Na Hilali A. Ruhundwa- COSTECH
Serikali za Finland na Tanzania kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) zimekubaliana kuendeleza sekta ya ubunifu (innovation) kupitia mradi wa TANZIS utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 28 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwakani 2017.
Hayo yamebainika jana wakati Waziri wa Biashara za Nje na Maendeleo wa Finland Bw. Kai Mykkänen na ujumbe wake walipotembelea COSTECH katika maadhimisho ya kukamilika kwa mradi wa miaka mitano wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) uliojulikana kama The Information Society and ICT Sector Development Project in Tanzania (TANZICT).
Bw. Mykkänen alisema amefurahishwa na jinsi mradi wa kwanza ulivyofanikiwa kwa kuendeleza vijana wabunifu zaidi ya 5,000 chini ya kitengo cha ubunifu (Buni Innovation Hub) kinachosimamiwa na COSTECH.
Waziri wa Biashara za Nje na Maendeleo wa Finland Bw. Kai Mykkänen akielezea ushirikiano wa Finland na Tanzania katika kuendeleza Teknolojia na Ubunifu.
“Tunafurahi kwa ushirikiano huu wa Tanzania na Finland hasa katika kuendeleza sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano kwa vijana wabubifu wa kitanzania. TANZICT imefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Baada ya mradi huu, tunategemea kuwa na mradi mpya kuanzia mwaka kesho”. Alisema waziri huyo aliyeambatana na balozi wa nchi hiyo hapa nchini Pekka Hukka.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dr. Hassan Mshinda, alisema kutokana na tatizo la ukosefu wa ajira nchini, mradi huo ulijikita zaidi katika kuendeleza ubunifu wa vijana wanaohitimu vyuo vikuu na vyuo vishiriki katika kuwaendeleza na kuwajengea maarifa ili waweze kumudu soko la ushindani wa ajira.
Meneja wa Buni Innovation Hub Bw. Jumanne Mtambalike akiwasilisha mafanikio ya mradi wa TANZICT mbele ya ujumbe toka Finland.
“Katika mradi huu mpya utakaoanza mwaka kesho, utajikita zaidi katika sekta za viwanda, kilimo na afya lengo zaidi ikiwa ni kuimarisha uchumi wa nchi na kuongeza masoko ya bidhaa”. Aliongeza Dr. Mshinda.
Kwa upande wake Meneja wa BuniHub Bw. Jumanne Mtambalike, alisema mradi huo umekuwa mkombozi mkubwa kwa vijana wabunifu ambao umewawezesha wahitimu wa vyuo kuanzisha kampuni zao na kujiajiri.
Mwaka 2011 serikali za Tanzania na Finland zilisaini makubaliano ya ushirikano katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo COSTECH ilianzisha kitengo cha ubunifu kiitwacho Buni Innovation Hub lengo kuu likiwa ni kukuza sekta ya ubunifu (innovation) na kuinua vipaji vya vijana wa kitanzania.
Mkurugenzi wa kampuni ya Ubongo Kids Bi. Nisha Ligon akiwasilisha namna kampuni hiyo inavyotengeneza vipindi vya watoto kwa kutumia katuni vinavyorushwa na runinga mbalimbali.
Buni inafanya kazi kwa karibu sana na vijana wabunifu, wengi wao wakiwa wametokea katika vyuo vikuu na shirikishi vya hapa nchini, ambapo COSTECH chini ya mradi wa TANZICT wameweza kutoa mitaji kwa kampuni zaidi ya 46 na nyingi zikiwa na matokeo chanya katika jamii.
Mwaka 2015, kampuni mpya rasmi na zisizo rasmi 68 zilianzishwa chini ya mradi huu. Huduma 18 mpya ziliingizwa sokoni; mfano kampuni ya Ubongo Kids inayoshughulika na kutengeneza vipindi vya masomo ya shule kwa kutumia katuni, vipindi hivyo vinaoneshwa kwenye vituo vya runinga mbalimbali barani Afrika . Kwa hapa Tanzania vinachorushwa na TBC 1 na mpaka sasa vina watumiaji/watazamaji zaidi ya milioni tano.
Mafanikio mengine yaliyopatikana na mradi huu ni ufunguzi wa vituo mbalimbali vya ubunifu vikiwemo Rlabs Iringa, Mbeya Living Lab, Sengerema Living Lab na kituo kipya kilichofunguliwa hivi karibuni kiitwacho Kiota Hub kilichopo ndani ya chuo kikuu cha Iringa.
Mradi huo wa TANZIS utakaoanza mwaka kesho 2017, unatarajiwa kugharimu jumla ya Euro milioni 12 sawa na fedha za kitanzania zaidi ya shilingi bilioni 28 zitakazotolewa na serikali za nchi zote mbili, Tanzania na Finland.
Waziri wa Biashara za Nje na Maendeleo wa Finland Bw. Kai Mykkänen akitembelea maonesho ya baadhi ya mashine zilizotengenezwa na vijana wabunifu kupitia mradi wa TANZICT.
Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dr. Hassan Mshinda akiwa na ujumbe toka Finland wakifuatilia mawasilisho toka kwa vijana wabunifu (hawapo pichani).
No comments:
Post a Comment