Kaimu Afisa Habari na Mawasiliano ambaye pia Ofisa Misitu Mkuu wa
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Nurdin chamuya (Kushoto)
akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) Jijiji Dar es Salaam
jana kuhusiana na kukamatwa kwa lori lenye namba za usajili T676 ANQ
lililokuwa linasafirisha mbao kinyume cha sheria kutoka Mkoani Kigoma
kuja Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Afisa wa Himasheria wa Wakala huyo,
Arjason Mloge.
Kaimu
Afisa Habari na Mawasiliano ambaye pia Ofisa Misitu Mkuu wa Wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania, Nurdin chamuya (Kushoto) na Afisa wa Himasheria wa Wakala huyo, Arjason Mloge wakionesha sehemu ya mbao zilizokuwa zimefunikwa na katoni za sabuni ndani ya lori
lenye namba za usajili T676 ANQ lililokuwa linasafirisha mbao hizo
kinyume cha sheria kutoka Mkoani Kigoma kuja Jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa sehemu ya mbao hizo zikiwa zimefunikwa na sabuni ndani ya lori hilo.
Maofisa wa kikosi Dhidi ya Ujangili kanda ya Dar es Salaam na kikosi cha Kufuatilia na Kuzuia Uharibifu wa Misitu cha Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania wakitumia mbwa maalum wa kunusa (Sniffer Dog) kwa ajili ya kutambua bidhaa haramu ndani ya lori hilo.
Muonekano wa nje wa Lori hilo.
______________Na Hamza Temba - WMU________________
Kikosi cha Kufuatilia na
Kuzuia Uharibifu wa Misitu cha Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwa
kushirikiana na Kikosi Dhidi ya Ujangili kanda ya Dar es Salaam kimefanikiwa
kukamata lori lenye namba za usajili T 676 ANQ lililokuwa likisafirisha mbao kinyume
cha sheria huku zikiwa zimefichwa kwa kufunikwa na bidhaa mbalimbali ikiwemo sabuni
ili zisionekane kiurahisi kwenye vituo vya ukaguzi.
Akizungumza na waandishi wa
habari Jijini Dar es Salaam leo, Kaimu Afisa Habari wa Wakala huyo, Nurdin
Chamuya alisema tukio hilo limetokea tarehe 14 Oktoba, 2016 majira ya saa kumi
usiku maeneo ya Amana, Ilala Jijini Dar es Salaam baada ya kupata taarifa
kutoka kwa raia wema juu ya uwepo lori hilo katika maeneo hayo.
Chamuya alisema baada ya
kupata taarifa hizo vikosi hivyo vilifika eneo la tukio na kufanya mahojiano na
baadhi ya wananchi waliokuwa karibu na lori hilo ambapo mmoja kati ya wahudumu
wa lori hilo alieleza kuwa lori hilo lilitokea Mkoani Kigoma na kwamba lilikuwa
limepakia mzigo wa sabuni na chupa za maji zilizotumika. Dereva wa lori hilo
hakuweza kupatikana.
“Wahudumu
hao walipotakiwa kufungua mlango wa lori hilo kwa ajili ya upekuzi zaidi walisita
kwa madai kuwa hawakuwa na funguo za lori hilo, Hatimaye waliwasiliana na mmlikiwa wa eneo ambaye
alikuwa amekabidhiwa funguo kwa ajili ya ulinzi” alisema Chamuya.
Alieleza
kuwa mmiliki huyo alipofika alisema, anamfahamu mwenye gari ambaye ndiye
mpangaji wa eneo lilipokutwa gari na kwamba anazo taarifa za gari hilo,
na ameombwa apokee mzigo na kuutunza hadi atakaporudi kutoka safari
ya Mwanza kwa tatizo la msiba wa Baba
yake.
Baada
ya mmiliki wa eneo hilo kufanya mawasiliano na mwenye gari kuhusu mzigo
uliokuwa kwenye gari hilo, mwenye gari alieleza kuwa kwa taarifa za dereva wake
na ajenti aliyepakia mzigo Kigoma, gari lake lilikuwa na chupa chakavu na
sabuni kutoka Kigoma na hakuna aina nyingine ya mzigo kwa ufahamu wake na
akaruhusu gari hilo kufunguliwa mbele ya mwenye eneo.
“Baada
ya gari hilo kufunguliwa, kilichoonekana kwa urahisi ni sabuni na mifuko
michache inayosomeka kwa nje kuwa ni dawa ya kuku. Baada ya upekuzi ndipo zilionekana
mbao zilizokuwa zimefichwa chini ya katoni za sabuni. Tumeshikilia Lori hilo kwa hatua zaidi za
kisheria.
“Kufuatia
tukio hili, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia kwa Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania tunatoa onyo kali kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo vya
uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu kinyume cha sheria ya misitu namba
14 ya mwaka 2002 pamoja na kanuni zake za mwaka 2004 na kwamba watakaobainika
watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria za nchi” alisema Chamuya.
Akizungumzia
athari mbalimbali za vitendo hivyo vya uvunaji holela wa mazao ya misitu bila
ya kufuata taratibu za kisheria za uvunaji endelevu alisema vitendo hivyo vinatishia
nchi kuwa jangwa ambapo takwimu zinaonyesha jumla ya hekta 372,000 za misitu nchini
hupotea kila mwaka kutokana na matumizi makubwa ya rasilimali hizo ambayo
yanazidi uzalishaji wake kwa ujazo wa mita 19.5 milioni kwa mwaka.
Chamuya
ametoa wito kwa wananchi wote nchini kushirikiana na Serikali katika uhifadhi na
ulinzi wa rasilimali za misitu na kuacha fikra potofu kuwa kazi hiyo ni ya Serikali
pekee na taasisi zake kwakuwa faida zake hunufaisha jamii yote na vivyo hivyo
kama athari zitajitokeza basi zitaikumba jamii yote bila kubagua.
No comments:
Post a Comment