Saturday, August 6, 2016

Waziri wa Mambo ya Ndani auagiza uongozi wa Magereza ya mkoa wa Iringa kuanza mchakato wa kuhamisha magereza ya Manispaa ya Iringa

WAZIRI wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba ameagiza uongozi wa Magereza ya mkoa wa Iringa kuanza mchakato wa kuhamisha magereza ya Manispaa ya Iringa ili eneo hilo kutumika kupanua Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa.


Nchemba ametoa agizo hilo leo baada ya kutembelea eneo hilo ambalo limekuwa likiombwa kwa muda mrefu na viongozi wa serikali ya mkoa wa Iringa ili litumike kwa ajili ya matumizi ya Hospitali hiyo ya Rufaa ya mkoa wa Iringa .

Akizungumza baada ya kutembelea eneo la Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa alisema kuwa amekubaliana na maombi ya viongozi wa mkoa wa Iringa ya kuomba gereza hilo kuhamishiwa katika eneo la Mlolo nje kidogo na Manispaa ya Iringa huku eneo hilo la Magereza litumike kupanua majengo ya Hospitali hiyo ya Rufaa ya mkoa wa Iringa.

“ Kwa kawaida kati ya Hospitali na magereza kinachotakiwa kuwepo mjini ni Hospitali na sio magereza hivyo hivyo kati ya mgonjwa na mfungwa ama mahabusu anayeweza kufanya kazi ya kufyatua tofari za ujenzi ni mahabusu ama mfungwa na sio mgonjwa , hivyo naagiza mtaalam wa ujenzi wa magereza kuanza kuandaa vifaa vya kufyatualia tofari na kwa kufuata taratibu za magereza waorodheshwe wale ambao watakuwa tayari kujitolea kufanya kazi ya ujenzi ili kazi hiyo ianze” 

Hata hivyo waziri huyo alisema kuwa kuanzia leo anataka kupata orodha ya wafungwa waliopo gerezani hapo ambao wanauwezo wa kufanya kazi.

Pia alisema suala la kuhamishwa kwa gereza hilo litafanyika kwa awamu na kuwa wakati gereza linajengwa na baadhi ya nyumba za watumishi bado askari wataendelea kuishi katika eneo hilo huku majengo yao likiwemo jengo la Ghorofa utawekwa utaratibu wa kujengewa jingine ili hilo linalotumiwa na magereza litumike kwa ajili ya madaktari.

 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akisalimiana na Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi (kulia) baada ya kukutana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, leo.
 
Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi (katikati)  akimtambulisha Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, wakati walipokutana leo nje ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akisalimiana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, SACP Peter Kakamba.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akizungumza katika kikao na Uongozi wa Mkoa wa Iringa.
 
Mbunge wa Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa wa pili kushoto wakisalimiana kwa furaha na mwenyekiti wa CCM Iringa mjini Abeid Kiponza huku Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela (kushoto) wakiangua kicheko
 
Mganga mkuu wa mkoa wa Iringa Dr Salmu Robart akimwonyesha waziri Nchemba ufinyu wa eneo la Hospitali hiyo ya rufaa ya mkoa wa Iringa. Picha na MatukiodaimaBlog.

No comments: