Wednesday, November 2, 2016

Mwaka Mmoja wa Magufuli, Huduma Zaimarika Maradufu Muhimbili

Na John Stephen, MNH
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeimarisha nafasi yake ya kutoa huduma za afya kama hospitali ya taifa ili kupunguza rufaa za wagonjwa wanaokwenda nje ya nchi kutibiwa.
Muhimbili imejipanga kutoa huduma katika ubora wa hali ya juu na tayari imepeleka wataalamu wake nje ya nchi ili kujengewa uwezo wa kutoa huduma kwa wagonjwa.
Akizungumza na waandishi wa habari LEO, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Buberwa Aligaesha amesema Muhimbili imepeleka wataalamu 20 nchini India kwa ajili kujifunza upandikizaji figo pamoja na kutoa huduma bora kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo.
Aligaesha amesema madaktari na wataalamu wengine wamerejea kutoka India ambako walikwenda kujifunza upandikizaji wa vifaa kwa wagonjwa wenye matatizo ya masikio.
Utekelezaji Maagizo ya Rais John Pombe Magufuli
Amesema baada ya Rais John Pombe Magufuli kuingia Ikulu, alitembelea Muhimbili na kuagiza hospitali hiyo itengeneze mashini ya MRI na  kwamba agizo hilo lilitekelezwa kwa wakati.
“Baada ya mashini hiyo kutengenezwa ilifanya kazi vizuri na katika kipindi cha Disemba 2015 hadi Oktoba 2016 wagonjwa 17,951 walipatiwa vipimo vya MRI ukilinganisha na wagonjwa 1,911 waliopatiwa vipimo Disemba 2014 hadi Oktoba 2015. Hii ni sawa na asilimia 839.35,” amesema Aligaesha.
Aligaesha amesema pia mashini ya CT-Scan ilitengenezwa na kufanya kazi vizuri na katika kipindi cha Disemba 2015 hadi Oktoba 2016, wagonjwa 10,259 walipatiwa huduma ukilinganisha na wagonjwa 3,319 waliopimwa Disemba 2014 hadi Oktoba 2015. Amesema ongezeko hilo ni sawa  asilimia 209.09.
 “Kasi ya utoaji huduma za afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeongezeka maradufu kutokana na wafanyakazi kulipwa  stahili zao kwa wakati na kusababisha kuongezeka kwa vipimo vya radiolojia kwa asilimia 129.57,” amesema.
Huduma za Upasuaji
Aligaesha amesema leo kwamba kasi ya kufanya upasuaji imeongezeka na kwamba wagonjwa kati ya 40 hadi 50 kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa wanafanyiwa upasuaji.
“Katika kuongeza wigo wa wagonjwa wanaohitaji kufanyiwa upasuaji, hospitali inaongeza vyumba vya upasuaji saba kutoka 13 hadi 20. Katika upande wa ICU, vitanda vimeongezeka kutoka 21 vilivyopo sasa hadi kufikia 101 sawa na ongezeko la vitanda 80. Hii ni sawa na asilimia 67.3 ambalo ni takwa la Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO),” amesema Aligaesha.
Aligaesha amesema  hospitali imeboresha huduma za afya na kwamba katika kipindi cha Disemba 2015 hadi Oktoba 2016, wagonjwa 55,073 walipatiwa huduma za vipimo vya radilolojia ukilinganisha na wagonjwa 23,989 waliopimwa Disemba 2014 hadi Oktoba 2015.
Muhimbili Yalipa Malimbikizo
Amesema uongozi wa hospitali umeongeza kasi ya kupunguza kero za wafanyakazi na kwamba wamekuwa wakilipa malimbikizo ya madai ya wafayakazi ambayo walikuwa wakidai kwa kipindi kirefu.
 Aligaesha amesema kutokana na utekelezaji wa kutoa huduma bora kwa wagonjwa, hivi sasa wagonjwa wanapata dawa kwa zaidi ya asilimia 96 kutoka kwenye maduka ya dawa ya hospitali hiyo.
 “Tumeboresha mfumo wa Tehama katika utoaji na uagizaji dawa, na wagonjwa wanaokosa katika maduka yetu, Hospitali inanunua haraka ili mgonjwa huyo aweze kupata dawa. Hivi sasa ukosekanaji wa dawa Hospitalini umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na huduma kuimarika ndani ya Muhimbili. Kabla ya hapo upatikanaji wa dawa ulikuwa chini kwa asilimia 35 hadi 35, sasa mambo ni mazuri,” amesema Aligaesha.
Pia, hospitali imeongeza mapato kwa zaidi ya asilimia 100 baada ya kupunguza kero za wafanyakazi.
Katika hatua nyingine, hospitali hiyo imekuwa kwenye mikakati ya kupunguza matumizi kwa kununua dawa na vifaa tiba kutoka viwandani badala ya kununua madukani.
 “Kwa mfano, Hospitali imenunua dawa za figo (immunosuppressant) kutoka nchini India kwa Shilingi milioni 226 wakati hapa nchini zingegharimu Shilingi milioni 500,” amesema Aligaesha.

No comments: