Thursday, October 20, 2016

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AFUNGUA MKUTANO WA 6 WA NSSF JIJINI ARUSHA, SERIKALI YAPUNGUZA DENI LA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali tayari imeshalipa sh. bilioni 722.7 kati ya sh. bilioni 964.2 za madeni ya michango ya jumla ambayo Serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii nchini. 
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Oktoba 20, 2016) wakati akifungua Mkutano wa Sita wa wadau wa NSSF ulioanza leo kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Arusha na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 600. 
Amesema sekta hiyo imekua kwa asilimia 15 kutoka sh. trilioni 8.9 mwaka 2015 hadi kufikia sh. trilioni 10.2 mwaka 2016. “Hadi kufikia Juni 2016, takwimu zinaonesha idadi ya wanachama imeongezeka na kufikia milioni 2.1. Rasilmali za mifuko zimefikia shilingi trilioni 10.28 na mafao yaliyolipwa kwa kipindi cha mwaka kinachoishia Juni 2016 ni shillingi trilioni 2.93. Michango ya wanachama kwa mwaka ni shilingi trilioni 2.15 uwekezaji katika nyanja mbalimbali umefikia kiasi cha shilingi trilioni 9.29,” ameongeza. 
Waziri Mkuu pia amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Prof. Godius Kahyarara awaandikie barua waajiri wote wanaodaiwa na shirika hilo na kuwataka wawasilishe fedha wanayodaiwa mara moja na wale ambao hawatalipa ndani muda utakaowekwa wafikishwe mahakamani na yeye apewe taarifa.

“Kumekuwepo na changamoto ya muda mrefu ya baadhi ya waajiri kutolipa michango kwa wakati hali inayoleta usumbufu mkubwa kwa wanachama hasa wanapofikia muda wa kustaafu. Suala hili halikubaliki, hivyo natoa maelekezo kwa waajiri wote nchini waheshimu sheria na wawasilishe michango yao kwa wakati,” amesisitiza. 
Mbali ya kuwabana waajiri, Waziri Mkuu pia amewataka wanunuzi wa nyumba za shirika hilo na wapangaji wote wanaodaiwa wakamilishe malipo yao na wasipofanya hivyo ndani ya muda uliopangwa wafikishwe mahakamani. 
“Nimeambiwa pia lipo tatizo la wadaiwa wa nyumba yaani wanunuzi na wapangaji. Suala hili lilitolewa maelekezo na Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu. Nataka nisisitize kuwa watu wote walionunua nyumba za NSSF na bado hawajakamilisha malipo na wale waliopanga lakini hawalipi kodi wanatakiwa kulipa haraka au wakabidhi nyumba hizo kwa NSSF ziuzwe kwa watu wengine, vinginevyo nao wafikishwe mahakamani.”

Akizungumzia utendaji wa shirika hilo, Waziri Mkuu amewapongeza viongozi wa shirika hilo na Bodi ya Wadhamini kwa uamuzi wake wa kuwekeza kwenye uzalishaji wa sukari nchini. Amesema kiwanda kitakachojengwa, kinatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 100,000 kwa Watanzania na hivyo kuongeza wanachama katika mfuko wa NSSF. 

Nimefurahishwa na uamuzi wa NSSF na PPF kuungana ili kukabiliana na tatizo la sukari nchini. Tumeelezwa hapa kuwa mashirika haya yatashirikiana kujenga Kiwanda cha Sukari kitakachozalisha tani 200,000 kwa mwaka. Kiwanda hicho kitajengwa katika eneo la Mkulazi lililopo mkoani Morogoro,” amesema. 
Mapemaakielezea utendaji wa shirika hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof. Godius Kahyarara alisema limeboresha mafao ya wanachama wake kutoka sh. 80,000 hadi sh. 100,000 kwa mwezi. 
Alisema limeanza kufanya upembuzi yakinifu wa kujenga nyumba za watumishi Dodoma ili kuendana na uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma. “Upembuzi bado unaendelea lakini tumeshabaini kuna uwezekano wa kujenga nyumba 200 hadi 300 mkoani Dodoma,” alisema.

Kuhusu uwekezaji kwenye ujenzi wa Daraja la Mwalimu Nyerere lililopo Kigamboni, Dar es Salaam, Prof. Kahyarara alisema uwekezaji huo unalipa kwa sababu makusanyo ya tozo kwa watumiaji yamefikia asilimia 109. “Tuna uhakika kwamba fedha tulizowekeza zitarudi,” amesisitiza.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amepokea msaada wa tani 45 za saruji ambazo ni sawa na mifuko 900 yenye thamani ya sh. milioni 15 kwa ajili ya waathirika wa tetememo la ardhi mkoani Kagera. Amepokea msaada huo kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Prof. Samuel Wangwe. 
Akiwasilisha msaada huo, Prof. Wangwe alisema wameguswa na tatizo lilitokea mkoani Kagera na wameamua kutoa mchango ili kusaidia juhudi za Serikali kukabiliana na maafa hayo. Pia alisema wamekamilisha ahadi yao ya madawati 6,000 yenye thamani ya sh. milioni 400 ambayo waliitoa awali. Waziri Mkuu aliwashukuru kwa misaada hiyo na kuwahakikishia kwamba itafikishwa kwa walengwa.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishiriki kuimba wimbo wa taifa kabla ya kufungua Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Oktoba 20, 2016. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama na  kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishiriki kuimba wimbo wa taifa kabla ya kufungua Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Oktoba 20, 2016. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama na  kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo. 
 Wabunge Aesh Hilaly  wa Sumbawanga Mjini na  Mohamed Mchengerwa wa Rufiji  wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majliwa wakati alipofungua Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSFmjini Arusha Oktoba 20, 2016. 

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama akizungumza   kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufungua Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Oktoba  20, 2016.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipiga makofi baada ya kupokea tani 45 za saruji  zenye thamani ya shilinigi milioni 15 zilizotolewa na NSSF  kabla ya kufungua  Mkutano wa  Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Oktoba 20, 2016. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Oktoba 20, 2016
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi, Meneja Mkuu wa Malipo wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Francis Mcharage cheti cha kuthamini michango   ya wafanyakazi wa shirika hilo kwa NSSF kila mwenzi  wakati alipofungua Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha  (AICC) Oktoba 20, 2016.  Watatu kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama na wapili kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Profesa Samuel Wangwe.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti  na Usimamizi wa Sekta  ya Hifadhi ya Jamii, Irene Isaka baada ya kufungua Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Oktoba 20, 2016. Kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde na kulia ni Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments: