Saturday, October 15, 2016

Wasanii wa Muziki wa Singeli waaswa kuzingatia mafunzo ya sanaa ya ujasiliamali

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bi.Joyce Hagu akifafanua jambo wakati wa ufunguzi wa semina ya wasanii wa muziki wa singeli jana Jijini Dar es Salaam,kulia ni Meneja Mkuu wa EFM Bw.Denis Ssebo na kushoto ni Mkurugenzi wa EFM Bw. Francis Ciza. 

Mkuu wa Matukio ya Sanaa wa Baraza la Sanaa la Taifa(BASATA),Bw.Kuwijira Maregesi akiongea na waasanii kuhusu maadili ya utunzi wa mashairi wa nyimbo zao wakati wa ufunguzi wa semina ya wasanii wa muziki wa singeli iliyoandaliwa na uongozi wa Radio ya EFM jana Jijini Dar es Salaam kushoto ni Afisa Sanaa Bi. Bona Masenge na kulia ni Mkurugenzi wa Radio EFM Bw.Francis Ciza. 
Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),Bw.Innocent Mungi akiwasisitiza wasanii (hawapo katika picha) matumizi sahii ya mitandao ya kijamii wakati wa semina ya wanamuziki wa singeli iliyoandaliwa na uongozi wa Radio ya EFM jana Jijini Dar es Salaam. 
Meneja Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bibi.Valentina Baltaz akiongea kuhusu umuhimu wa wasanii kulipa kodi kupitia kazi zao za sanaa ili kuchangia pato la taifa wakati wa semina la wasanii wa muziki wa singeli iliyoandaliwa na uongozi wa Radio ya EFM jana Jijini Dar es Salaam kulia ni Mhariri Mkuu wa EFM Bi.Scholastica Mazula. 
Afisa Sanaa kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bi.Bona Masenge akiongea na wasanii(Hawapo katika Picha) kwa kuwataka kutunza na kuendeleza utamaduni wa kitanzania kwa kufuata taratibu na sheria katika kazi zao za sanaa wakati wa semina ya wasanii wa muziki wa singeli leo Jijini Dar es Salaam, kushoto ni Meneja Mawasiliano wa Taasisi ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),Bw.Innocent Mungi na kulia ni Mkuu wa Matukio ya Sanaa wa Baraza la Sanaa la Taifa(BASATA),Bw.Kurwijira Maregesi 
Baadhi ya Wasanii wa Muziki wa Singeli waliohudhuria semina iliyoandaliwa na uongozi wa radio EFM kwa lengo la kuwapata somo la kuifanya sanaa kuwa ujasiliamali ikiwemo kupata mbinu mbalimbali za uwekezaji . 
Baadhi ya Wasanii wa Muziki wa Singeli waliohudhuria semina iliyoandaliwa na uongozi wa radio EFM kwa lengo la kuwapata somo la kuifanya sanaa kuwa ujasiliamali ikiwemo kupata mbinu mbalimbali za uwekezaji . 
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa wa Wizara ya Habari Utamaduni,Sanaa na Michezo Bi.Joyce Hagu(wa tano kutoka kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wasanii wa muziki wa singeli baada ya semina iliyokuwa imeandaliwa na uongozi wa Radio EFM jana Jijini Dar es Salaam. Picha na Lorietha Laurence 


Na Lorietha Laurence-WHUSM 

Wasanii wa Muziki wa Singeli wameaswa kuzingatia mafunzo ya sanaa ya ujasiliamali yatakayowasaidia kuongeza weledi na mbinu za kukuza kazi zao na hatimaye kuwa na sanaa bora kwa ukanda wa Afrika Mashariki. 

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa wa Wizara ya Habari Utamaduni,Sanaa na Michezo Bi.Joyce Hagu wakati wa ufunguzi wa semina ya wasanii wa muziki wa singeli jana Jijini Dar es Salaam. 

Bi Joyce aliongeza kwa kusema kuwa sanaa ya muziki ni kazi kama kazi nyingine hivyo ni budi kusimamia misingi iliyo bora inayoendana na utamaduni wa kitanzania katika utunzi wa tungo za singeli. 

“Utamaduni ni mali ya jamii hivyo ni jukumu letu sote kupenda,kuthamini na kuendeleza utamaduni wetu kupitia kazi za sanaa na hii itasaidia kutekeleza kwa vitendo Sera ya Taifa ya Utamaduni” alisema Bi.Joyce. 

Aidha aliupongeza uongozi wa EFM kwa kuandaa semina hiyo ambayo imewapa fursa wasanii kupata elimu ya msingi kuhusu muziki na kuifanya kazi ya sanaa kuwa ya thamani kwa jamii. 

Naye Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),Bw.Innocent Mungi amewataka wasanii hao kutumia vizuri mitandao ya kijamii kwa kuuza kazi zao za mziki na hivyo kuwa na soko la kimataifa na sio kutumia mitandao kwa ajili ya kuchafuana. 

Kwa Upande wake Mkuu wa Matukio ya Sanaa wa Baraza la Sanaa la Taifa(BASATA),Bw.Kuwijira Maregesi amewakumbusha wasanii hao umuhimu wa kuzingatia maadili pale wanapofanya utunzi wa nyimbo zao ili kuepuka usumbufu wa kufungiwa. 

Mbali na mada ya maadili wasanii walipata fursa ya elimu ya mlipa kodi kutoka kwa Meneja Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bibi.Valentina Baltaz ambapo aliwaeleza wasanii umuhimu wa kulipa kodi kupitia kazi zao za sanaa kulingana na sheria na taratibu za nchi ili kuchangia katika kukuza pato la taifa.

No comments: