Na Hussein Makame, NEC
Watanzania wengi hawaijui Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC), majukumu yake na miongozo inayoongoza uchaguzi, hali
inayosababisha manung’uniko mengi na upotoshaji kwa umma juu ya tume hiyo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani (pichani) wakati akitoa tathmini ya elimu
ya mpiga iliyotolewa hivi karibuni kwenye Mkutano Mkuu wa 32 wa Jumuiya ya
Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika wiki mbili zilizopita mjini Musoma.
Bw. Kailima alisema kutokana na hali hiyo, NEC
imeanza kutekeleza mkakati kabambe wa kutoa elimu ya mpiga kura kupitia njia
mbalimbali ikiwemo kushiriki kwenye maonesho na mikutano inayojumuisha wadau
muhimu wa uchaguzi.
Alisema kutokana na utekelezaji huo wa mkakati wa elimu
ya mpiga kura anaamini baada ya miaka mitano au kumi ijayo Watanzania
wataifahamu tume hiyo na kufanikisha chaguzi zijazo bila ya manung’uniko na kwa
mafanikio makubwa zaidi.
“Baada ya miaka 5 au 10 ijayo, tunategemea kwanza
watu wataijua Tume ya Taifa ya Uchaguzi
kwa sababu bila kumung’unya maneno watu hawaijui Tume ndio maana wanauliza “hivi
baada ya uchaguzi nyinyi tume mnafanya nini” alisema Bw. Kailima na kuongeza
kuwa:
“Sasa wakiijuia Tume na ule uhalali wake, uiaminifu
wa wananchi kwa NEC utaongezeka kwa kiwango kikubwa sana, manung’uniko kwamba
tume haitimizi wajibu wake yatapungua kwa kiwango kikubwa ”
“Pili ule upotoshaji itapungua kwa sababu wananchi
watakuwa wameelewa kwa kiwango fulani kuhusu Tume, taratibu za uchaguzi na wakishaelewa
wewe ukienda na jambo lako watakushangaa.”
Alisema iwapo Watanzania watapata elimu ya mpiga
kura na kuizingatia hata uchaguzi wa mwaka 2020 utakuwa mzuri kwa sababu kila
atakayeshiriki atakuwa na uelewa wa kiwango cha juu kuhusu uchaguzi na maswali kawaida
yatakwisha kabisa.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, anaamini watu
wakielimika pia mvurugano zitapungua katika mchakato wa kupiga kura, kuhesabu kura, kujumlisha kura
na kutangaza matokeo kwani kila mtu atakuwa anajua taratibu zinazoongoza
mchakato huo.
“Hata zile kelele za kusema tunakaa mita 200 au
mita 300 hazitakuwepo kwa sababu kila mtu atakuwa amefahamu kumbe hata kama nisipokaa
huu ni utaratibu kwa hiyo mambo yatakwenda vizuri”alisisitoza Bw. Kailima.
Akitoa tathmini ya mkutano wa ALAT, Bw. Kailima
alisema washiriki wengi wa mkutano huo wanahitaji kueleweshwa mambo mbalimbali
kuhusu uchaguzi na tume inayosimamia na kuratibu uchaguzi huo.
“Kuna maswali ambayo yaliulizwa pale ambayo kwa
mtendaji ambaye ni mzoefu asingeweza kuuliza maswali ya namna ile, ni maswali
ambayo yako wazi ikiwemo kuhusu fomu ya kutoa matokeo namba 21 (a) na (b)”
alisema Bw. Kailima.
Hivyo alionesha kuwa kunahitajika kiwango cha juu cha
elimu ya mpiga kura kwa watendaji na wenyeviti wa halmashauri na wagombea kwa
ujumla.
Aliongeza kuwa amegundua pia kwamba watu wana
shauku kubwa ya kujua mambo mbalimbali kuhusu uchaguzi na tume huku akikiri
baadhi yao kudhani kama Tume inachelewa kutoa elimu na wengine wakistaajabishwa
na Tume kuwepo kwenye mkutano huo.
Bw. Kailima alisema jambo lilionesha sura tofauti
na aliyoizoea ni kuona washiriki wa mkutano huo kuwa na umoja bila ya kuonesha
kwa tofauti za vyama.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na kutoa
elimu ya mpiga kura katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye shule za sekondari
na maonesho na hivi karibuni inategemea kushiriki kwenye utoaji elimu katika
maeneo mengine nchini.
No comments:
Post a Comment