Friday, October 7, 2016

Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekeleawa na TASAF kisiwani Pemba waipongeza Serikali.


    Mmoja wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini katika shehia ya Ndagoni kisiwani Pemba akitoa maelezo kwa baadhi ya wadau wa maendeleo waliotembelea eneo hilo kuona utekelezaji wa shughuli za Mpango.
   Mmoja wa wadau wa maendeleo kutoka Benki ya Dunia Bwana Salazar  Manuel (mwenye miwani) akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika shehia ya Ndagoni( hawapo pichani). 

 
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bwana Ladislaus Mwamanga (aliyeshika kitabu) akiwa na baadhi ya wadau wa maendeleo wakipata maelezo kutoka  Kwa Mratibu wa shughuli za TASAF huko Zanzibar juu ya upandaji wa mikoko ikiwa ni hifadhi ya mazingira  na ujenzi wa kinga maji katika shehia ya Ndagoni uliofanywa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia utaratibu wa ajira ya muda..

Estom Sanga- TASAF
Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF wamepongeza hatua ya serikali ya kubuni Mpango huo ambao wamesema umeanza kubadili maisha yao kwa kuwajengea msingi imara wa kujitegemea na kuboresha maisha yao.

Wakizungumza na ujumbe wa maafisa wa serikali, wadau wa maendeleo na viongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii waliotembelea shehia ya Ndagoni na Shidi kisiwani Pemba, Walengwa wa Mpango huo wameeleza kuwa tangu waanze kupata ruzuku ya fedha kupitia utaratibu wa uhawilishaji fedha wameimarisha uwezo wao wa kugharamia lishe,elimu na afya kwa watoto wao huku wengi wao wakianzisha shughuli za ufugaji wa kuku na biashara ndogo ndogo ambazo huwaongezea kipato.

”Tunaishukuru serikali yetu kwa kutukumbuka sisi wananchi wa hali ya chini ambao wengi wetu tulikuwa tumekata tamaa ya maisha lakini baada ya utaratibu huu, alhamulah, hali zetu zimeanza kutononeka” alisema mmoja wa walengwa Bi. Mwanaidi Suleiman Abdallah.

Licha ya kupata ruzuku ya fedha ,Walengwa hao kupitia Mpango wa Ajira za Muda, PWP ambao pia hutekelezwa chini ya Mpango wa Kunusuru kaya maskini katika shehia ya Ndagoni wameweza kuibua na kutekeleza miradi miwili ikiwemo ujenzi wa tuta la kuzuia maji chumvi na kupanda mikoko kazi ambazo zimewawezesha kuongeza eneo la kilimo cha mpunga ambalo lilikuwa limathiriwa na maji ya bahari .

Aidha walengwa hao wamewaambia wadau hao wa maendeleo kuwa, kumekuwa na mwitikio wa kuridhisha wa mahudhurio ya watoto shuleni hususani kutoka kaya maskini ambao chini ya utaratibu wa Mpango wa Kunusuru kaya maskini mahudhurio yao ni moja ya masharti ya kupataruzuku kupitia TASAF.

Wakizungumza na walengwa wadau wa maendeleo waliotembelea shehia ya Ndagoni na Shidi wamepongeza hatua iliyofikiwa katika kuzihudumia kaya za walengwa na kuridhishwa na mwamko ulioonyeshwa na walengwa hao katika kutumia fedha za ruzuku vizuri hususani kwa kubuni miradi midogo midogo ikiwemo ususi wa vikapu, mikeka na kutengeneza manukato na sabuni.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bwana Ladislaus Mwamanga amesema serikali inaendelea kutekeleza wajibu wake kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kwa kutoa fedha za ruzuku ambapo hadi mwezi huu wa Octoba mizunguko 17 imekwishatolewa na kuwataka walengwa hao kuzitumia vema fedha hizo ili waweze kuboresha maisha yao na kuondokana na umaskini uliokithiri. 

Wadau wa maendeleo kutoka taasisi mbalimbali zinazochangia Mpango wa Kunusuru Kaya maskini wametembelea maeneo ya Pemba,Mbarali,Mkalama,Muheza na Chato kuona Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unavyotekelezwa na namna walengwa wanavyonufaika na Mpango huo kwa kuwatembelea na kuona shughuli wanazozifanya kwenye maeneo yao.

No comments: