Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa
ameuagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuboresha Idara ya
Mipango na Usanifu katika wakala huo ili kupata matokeo mazuri katika
utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini.
Prof. Mbarawa ameutaka wakala huo kuboresha kanuni zinazosimamia
aina ya vyombo vya moto vinavyotumia barabara zote nchini ikiwemo ili
kuweza kusaidia miundombinu hiyo kudumu muda mrefu. Akizungumza mkoani Dodoma katika ufunguzi wa Baraza la Saba la
Wafanyakazi wa Wakala huo Prof. Mbarawa amesema kuwa wakala
unabidi uanze kubadili aina ya mfumo wa usanifu uliokuwa ukitumika awali
na badala yake utumike usanifu wa kisasa unaoendana na mahitaji halisi
ya watumiaji wa barabara hizo.
“Kama mnaona kuna mabadiliko yoyote mnayohitaji kuyafanya ili barabara
zetu zidumu, boresheni kanuni na mlete kwangu ili nizifanyie kazi”,
amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa katika kuboresha utendaji katika wakala huo, Serikali ina
mpango wa kuwapa fursa za ajira wahandisi hususani wanawake ili na
kuwajengea uwezo na kuweka uwiano katika taalamu hiyo. Aidha Waziri Prof. Mbarawa ameahidi kuongeza fedha za uendeshaji kwa
wakala huo ili kuuwezesha kutekeleza miradi mbalimbali inayoendelea
nchini.
“Kumbukeni majukumu ya Wakala yameongezeka sasa hamtajenga
barabara pekee, mmeongezewa jukumu la kujenga miundombinu ya
viwanja vya ndege hivyo ni muhimu kujipanga kutekeleza kazi hii”,
amesisitiza Prof. Mbarawa.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Patrick Mfugale ameahidi
kushughulikia ujenzi wa viwanja vya ndege ikiwemo kufanya kazi kwa
weledi na uadilifu kama ambavyo wakala huo unatekeleza miradi yake ya
barabara. Ameongeza kuwa Wakala unaendelea kufanya kazi na Makandarasi
wenye uwezo na wanaozingatia thamani ya fedha katika miradi yote
inayotekelezwa nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TANROADS, Eng. Hawa
Mmanga amemuahidi Waziri Prof. Mbarawa kufanya kazi kwa uadilifu, bidii,
na kuzingatia thamani ya fedha katika miradi yote inayotekelezwa na
wakala.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza
na wajumbe katika Baraza la Saba la Wafanyakazi wa Wakala wa Barabara nchini
(TANROADS), lililofanyika mkoani Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Patrick
Mfugale ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Saba la Wafanyakazi akitoa taarifa ya
utendaji kazi wa Wakala huo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa
Makame Mbarawa (hayupo pichani). Baraza hilo limefanyika mkoani Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Saba la Wafanyakazi wa Wakala wa Barabara nchini
(TANROADS), wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa
Makame Mbarawa (hayupo pichani), katika Baraza hilo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Patrick
Mfugale (kushoto) akiteta jambo na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa
Makame Mbarawa katika Baraza la Saba la Wafanyakazi wa Wakala huo lililofanyika
mkoani Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiwa katika
picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Saba la Wafanyakazi wa Wakala wa
Barabara nchini (TANROADS).
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akimsikiliza
mmoja wa wajumbe waliohudhuria katika Baraza la Saba la Wafanyakazi wa Wakala
wa Barabara nchini (TANROADS), mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment