (UBOJA) chini ya
Mlezi Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Gambo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo (aliyesimama mbele) akihitimisha kikao chake na waendesha boda boda wa Wilaya ya Arusha.
RC Gambo alikamilisha Kikao hicho kwa kusimamia uchaguzi wa viongozi wa mpito kutoka
katika Kila Kata na hatimaye kupatikana viongozi watano watakaoratibu mpango wa awali
wa utoaji wa Pikipiki kwa vijana.
Pikipiki zitakazotolewa katika awamu ya kwanza ni 200 zikiwa na thamani ya Tsh Mil 400
na zitatolewa sanjari na Bima kubwa(Comprehensive Insurance) kwa vijana 200 ambapo
kila Kata itatakiwa kutoa vijana 8.
Vijana wa Arusha watakabidhiwa Pikipiki hizi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Kassimu Majaliwa tarehe 03/12/2016 kwenye uwanja wa Sheikh
Amri Abeid.
Baadhi ya waendesha boda boda wakifuatilia kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa
wa Arusha.
Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya Ndg. Polycarp Nkuyumba(aliyesimama)
akiwakaribisha viongozi na wadau kwenye Kikao na waendesha boda boda wa
Wilaya ya Arusha.
Serafini Shirima(aliyesimama) ni dereva wa boda boda kutoka Kata ya Levolosi
akichangia uanzishwaji wa umoja wa wandesha boda boda Wilaya ya Arusha
(UBOJA).
Viongozi wa mpito waliochanguliwa kusimamia taratibu za uanzishjwaji wa Umoja
huo pamoja na utoaji wa Pikipiki wa vijana nane wa Kila Kata.
No comments:
Post a Comment