Tuesday, November 22, 2016

MAKONDA AWATAKA WADAU WENGINE KUWEKEZA KATIKA SOKA ILI KUKUZA VIPAJI VYA VIJANA


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda, amefanya ziara kwenye Makao Makuu ya klabu ya Azam akiwa na lengo kuu la kuipongeza kutokana na juhudi kubwa wanazofanya za kuwekeza katika kukuza vipaji vya vijana na kutoa wito kwa watu wengine wenye uwezo kujitokeza, na kuiga mfano wa Azam ili kuwa na timu nyingi zenye ushindani na kuondoa migogoro kwenye soka la Tanzania.

Kwenye msafara huo, Makonda aliambatana baadhi ya viongozi wengine wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, alikofanya ziara tofauti kusikiliza kero za wananchi wa wilaya hiyo akiwa sambamba na Mkuu wa Wilaya hiyo, Felix Jackson Lyanivana na ugeni huo ulipokelewa na viongozi wa juu wa Azam FC, wakiongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, Makamu Mwenyekiti, Nassor Idrissa, Meneja wa timu, Phillip Alando, ambao katika kumalizia ziara hiyo waliweza kumtembeza kwenye maeneo mbalimbali yaliyofanyiwa uwekezaji ndani ya Azam Complex oliyopo Chamazi.

Akitoa neno lake kwenye ziara hiyo, Makonda alisema haina ubishi kuwa Azam ndiyo timu pekee iliyofanikiwa kuwekeza ipasavyo kwenye soka huku akidai kuwa timu hiyo imeshaanza kwa vitendo kutekeleza suala la kupunguza idadi ya vijana walioko mtaani wasiokuwa na dira wala matumaini, “Leo hii mnatuunga mkono zaidi kwa sababu ni kiwanja kimoja na ni timu moja ambayo kila mtu aliye kwenye mkoa wa Dar es Salaam anaizungumzia, katika suala zima la kupunguza idadi ya vijana walioko mtaani wasiokuwa na dira wala matumaini nyinyi Azam mmeshaanza kutekeleza kwa vitendo na watu wote hatuwezi kuajiriwa serikalini, haiwezekani leo serikali ikaajiri watu wote.

Watu wengine waige mfano wa Azam, watengeneze timu zao, watengeneze viwanja ili tuwe na watu wengi, tuwe na timu nyingi zenye ushindani na hata hii migogoro inayotokea Yanga na Simba, wenye hela zao wasihangaike kama wamegoma kukodishwa wafanye maamuzi ya kutengeneza timu zao ili na wenyewe waendelee kunufaika kwa sababu mwisho wa siku tunajua tukiwa na timu nyingi kama ilivyo Azam ushindani utakuwa mkubwa sana.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Azam FC, alimshukuru Makonda kwa ugeni wake huo ndani ya klabu hiyo, huku akichukua fursa hiyo pia kumwelezea historia fupi ya Azam tokea ianzishwe mwaka 2004 hadi ilipo mpaka sasa.

Mbali na historia, alimweleza timu mbalimbali zilizoko ndani ya Azam Complex, timu ya vijana (U-20) na ile ya wakubwa pamoja na mipango kabambe inayoendelea ya kuunda timu za vijana za chini ya umri wa miaka 15 na 17, mchakato unaoelekea ukingoni ukihusisha mikoa mbalimbali.

“Baada ya michuano ya Copa Coca Cola kutokuwa na mwelekeo, kama klabu tumeamua kuwafuata vijana kule walipo tumefanya majaribio katika mkoa wa Dar es Salaam, tumekwenda Zanzibar, Tanga, Morogoro na wiki iliyopita tulikuwa mkoani Mbeya tulikopata vijana saba, bado tutaendelea kufanya uwekezaji tutaenda mkoani Tabora, Mwanza, Kigoma na Mtwara,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Kwa hiyo sisi tunaamini ya kuwa hata Mheshimiwa hapa Mkuu wa Mkoa utakuwa ni miongoni mwa wadau wetu wakubwa wa kutusapoti na karibu sana Azam usichoke kuja wakati wowote. Yote tunayoyafanya ni kutokana na kampuni mama ya Azam na wadhamini wetu ambao ni Benki ya NMB lakini haitoshi kwa hiyo tunachukua fursa hii kuyaomba makampuni mengine ambayo yanaweza kuona nafasi ya wao kuwekeza waje, tuna timu za vijana, njooni mfanye kazi na sisi tuweze kusomba mbele.”
Makonda akisalimiana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul  Makao Makuu ya klabu ya Azam akiwa na lengo kuu la kuipongeza kutokana na juhudi kubwa wanazofanya za kuwekeza katika kukuza vipaji vya vijana
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda akionyesha jezi ya Azam aliyokabidhiwa na Ofisa Habari wa Azam Fc Jaffar Iddy wakati wa ziara yake aliyoifanya kwenye Makao Makuu ya Klabu hiyo leo Jijini Dar es salaam.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda(wa kwanza kushoto) akiongea na baadhi ya watendaji wa klabu ya Azam Fc wakati wa ziara yake aliyoifanya kwenye Makao Makuu ya Klabu hiyo leo Jijini Dar es salaam.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba (aliyesimama) akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Azam FC na kumshukuru Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda kwa ugeni wake huo wenye tija kwao.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda akiwa anatembelea maeneo mbalimbali ya Uwanja wa Azamuliopo Chamazi baada ya kufanya ziara leo Jijini Dar es salaam.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda akisalimiana na viongozi mbalimbali wa Azam Fc leo Jijini Dar es salaam.

No comments: