Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa mkandarasi wa Kampuni ya Chongqing Foreign Trade and Economic Cooperation (Group) kutoka China anayejenga barabara ya Tabora-Nyahua yenye urefu wa KM 85 alipokagua kipande cha barabara ya Tabora mjini chenye urefu wa KM 6, mkoani Tabora.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akipokea taarifa ya maendeleo ya mradi wa barabara ya Tabora-Nyahua kutoka kwa Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Tabora Eng. Damian Ndabalinze, alipokagua kipande cha barabara ya Tabora mjini chenye urefu wa KM 6.
Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Tabora Eng. Damian Ndabalinze, akionesha hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara ya Tabora- Sikonge (Usesula) yenye urefu wa KM 30 kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Tabora- Sikonge (Usesula) yenye urefu wa KM 30 ikiwa katika hatua ya awali ya ujenzi wake.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa mkandarasi wa kampuni ya Chongqing International Construction Corporation (CICO), kutoka China anayejenga barabara ya Tabora- Sikonge (Usesula) yenye urefu wa KM 30 alipokagua ujenzi wake.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa wiki mbili kwa mkandarasi wa Kampuni ya Chongqing International Construction Corporation (CICO), kutoka China anayejenga barabara ya Tabora- Sikonge (Usesula) yenye urefu wa kilometa 30 kuongeza vifaa vya ujenzi katika eneo la mradi na kuhakikisha ujenzi wake unatekelezwa kwa kasi na kukamilika kwa wakati.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo na kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wake profesa Mbarawa amemtaka Mkandarasi huyo kutumia kipindi cha muda wa ziada cha utekelezaji wa mradi huo kilichoongezwa kukamilisha.
“Siridhishwi na kasi unayoendelea nayo, kama hautatekeleza agizo hili haraka iwezekanavyo nitasitisha mkataba huu mara moja na usitegemee kupata mradi mwingine wa barabara nchini”, amesema Profesa Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa amesema kuwa ujenzi wa mradi huo uende sambamba na viwango bora vya barabara vilivyomo kwenye mkataba uliosainiwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa amekagua barabara ya Tabora – Nyahua yenye urefu wa kilometa 85 kipande cha barabara ya Tabora mjini chenye urefu wa kilometa 6 kinachojengwa na kampuni ya Chongqing Foreign Trade and Economic Cooperation (Group) kutoka China na kumtaka mkandarasi kukamilisha barabara hiyo ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.
“Mpaka mwezi Disemba nataka barabara hii iwe imekamilika kwa kiwango cha lami, wananchi wa eneo hili wamekuwa wakiisubiri kwa hamu, hivyo hakikisha unaikamilisha”, amesisitiza Prof Mbarawa.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Tabora Eng. Damian Ndabalinze amesema kuwa wakala utamsimamia mkandarasi na kuhakikisha vifaa vinaletwa katika eneo la mradi ndani ya mwezi huu.
Ameongeza kuwa mradi huo unaenda sambamba na ujenzi wa madaraja makubwa mawili na unagharimu zaidi ya Bilioni 28.
Kukamilika kwa ujenzi wa miradi hiyo miwili kutafungua fursa nyingi ikiwa ni pamoja na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa katika maeneo ya kati na Magharibi mwa nchi yetu.
Waziri Mbarawa yupo katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Tabora kukagua miundombinu ya barabara, uwanja wa ndege, reli na mawasiliano.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment