Monday, October 10, 2016

WAZIRI WA MAJI AFANYA ZIARA UKEREWE

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge akikagua mradi wa kituo cha kutibu maji taka kilichopo Hamkoko wilayani Ukerewe, mwenye fulana ya michirizi ni mhandisi mshauri wa mradi huo Mhandisi Edward Kazimoto na kushoto mwenye kofia ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella.Nyuma kushoto kwa waziri ni Mkurugenzi wa MWAUWASA Mhandisi Anthony Sanga. Picha Na Baltazar Mashaka.
Mhandisi mshauri wa mradi wa Usafi wa Mazingira Ziwa Victoria (LVWATSAN) mhandisi Edward Kazimoto kitoa ufafanuzi wa ramani (michoro) ya miundo mbinu ya chanzo cha Maji Nebuye na kituo cha kutibu maji taka cha Hamkoko kwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge (mbele) mwenye shati la mchanganyiko wa rangi.Kusjhoto mwenye suti ya rangi ya kahawia ni Mkurugenzi mtendaji wa Mwauwasa Mhandisi Anthony Sanga.
Mhandisi mshauri wa mradi wa Usafi wa Mazingira Ziwa Victoria (LVWATSAN) Ukerewe (kushoto)mhandisi Edward Kazimoto juzi akimwongoza Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge kukagua miundombinu ya chanzo cha maji Nebuye kushoto kwa waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Estomihn Chang'ah na kulia kwake ni Mkurugenzi wa Mwauwasa Mhandisi Anthony Sanga . Na Baltazar Mashaka
Waziri wa maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge akionyeshwa sehemu ya mabawa wa ya kupokelea maji kabla ya kutibiwa na kusafishwa kabla ya kusukumwa kwenye tanki la kuhifadhia maji katika chanzo cha Nebuye. Kutoka kulia wa pili ni Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Estomihn Chang'a. Na Baltazar Mashaka. 
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge akiangalia mitambo ya kusukuma maji katika chanzo cha Maji Nebuye wilayani Ukerewe juzi.kushoto ni mhandisi mshauri wa mradi wa Usafi wa Mazingira Ziwa Victoria (LVWATSAN) mhandisi Edward Kazimoto. Na Baltazar Mashaka

NA BALTAZAR MASHAKA,NANSIO UKEREWE

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amewakemea Watumishi wa umma wasiowajibika na wanaofanya kazi kwa mazoea kuwa watafute mlango wa kutokea kwa kuwa wamekuwa chanzo cha kufa kwa miradi mingi ya serikali.

Pia waziri huyo alisema hakuna maji ya bure na kuwataka wananchi Ukerewe kuchangia gharama za huduma ya maji watakayoyatumia baada ya kukamilika kwa mradi wa Maji Nansio ili uwe endelevu na kuwawezesha watu wengine wa serikali na binafsi kupata huduma hiyo.

Mhandisi Lwenge alisema juzi mjini Nansio Ukerewe alipozungumza na baadhi ya wananchi, wadau na watumishi wa idara za Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo mara baada ya kukagua chanzo cha maji Nebuye na kituo cha huduma ya majitaka Hamkoko.

“Mradi huu wa Maji Nansio na kituo cha maji taka ambao umegharimu bilioni 13 ni mzuri ni wa pekee nchini.Wengine watakuja kujifunza hapa na utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 8 za maji kwa siku licha ya changamoto ya uhaba wa wahandisi wa ujenzi, umeme na mitambo,” alisema Mhandisi Lwenge.

Waziri huyo wa Maji alisema serikali imedhamiria kuwa ifikapo mwaka 2020 asilimia 100 ya wananchi wa Ukerewe wapate maji safi na salama kwa maeneo mengine asilimia 85 na hivyo kazi ya mazoea imepitwa na wakati.

“ Tunalo deni kwa waliotuchagua baada ya kuona ilani inatekelezeka.Kazi ya mazoea imepitwa na wakati,watumishi ambao hawatawajibika watafute mlango wa kutokea kwa sababu miradi mingi ya serikali inakufa kutokana na watendaji kutowajibika.Tuutunze miradi huu uwe endelevu,”alisema Lwenge.

Waziri huyo wa maji alieleza kuwa majungu hayasaidii ila atakayefanya ya ovyo watu waseme kwani ili kuwekana sawa kuelekea kwenye maendeleo ya Wilaya ya Ukerewe na kuomba ushirikiano katika kuwaongoza wananchi walioipigia kura nyingi serikali ya CCM .

Alisema kuwa chama ( CCM ) kianze kuisimamia serikali ili irudi kwenye misingi kwa sababu inawajibika kwa wananchi kma hawachangii maendeleo katika maeneoe yao hapo kuna tatizo na lazima kiongozi wa hapo aulizwe.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Estomihn Chang’ah alisema mradi huo una manufaa makubwa kwa wananchi wa Nansio na wilaya hiyo na asilimia 70 watanufaika kwa kupata huduma ya maji safi na salama na inahitaji sh. milioni 533,600,000 ili Mamlaka ya Maji Nansio imudu kuuendesha.

Alieleza kuwa fedha hizo ni za nishati ya umeme wa kuendesha mitambo, manunuzi ya dawa ya kutibu maji,dira za maji,mabomba na viunganishi na mishahara ya watumishi watakaosimamia mradi huo kwa mwaka .

“Mradi huu ni mkubwa kulinganisha na uwezo wa sasa wa rasilimali fedha wa mamlaka, Serikali kupitia Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mwanza (MWAUWASA) tunaomba itupatie mtaji wa sh. 533,600,000 ,”alisema Chang’ah.
Aidha, mshauri wa mradi huo Mhandisi Edward Kazimoto alisema kuwa kasoro alizoelezwa waziri walishaziona na kuzirekebisha na kazi kubwa iliyobaki ni halmashauri kuwafungia wananchi dira za maji ili waanze kupata huduma hiyo.

Mradi huo wa Maji Nansio umefadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) pamoja na serikali kwa gharama ya Bilioni 13 na kutekelezwa na mkandarasi kampuni ya Angelique International Limited ya India.

No comments: