Kwa muda sasa kumekuwepo na usambazaji wa taarifa za upotoshaji zinazotolewa na
baadhi ya wanasiasa wakishirikiana na baadhi ya vyombo vya habari zinazolenga
kukejeli, kudhihaki, kukatisha tamaa, kubeza na kudhoofisha jitihada
zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi na Serikali zake katika kuleta maendeleo
kwa Watanzania.
Kumekuwepo na makala zinazoandikwa na magazeti mawili ya nje ambazo hutolewa
kila baada ya miezi miwili na ambazo zinapotosha na kuandika habari zisizo za
kweli kuhusu Tanzania.
Pia, yapo magazeti mawili ya ndani ambayo yamekuwa yakitoa makala mfululizo kwa
kila wiki zinazolenga kumchafua Mheshimiwa Rais na kuichafua taswira ya nchi
yetu.
Tumesikitishwa na waandishi wa makala hizo walioamua kujivua uzalendo na
kushiriki mpango wa kuiharibu heshima na taswira ya nchi yetu kwa maslahi ya
maadui zetu wa nje na baadhi ya wanasiasa. Tunafuatilia kujua nini kinawasukuma
kufanya hivyo na kwa maslahi ya nani ilhali sote ni Watanzania. Je ni tamaa ya
madaraka tu au mengine? Hakuna anayepinga ukosoaji bali unapaswa uwe ukosoaji
wenye nia njema kwa nchi.
Mtakumbuka hivi karibuni aliyewahi kuwa Waziri Mkuu aliyejiuzulu ambaye ni
mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa, alisambaza taarifa kwa vyombo
vya habari aliyoiita ya tathmini ya mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu wa
Oktoba 25, 2015.
Katika taarifa yake hiyo, alidai kuwa alileta msisimko mpya katika siasa za Tanzania,
kwamba ameshirikiana na wenzake kuionyesha nchi yetu maana ya demokrasia na
kukosoa juhudi za serikali na wateule wa Rais.
Demokrasia kimsingi ni dhana inayohusisha ushiriki na kuheshimu mawazo ya wengi
katika kufikia uamuzi. Ikiwa maana halisi ni hii, tunajiuliza ni ipi demokrasia
aliyoionyesha Lowassa ambayo leo anajisifu kuwa nayo?
Tulishuhudia akiwa mgombea urais wa chama ambacho hakijui, hakushiriki
kukijenga wala kutoa mchango wowote unaompa hadhi ya kupeperusha bendera huku
katiba na kanuni ya chama hicho ikivunjwa. Kidemokrasia, anayepewa fursa ya
kupeperusha bendera ya chama chochote makini duniani ni kiongozi au mwanachama
aliyethibitika kwa imani na matendo, kuzielewa, kuzitekeleza, kuzitetea
falsafa, itikadi na malengo ya msingi ya chama hicho. Mgombea ni taswira halisi
na alama muhimu inayoakisi dhamira ya chama husika machoni kwa wananchi.
Demokrasia ya kweli lazima ianzie ndani ya chama, ni demokrasia ipi iliyotoa
mamlaka kwa vyama vinavyounda UKAWA kuwanyima wanachama wao haki ya kuomba
ridhaa ya kupeperusha bendera za vyama walivyoviasisi, kuvitetea, kuvigharamia
na walivyovitumikia kwa kuamua kumteua mgombea “MTUNGUO” (ambaye hajapimwa wala
hajawahi kuvipigania). Kitendo hicho cha kutowashirikisha wanachama na
kuwanyima haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kilidhihirisha
usaliti wa hali ya juu wa misingi ya demokrasia.
CHADEMA watuambie njia iliyotumika kuwapata wabunge wa viti maalumu. Ni
demokrasia gani inayotoa fursa kwa baadhi tu ya viongozi kuteua wabunge ambao
wanakiwakilisha chama chote. Ambapo kila kiongozi aliteua maswahiba zake na
wengine kwa ugeni wao ndani ya CHADEMA walikosa watu wanaowafahamu na kuamua
kuwateua wanawake maswahiba wao ndani ya CCM. Msingi wa kawaida wa kupata
wabunge wa viti maalum ukiacha kura za maoni, kigezo kingine muhimu ni mchango
wa mgombea/mwanachama huyo katika kukijenga na kukitumikia chama chake.
Yaliyotokea kwa CHADEMA kwenye wabunge wake wa viti maalum ni mapya kwenye
ulimwengu wa demokrasia. Inahitaji wataalamu wa sayansi ya siasa kufanya
utafiti wa aina hii mpya ya demokrasia.
Tulidhani baada ya mwaka mmoja kupita, wenzetu hawa wangelikuwa wamejifanyia
tathmini, kujikosoa, kujisahihisha na hata kufanya uungwana wa kuwaomba radhi
wanachama wao kwa uvunjifu mkubwa wa misingi ya demokrasia, katiba na kanuni za
vyama vyao.
Tunatoa wito kwa vyama vya siasa nchini kutochukulia kwa wepesi masuala ya
demokrasia na mabadiliko, yasiwe ni nyimbo za kuburudisha au kutoa matumaini
hewa kwa wanachama na wananchi. Kanuni mojawapo ya demokrasia ndani ya vyama ni
lazima ionekane katika muundo wake na katika utekelezaji wa muundo huo.
Umefika wakati vyama vya siasa vinapaswa kujifunza kuuza sera ili kujijenga na
sio kusubiri matukio kwa ajili ya kupata huruma ya wananchi. Tunasubiri
kushuhudia na kusikia demokrasia itakavyoendeshwa katika uchaguzi wa ndani wa
vyama hivyo ambapo kuna taarifa mmoja wa vigogo amefanikiwa kupata kiasi cha
dola milioni 15 zitakazomsaidia kupanga safu yake ya uongozi.
Katika kutimiza mpango huo, tayari yapo mawasiliano ya mara kwa mara ya baadhi
ya viongozi wakitoka Zanzibar na sehemu zingine za nchi kuja Dar es Salaam, na
imeonekana dhahiri mazungumzo yao kutowashirikisha viongozi wenzao waandamizi
kwani yanalenga kufanikisha mpango huo.
Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli, ameendela kufanya juhudi kubwa katika
kuijenga nchi kwa kuimarisha utendaji na nidhamu ya utumishi serikalini,
kukusanya mapato na kusimamia matumizi sahihi ya fedha, kupambana na kuzuia
mianya ya rushwa pamoja na kusimamia haki, usawa na wajibu kwa raia. Mwenzetu
anayaona haya kuwa ni kuufanya utumishi wa umma kaa la moto.
Juhudi hizi na nyinginezo ikiwemo ununuzi wa ndege mpya, ujenzi wa miundombinu
ya barabara, reli, afya kwa kununua vitanda vya wazazi, kutoa elimu bure
kuanzia shule ya msingi hadi sekondari na nyinginezo hazipaswi kukatishwa tamaa
kwa maslahi ya wachache, ni vyema kuziunga mkono kwa maslahi ya taifa letu.
Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Rais Dk. Magufuli madarakani, CCM
inawaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono katika dhamira yake safi ya
kuwaondolea kero, kuboresha huduma za jamii na kuwaletea maendeleo ya kiuchumi
na kijamii.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na;-
CHRISTOPHER OLE SENDEKA
MJUMBE WA NEC NA MSEMAJI WA CCM
28/10/2016.
No comments:
Post a Comment