Thursday, October 13, 2016

MISRI YADHAMIRIA KUMUUNGA MKONO RAIS MAGUFULI

Na Veronica Simba

Balozi wa Misri nchini Tanzania, Yasser El Shawaf amesema nchi yake ingependa kuwekeza katika sekta ya nishati hapa nchini ili pamoja na mambo mengine, isaidie katika kuzalisha umeme wa kutosha na hivyo kuunga mkono kwa vitendo azma ya Rais John Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda.

Aliyasema hayo hivi karibuni, alipomtembelea Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na kujadili kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati.

Kwa upande wake, Waziri Muhongo alimhakikishia Balozi huyo kuwa, Tanzania inazo fursa nyingi za uwekezaji katika sekta husika na hivyo kumkaribisha Balozi huyo kwa niaba ya nchi yake kuja kuwekeza nchini.

Katika mazungumzo yao, walijadili kwa kina kuhusu fursa mbalimbali zilizopo nchini, zikiwemo za uzalishaji umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali kama vile makaa ya mawe, jotoardhi, upepo, jua, mawimbi ya bahari na gesi asilia. Pamoja na kujadili fursa hizo, Profesa Muhongo alibainisha kuwa, utaratibu ambao Serikali imedhamiria kuutumia katika kuwapata wawekezaji mbalimbali ni kupitia ushindani wa wazi utakaozingatia vigezo muhimu ikiwemo uwezo/mtaji, utaalam na uzoefu wa mwekezaji husika.

Wataalam mbalimbali wa sekta husika kutoka wizarani na taasisi zilizo chini yake, pamoja na Ujumbe ulioongozana na Balozi Shawaf, walishiriki pia katika kikao hicho.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia), akiwa na Balozi wa Misri nchini, Yasser El Shawaf, baada ya kikao baina yao kilichofanyika hivi karibuni Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Misri nchini, Yasser El Shawaf (wa pili kutoka kushoto) na Ujumbe wake, wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kutoka kulia).
Balozi wa Misri hapa nchini, Yasser El Shawaf (katikati), akisaini kitabu cha wageni ofisini kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia).
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), akionesha zawadi aliyopewa na Balozi wa Misri hapa nchini, Yasser El Shawaf (kulia).
Mtaalam kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), akifafanua jambo, wakati wa kikao baina ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) na Balozi wa Misri hapa nchini, Yasser El Shawaf na Ujumbe wake (hawapo pichani).

No comments: