Klabu
ya Rotary ya Oyster Bay imeandaa kambi ya matibabu ya bure
itakayofanyika eneo la Kerege wilayani Bagamoyo. Huduma hizo za matibabu
zitatolewa siku ya Jumapili tarehe 27 Novemba katika shule ya Msingi ya
Kerege.
Timu
ya wataalamu wa afya kutoka Hospitali mbalimbali, wanafunzi wa
udaktari, wanachama wa Rotary na wafanyakazi wa kujitolea kutoka sekta
mbalimbali watashiriki katika kambi hiyo ya matibabu.
Vipimo
na matibabu yatatolewa kwa magonjwa kama malaria, upungufu wa damu,
kisukari na shinikizo la damu, masikio, pua na koo (ENT), magonjwa ya
ngozi, macho, meno na kansa ya kizazi kwa akina mama. Miwani zitatolewa
kwa watu watakaokutwa na matatizo ya macho. Huduma za ushauri kwa
wajawazito zitatolewa na wajawazito pia watapatiwa vifaa vya
kujifungulia bure.
Wakazi
wa Kerege na maeneo ya jirani wanaombwa kujitokeza kwa wingi na kutumia
fursa hiyo ya matibabu ya bure haswa akina mama na watoto.
Akizungumza
kuhusu mradi huu, Alfred Woiso, Rais wa Klabu ya Rotary ya Oyster Bay
alisema, “Tuna furaha kuandaa kambi hii kwa mara nyingine tena kwa
wakazi wa Kerege ambapo lengo letu ni kuwasaidia watu ambao hawana uwezo
wa kumudu gharama za matibabu. Tunawashukuru wadhamini na watu wote
wanaojitolea katika mradi huu na tunakaribisha watu kuhudhuria na
kusaidia kwa namna yoyote ile katika kambi hii ya matibabu.”
Usajili
wa matibabu utaanza mapema asubuhi na watu wapatao 1,200 wanatarajiwa
kupata huduma za matibabu kulingana na mwenendo wa idadi ya watu ambao
huwa wanajitokeza kila mwaka kambi hiyo inapofanyika. Wakazi wa Kerege
wanashauriwa kufika mapema ili kuweza kupata huduma.
Kambi
hiyo ya matibabu imedhaminiwa na Diamond Trust Bank na inaandaliwa kwa
ushirikiano na Shree Hindu Mandal Hospital, Vital Supplies, Whitedent,
vClick Concepts Inc, MAK Books and Brains, ABACUS Pharmaceuticals, Fazel
Foundation na wanachama wa Klabu ya Rotary na Rotaractor.
No comments:
Post a Comment