WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Waislamu watumie nyumba za ibada kuhubiri uislamu na misingi yake.
Ametoa wito huo leo mchana (Ijumaa, Oktoba 28, 2016) wakati akishiriki sala ya Ijumaa katika msikiti wa Nunge mjini Dodoma.
Amesema dini ya Kiislam inafundisha kwamba sala ndiyo msingi mkubwa unaopaswa kufuatwa na kila muumini hivyo ni lazima wafanye ibada kwa wakati.
“Nasisitiza kwamba wote tutumie muda wetu vizuri pamoja na mambo mengine tufanye ibada kwani dini inatuekeza kuwa sala ndiyo msingi mkubwa kwenye Uislamu. Tunayo kazi ya kuimarisha misingi ya dini kwa kutumia nyumba za ibada,” amesema.
Waziri Mkuu amesema Waislamu wana jukumu la kufundisha watoto wao na kuhakikisha wanakua kwenye imani na kujengeka katika maadili mema.
“Dini inajenga maadili mema kwa mtoto na hata mtu mzima. Pia dini inajenga misingi ya uvumilivu na inamuwezesha mtu kumtambua Mwenyezi Mungu. “Tuendelee kuwafundisha vijana wetu umuhimu wa kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya kidini ili wakikua waweze kuiendeleza kwa vizazi vijavyo,” amesema.
Waziri Mkuu ambaye ametumia fursa hiyo kujitambulisha kwa waumini wenzake wa mkoa wa Dodoma baada kuhamia rasmi, ameahidi kutoa ushirikiano kwao na pia amewaomba wampe ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
“Nimekuja kujitambulisha. Mimi ni kijana wenu, ndugu yenu. Nimekuja Dodoma rasmi nyumbani na kikazi. Naomba mnipokee na naamini katika kipindi chote nitakachokuwa hapa nitapata ushirikiano nanyi na pia nitawapa ushirikiano,” amesema.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliwaomba waumini hao wawaombee dua wanafunzi wa kidato cha nne ambao wanatarajia kuanza mitihani ya kuhitimu Novemba Mosi, mwaka huu ili waweze kufaulu.
Waziri Mkuu amewaomba waumini hao waendelea kuwaombea viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Rais Dk. John Magufuli ili waweze kutekeleza vizuri majukumu yao na kufikia malengo yanayotarajiwa na wananchi.
Aidha, Waziri Mkuu amechangia sh. milioni moja kwa ajili ya kuendeleza mradi wa ujenzi wa zahanati katika msikiti huo. Miradi inayojengwa na waumini wa msikiti huo kwa sasa ni zahanati, madarasa ya shule ya awali na shule ya ufundi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya Sala ya Ijumaa kwenye Msikiti wa Nunge mjini Dodoma Oktoba 28, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishiriki katika Dua ya kuwaombea wanafunzi wote wa Tanzania wanaotarajia kufanya mtihani wa Kidato cha Nne ili wafanye vizuri akiwa katika Sala ya Ijumaa kwenye Msikiti wa Nunge mjini Dodoma Oktoba 28, 2016.
Baadhi ya waumini wa dini ya Kiislam wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza baada ya sala ya Ijumaa kwenye Msikiti wa Nunge mjini Dodoma Oktoba 28, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na baadhi ya waumini wa dini ya Kiislam baada ya Sala ya Ijumaa kwenye msikiti wa Nunge mjini Dodoma Oktoba 28, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Meya wa manispaa ya Dodoma, Jafar Mwanyemba na Sheikh Shabaan Kitila baada ya Sala ya Ijumaa kwenye Msikiti wa Nunge mjini Dodoma Oktoba 28, 2016.
No comments:
Post a Comment