Monday, November 7, 2016

Mama Mwanamema Shein aongea na Waumini wa Madhehebu ya dini ya Kikristo Chakechake, Pemba


Rajab Mkasaba, 
Ikulu Zanzibar
MKE wa Rais wa  Zanzibar Mama Mwanamwema Shein amewataka Waumini wa Madhehebu ya Kikristo wasichoke kuiombea nchi amani kwani bila ya amani hakuna maendeleo. 
Mama Mwanamwema Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Amali Vitongoji, Chake Chake Pemba katika mkutano maalum kati yake na Waumini wa Madhehebu ya dini ya Kikristo. 
Katika maelezo yake Mama Shein, alisema kuwa bila ya amani hakuna mafanikio na wala mwanaadamu hawezi hata kupata muda wa kumuwabudu Muumba wake, hivyo suala la amani halina mbadala. 
Alisema kuwa ni ukweli uliowazi kwamba amani inapotoweka, waathirika wakubwa kwa bahati mbaya ni akina mama na watoto hivyo aliwataka wananchi kutolipa nafasi jambo hilo kutokea kwani athari zake ni kubwa. 
Mama Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza waumini hao kwa kuwa wapenda amani na usalama wa nchi yao kwa kuiombea amani kabla ya uchaguzi na hadi sasa baada ya uchaguzi, bila ya kuchoka kama wanavyofanya waumini na wananchi wa dini nyengine ambao wanaitakia mema nchi hii. 
“Kwa mapenzi makubwa ya Mwenyezi Mungu amezisikia sala na dua tunazoziomba na anaendelea kutupa neema hii, ambayo katika sehemu nyengine duniani wanaitamani lakini wanaikosa”,alisema Mama Shein. 
Aidha, Mama Shein alitoa wito kwa waumini hao kutochoka kuiombea nchi amani na kuijenga kwa nguvu zao zote.
Mama Shein alitoa nasaha zake kwa akina mama wenzake na kuwataka kuepuka kushiriki kwenye jambo lolote linaloweza kuondoa amani na kutoa wito kwa jamii kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kuzungumza na watoto wao ili waepuke kutumika kwa malengo mabaya yanayoweza kuwaharibia maisha yao. 
“Vitabu vya dini vimetueleza juu ya kuwapenda, kuwaenzi na kuwatunza watoto wetu kwani watoto ni neema ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia, na hatuna budi kuonesha shukurani zetu kwake kwa kuwalea vyema ili waje watufae katika siku zijazo”,alisema Mama Shein. 
Aidha, Mama Shein aliwataka wazazi wenzake kupiga vita vitendo vya udhalilishaji kwa kutoa ripoti katika vyombo vya sheria na taasisi zinazohusika pale inapobainika matukio ya udhalilishaji. 
Mama Shein aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali yao iko imara na inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti vitendo vya udhalilishaji kupitia Taasisi, Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto pamoja na vyombo mbali mbali vya sheria. 
Sambamba na hayo, Mama Shein aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana bila ya kubaguana kwa kuzingatia mila, silka na utamaduni wa tangu enzi wa kuvumiliana na kuheshimiana kwani hiyo ni nguzo  muhimu ya kuendeleza amani na utulivu uliopo hapa nchini. 
Wakati wa mchakato wa Kampeni za Uchaguzi uliopita Mama Shein alikutana na Waumini hao ambapo aliwanasihi kuliombea taifa ili lizidi kuwa na amani na kuingia katika mchakato huo kwa salama na hatimae ndicho kilichotokea ambapo Mwenyezi Mungu ameivusha nchi salama na viongozi waliochaguliwa na wananchi wanaendelea kuyatekeleza majukumu yao kwa mafanikio makubwa. 
Nae Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Asha Balozi aliwaeleza waumini hao kuwa mkutano huo una lengo la kuwashukuru na kuwasalimia waumini hao kutokana ushiriki wao uliopelekea kufanyika kwa uchaguzi mkuu kwa salama na amani na hatimae Chama Cha Mapinduzi na viongozi wake kupata ushindi. 
Alisema kuwa mshikamano uliopo ndio uliowafikisha hapo huku akiwapa pole kwa changamoto mbali mbali walizopambana nazo katika kipindi cha uchaguzi na kuwapongeza kwa mshikamano wao huku akieleza kuwa dini zote zinahubiri amani na utulivu wala hakuna dini inayohubiri ugomvi na fujo. 
Mapema Mama Fatma Karume nae alitumia fursa hiyo kueleza uhusiano wa kihistoria uliokuwepo kati ya waumini wa dini ya kikristo na dini nyengine hapa nchini kwani waumini wote ni ndugu na walikuwa kitu kimoja katika kugombania uhuru wa Zanzibar na hatimae kufanyika Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 yaliyowaweka huru wanyonge wa nchi hii. 
Katika hafla hiyo, Mama  Shein alizindua Albamu ya Kwaya yenye jina la ‘Mungu Baba’ ambayo ina nyimbo 11 zikiwa katika mfumo wa sauti kutoka Kanisa la Redeemed Gospel lililopo Chake Chake Pemba, ambapo wanakwaya hao nao walipata fursa ya kutumbuiza baadhi ya nyimbo zao hizo. 
Nae Mwenyekiti  wa Umoja wa Wachungaji Pemba, kutoka Kanisa la Anglican Wete, Mchungaji Emanuel John Masoud alieleza kuwa mchakato wote wa uchaguzi umeenda salama na kila aliekuwa na haki ya kupiga kura alipata nafasi nzuri ya kupiga kura. 
Pia, Mchungaji Masoud alivipongeza vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama kwa kufanya kazi yao vizuri, iliyosaidia kuondoa hofu kwa wapenda amani wote na kuweka mashaka na woga kwa wale waliokusudia kuchafua amani ya nchi. 
Wachungaji hao walieleza kuwa dua, sala na maombezi ya kuiombea nchi, wananchi pamoja na viongozi wote hapa nchini kwao ni kitu kilichopewa kipaumbele katika ibada zao zote wanazofanya kila siku. 

Viongozi mbali mbali wa madhehebu ya dini ya kikristo walihudhuria katika hafla hiyo wakiwemo Wachungaji wa Makanisa yote ya Pemba na kutoa shukurani zao kwa Mama Shein kwa kwenda kuwashukuru kwa kushiriki uchaguzi uliokwenda kwa amani na utulivu na kuahidi kuendelea kuhubiri utii wa sheria bila shuruti sambamba na amani na utulivu kwani ni agizo la Mungu.

No comments: