Thursday, November 17, 2016

CCM Z'BAR YAIPA MAJUKUMU MAZITO UWT.

Na Is-haka Omar, Zanzibar.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar  kimewataka Viongozi na Watendaji wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake  CCM (UWT) Tanzania  kuongeza juhudi katika kuimarisha Chama ili kiweze kushinda na kuendelea  kuongoza dola katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Rai hiyo imetolewa na Katibu wa Idara ya Organazesheni Afisi Kuu Zanzibar, Nd. Haji Mkema wakati akizungumza na Watendaji wa Jumuiya hiyo kwa ngazi za Mikoa na Wilaya za Unguja Kichama katika ziara ya kuimarisha uhai wa Chama katika jumuiya hiyo.  

Alisema jumuiya hiyo inatakiwa kuandaa mapema mipango endelevu ya kuimarisha chama kwa kuongeza wanachama wapya ndani ya chama na Jumuiya  kwa lengo la kufanikisha ushindi wa CCM wa mwaka 2020.

Nd. Mkema alieleza kwamba lengo la ziara hiyo ni kuwakumbusha viongozi na watendaji wa UWT, majukumu ya msingi yanayotakiwa kufanyiwa kazi kwa haraka ili kuhakikisha CCM inaendelea kubaki na hadhi yake ya kusimamisha Dola inayojali misingi ya Demokrasia, Haki na utawala wa kisheria.

“ Chama Chetu kinajivunia kuwa na jumuiya imara ya Akina Mama ambayo imekuwa mstari wa mbele kutetea na kupigania maslahi ya CCM bila ya hofu katika mapambano ya Kisiasa nchini, na kupata ushindi wa kishindo unaotokana na ridhaa halali ya wananchi”., alisema Mkema na kusisitiza kuwa  Watendaji wa jumuiya hiyo wanatakiwa kutafuta ufumbuzi wa kudumu juu ya kasoro ndogo ndogo zilizomo katika jumuiya hiyo ili kuongeza ustawi wa CCM kisiasa nchini.

 Alisema kwamba Akina Mama ndio nyenzo muhimu ya kisiasa kwa chama hicho hivyo wanatakiwa kuendea na harakati za kujenga ushawishi kwa akina Mama wenzao waliopo katika makundi na vyama mbali mbali kujiunga na Chama hicho.

Aliwasihi Akina Mama hao kuhakikisha afisi za jumuiya hiyo kuanzia ngazi za Matawi hadi Taifa zinafanya kazi kwa mujibu wa Katiba ya jumuiya  na miongozo ya CCM ili kuongeza kasi za kiutendaji.

Katibu huyo aliwambia  Akina Mama  hao kwamba pamoja na kufanya kazi za kisiasa wanatakiwa kuwa mfano wa kuingwa katika kufanya tafti mbali mbali juu ya mifumo ya uendeshaji wa Sekta za Afya, Elimu, Miundombinu na Kilimo kwa lengo la kubaini changamoto zilizomo katika sekta hizo ili kuishauri serikali kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa sekta hizo.

Aliwashauri  Jumuiya hiyo kuwakumbusha Wanawake wenzao kuhakikisha wanawapa malezi bora na kufuatilia kwa karibu tabia za  watoto wao katika familia ili waweze kukuwa wakiwa katika maadili mema watakaoweza kushika nyadhifa za chama na serikali kwa uadilifu hapo baadae.

Alisisitiza Ushiriki  wa Wanawake katika harakati mbali mbali sio tu nafasi za kisiasa bali waelekeze nguvu na ushawishi wa maendeleo katika Vikundi vya Ujasiria Mali na Saccos kwa nia ya kupata fursa ya kujiajiri wenyewe ili waondokane na dhana ya kuwa tegemezi kwa Wanaume.

 Mapema Akimkaribisha Mgeni rasmi, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya  hiyo anayefanyia kazi zake Zanzibar, Bi. Tunu Juma Kondo aliipongeza CCM kwa kufanya ziara Maalum ya kukutana na watendaji na viongozi hao kwa lengo la kubadilishana mawazo yatakayosaidia kujenga ufanisi ndani ya chama.

Wakati huo huo Katibu  Mkema , alitembelea Vikundi Vitano (5) vya Ujasiria Mali vya Akina Mama wa UWT katika Majimbo Chumbuni na Jang’ombe na kuona kazi mbali mbali zikiwemo za mikono na kilimo zinazofanywa na wanawake hao kwa lengo la kujikomboa na umasikini.

Nao Akina Mama hao kwa nyakati tofauti  walizitaja changamoto zinazowakabili katika vikundi hivyo kuwa ni pamoja na ukosefu wa mafunzo, ukosefu wa ofisi, ukosefu wa soko la uhakika, upungufu wa mitaji pamoja wizi wa mazao yao.

No comments: