Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dk. Juliana Pallangyo (kushoto) akifugua kongamano la nne linalohusu gesi na mafuta lililoambatana na maonesho , lililokutanisha wadau mbalimbali kutoka makampuni yanayohusika na utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi, vyuo vikuu, wizara na taasisi za serikali jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dk. Juliana Pallangyo (kushoto), akibadilishana mawazo na Kaimu Kamishna wa Nishati na Maendeleo ya Petroli, James Andilile (kulia) katika kongamano hilo
Kutoka kulia; mwakilishi kutoka Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), Profesa Abraham Temu, Kaimu Kamishna wa Nishati na Maendeleo ya Petroli, James Andilile na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dk. Juliana Pallangyo wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa katika kongamano hilo.
Washiriki kutoka makampuni yanayohusika na utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi, vyuo vikuu, wizara na taasisi za serikali wakifuatilia hotuba iliyokuwa inatolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dk. Juliana Pallangyo (hayupo pichani) katika kongamano hilo.
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Kapuulya Musomba (kushoto) akipokea tuzo kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dk. Juliana Pallangyo (kulia) kwa mchango wa shirika hilo katika kufanikisha kongamano hilo.
Mwakilishi kutoka Benki ya Standard Chartered, Thomas Bisonga (kushoto) akipokea tuzo kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dk. Juliana Pallangyo (kulia) kwa mchango wa benki hiyo katika kufanikisha kongamano hilo.
Mwakilishi kutoka kampuni inayojihusisha na ujenzi wa mabomba ya gesi kutoka China (kushoto) akipokea tuzo kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dk. Juliana Pallangyo (kulia) kwa mchango wa kampuni hiyo katika kufanikisha kongamano hilo.
Meneja Mawasiliano kutoka kampuni ya utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta nchini ya Statoil, Genevieve Kasanga (kushoto), akipokea tuzo kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dk. Juliana Pallangyo (kulia) kwa mchango wa kampuni hiyo katika kufanikisha kongamano hilo.
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Kapuulya Musomba akieleza jambo katika kongamano hilo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dk. Juliana Pallangyo (katikati waliokaa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya washiriki wa kongamano hilo.
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Kongamano la Nne linalohusu sekta ndogo ya mafuta na gesi lililoambatana na maonesho kuhusu sekta hiyo na kukutanisha Wadau mbalimbali ikiwemo Kampuni zinazojishughulisha na utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi, Vyuo Vikuu, Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali limeanza kufanyika jijini Dar es Saalaam.
Kongamano hilo lilifunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dk. Juliana Pallangyo ambapo aliwaeleza wadau hao kuwa, usimamizi madhubuti wa sekta ndogo ya gesi na mafuta utaleta mapinduzi makubwa kwenye ukuaji wa viwanda na kuiwezesha Tanzania kuingia kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Katika kongamano hilo linalofanyika kuanzia tarehe 20 – 21 Oktoba, 2016, Dk. Pallangyo alisema kuwa kutokana na kiasi kikubwa cha gesi kilichogunduliwa ambacho ni futi za ujazo trilioni 57.2, kampuni mbalimbali za kigeni zimeanza kujitokeza na kuwekeza katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo gesi imegunduliwa
Alisema kutokana na uwekezaji katika shughuli za gesi na mafuta, kumekuwepo na mabadiliko ya kiuchumi katika mikoa hiyo kama vile kuongezeka kwa fursa za ajira, malazi na utoaji wa huduma kwa wawekezaji.
Aliongeza kuwa ni vyema wananchi hususan wa maeneo hayo kujiandaa na uwekezaji mkubwa katika mikoa hiyo ambapo kwa sasa katika mikoa ya Lindi na Mtwara kunatarajiwa kujengwa viwanda vikubwa vya mbolea, vitakavyoleta neema katika mikoa hiyo.
Alisema katika kujiandaa na kasi ya ukuaji wa sekta za gesi na mafuta nchini serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunakuwepo na sera na sheria zitakazowezesha wazawa kuwa sehemu ya umiliki wa uchumi wa gesi na mafuta.
Alitaja mikakati mingine ni pamoja na uanzishwaji wa kozi zinazohusu masuala ya gesi na mafuta katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Aliongeza kuwa, Serikali imekuwa ikipeleka nje ya nchi kusomea masuala ya gesi na mafuta katika ngazi ya shahada ya uzamili (masters degree), wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi katika ngazi ya shahada.
“Lengo letu kama Serikali ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na wataalam wa kutosha watakaoshiriki katika uchumi wa gesi na mafuta kwa kuajiriwa kwenye makampuni yanayojihusisha na utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta,” alisema Dk. Pallangyo.
Wakati huo huo akizungumza katika kongamano hilo, mwakilishi kutoka Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), Profesa Abraham Temu alisema kuwa lengo la kongamano hilo lilikuwa ni kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu sekta za gesi na mafuta nchini.
Alisema mambo yatakayojadiliwa katika kongamano hilo ni pamoja na uelewa kuhusu sekta za gesi na mafuta, sera na sheria za mafuta na gesi, ushirikishwaji wa wazawa kwenye sekta za gesi na mafuta, changamoto na matumizi endelevu ya mafuta na gesi na rushwa.
Kongamano hilo liliandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)
No comments:
Post a Comment