Tuesday, November 15, 2016

DC HAPI AFUNGUA RASMI MAFUNZO YA UJASIRIAMALI KWA VIJANA WA KINONDONI


Na: Debora Charles

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe.Ally Hapi leo jumatatu tarehe 14/11/2015 amefungua rasmi mafunzo ya ujasiliamali kwa awamu ya kwanza.

Katika Uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya amewata Vijana kuondokana na mawazo ya kuajiriwa pindi wanapohitimu vyuo vya Elimu ya juu na hata wale wasio na elimu hiyo, bali wajikite kutumia fursa zilizopo kujiajiri jambo ambalo litawasaidia kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira na kujenga uchumi wao na wa taifa.

Hayo yamebainishwa leo na mkuu wa wilaya ya kinondoni, Ally Hapi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya ujasiliamali wilaya ya Kinondoni kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kubuni, kuanzisha na kusimamia biashara na miradi mbalimbali.

Hapi amesema kuwa hakuna serikali duniani yenye uwezo wa kuajiri watu wake wote wenye uwezo wa kufanya kazi kutokana na ufinyu wa nafasi za ajira kulinganisha na mahitaji halisi. Bali wanaweza kujenga maisha yao kwa kubadilisha fikra na kuamua kujiajiri katika vikundi.Amesema, kuwa jukumu la serikali ni kuwawekea sera, mikakati na mazingira mazuri kwa vijana ili waweze kujiari katika shughuli za ujasiriamali.

"Kazi tunayoifanya hapa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, ambayo inaeleza wazi jukumu la serikali ya awamu ya Tano katika kuwasaidia vijana wa elimu tofauti kujiajiri na kufanya shughuli za ujasiriamali katika vikundi. Tumeanza na awamu hii ya kwanza itakayonufaisha vijana elfu moja, na tutaendelea na awamu nyingine hadi tumalize vijana wote elfu kumi waliojiandikisha." 
Alisema Hapi.

Hata hivyo, DC Hapi amesema ameanzisha mafunzo hayo kwa nia ya kuwaondoa uwoga vijana na kuwajengea ujasiri na uthubutu katika kuamua kujiajiri kwani amebaini vijana wengi na hasa wanaohitimu vyuoni ni wazito na waoga kujiajiri, jambo ambalo ameeleza kuwa linatokana na mfumo wa elimu kujikita katika nadharia zaidi kuliko kuwaandaa vijana kifikra na kivitendo kuanzisha shughuli zao binafsi za kiuchumi.

"Rais wetu Dr. John Magufuli ameahidi kupitia Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kuwa mikopo itatolewa katika ngazi ya mitaa na vijijini ili kuwawezesha vijana kujiajiri katika vikundi. Sisi kama Kinondoni tumeamua kujiandaa kwanza kwa kutoa mafunzo kwa watu wetu. Ili wajue nidhamu ya kukopa, kulipa deni, kubuni wazo la biashara, kuanzisha na kusimamia biashara na kutumia fursa zilizopo kujenga uchumi wao.
Hatutaki vijana wetu wakope fedha hizo wakiwa hawajapata elimu ya kutosha kuwawezesha kufanya ujasiriamali wa kisasa. Matokeo yake fedha zitatolewa na zitashindwa kuleta matunda yaliyokusudiwa."
Alisema Mh. Hapi

Kwa upande wao vijana ambao wameanza mafunzo hayo leo wamemshukuru Mkuu huyo wa wilaya huku wakihaidi kuitumia elimu watakayopewa kujenga maisha yao na uchumi wa taifa.

Vijana wapatao 10,000 walijitokeza kuitikia wito wa kampeni iliyoanzishwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni mapema mwezi June ambao watapatiwa mafunzo ya ujasiriamali bure ili kujiandaa kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira nchini. Awamu hii ya mafunzo inajumuisha washiriki 1000 kwa uwakilishi kutoka kila kata katika kata 20 za Kinondoni.

Mafunzo hayo yamefunguliwa katika ukumbi wa king solomon Namanga jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka benki ya NMB, PPF, Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi NEEC n.k.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Ally Hapi akisalimiana na Mkufunzi wa Ujasiriamali Bi. Debora Charles (kushoto) wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wajasiriamali vijana wa Manispaa ya Kinondoni jana Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Ally Hapi akizungumza na vijana wajasiriamali wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wajasiriamali vijana wa Manispaa ya Kinondoni jana Jijini Dar es Salaam.
Mkufunzi wa Ujasiriamali Bi. Debora Charles akitoa mada wakati wa mafunzo ya wajasiriamali vijana kutoka Manispaa ya Kinondoni jana Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ujasiriamali kutoka Manispaa ya Kinondoni wakifuatilia mafunzo ya ujasiriamali wakati wa mafunzo hayo jana Jijini Dar es Salaam.

No comments: