Tuesday, August 2, 2016

WAZIRI MBARAWA AITAKA TPA KUPUNGUZA VIKAO

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Rukwa Arch. Deocles Alphonce wakati alipokagua ujenzi wa ofisi za Bonde la Ziwa Rukwa na Maabara zake zilizopo Sumbawanga Mjini.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akikagua nondo zilizosukwa kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Kalambo lililopo katika barabara ya Sumbawanga-Matai- Kasanga yenye urefu wa KM 112, Mkoani Rukwa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiendelea na ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Sumbawanga-Matai- Kasanga yenye urefu wa KM 112, Mkoani Rukwa.
Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya Nicholas O’Dwyer Eng. Farley Vicente akitoa taarifa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuhusu ujenzi wa barabara ya Sumbawanga-Matai- Kasanga yenye urefu wa KM 112, Mkoani Rukwa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa China Railway 15 Bureau Group Corporation kutoka China Zhang Tonggang (mwenye sweta nyekundu) inayojenga barabara ya Sumbawanga-Matai- Kasanga yenye urefu wa KM 112 kwa kiwango cha lami, Mkoani Rukwa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akihakiki taarifa za mapato katika Bandari ya Kasanga iliyopo Mkoani Rukwa. Katikati ni Msimamizi wa bandari hiyo Bw. Seleman Kalugendo.
Meneja wa Shirika la Posta Tanzania Bi. Zahara Sukeiman akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuhusu huduma ya kutuma na kupokea Vifurushi wakati Waziri alipotembelea ofisini hapo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa Maelekezo kwa Meneja wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) nyanda za juu kusini Bw. Peter Kaguru wakati alipotembelea ofisi hizo Mkoani Rukwa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kupunguza idadi ya vikao vya baraza visivyo na ulazima ili kuondokana na matumizi mabaya ya fedha na badala yake fedha hizo zielekezwe kwenye uendelezaji wa miundombinu ya  bandari za maziwa.

Ametoa agizo hilo mara baada ya kukagua shughuli za utendaji  wa bandari ya Kasanga iliyopo mkoani Rukwa inayohudumia mkoa wa Kigoma, nchi ya Burundi na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC) ambapo amebaini mapungufu ya kiutendaji ikiwemo malipo yasiyotumia njia za kielektroniki na miundombinu isiyo rafiki katika kukidhi ushindani wa kibiashara katika bandari hiyo.

Waziri Mbarawa ameitaka TPA kuweka mfumo wa uendeshaji vikao kwa njia ya kieletroniki (video conference) kwa lengo la kudhibiti matumizi ya fedha nyingi zilizokuwa zikitumika katika uendeshaji wa vikao hivyo.

“Nataka TPA muanze kutumia video Conference katika vikao vyenu ili fedha zilizokuwa zikitumika zifanyie kazi nyingine za maendeleo ya Taifa”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa TPA imekuwa na wajibu mkubwa wa kuchangia pato la Taifa kupitia huduma za upakiaji na upakuaji wa mizigo hivyo wanapaswa kuanza kutumia mfumo wa kielekroniki katika ukusanyaji wa mapato katika bandari zote nchini ili kudhibiti upotevu wa mapato.

“Tukianzisha mfumo wa kielekroniki katika bandari hii tutakuwa na uwezo wa kufuatilia mapato yanayopatikana katika utoaji wa huduma na kujua kama malengo yamefikiwa”, amesema Prof. Mbarawa

Katika Hatua nyingine Profesa Mbarawa amekagua barabara ya Sumbawanga-Matai- Kasanga Port yenye urefu wa KM 112 inayojengwa kwa kiwango cha Lami na kumtaka Mkandarasi wa barabara hiyo China Railway 15 Bureau Group Corporation kukamilisha ujenzi huo ifikapo Julai mwakani.

Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutaunganisha mji wa Sumbawanga na Bandari ya Kasanga na hivyo kurahisisha shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka bandarini hapo na hivyo kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

“Kukamilika kwa barabara hii kutawawezesha wananchi kusafirisha bidhaa zao, kutoka sehemu moja hadi nyingine na hivyo kukuza uchumi wao na kuongeza pato la Taifa”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Aidha Waziri Mbarawa amemuhimiza Mkandarasi huyo kujenga barabara hiyo kwa viwango vilivyopo katika mkataba na kuzingatia thamani ya fedha katika ujenzi huo ili kuwezesha barabara hiyo kudumu kwa muda mrefu.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini, Mkoa wa Rukwa Eng. Masuka Mkina amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo umekamilika kwa asilimia 62 ambapo kukamilika kwa ujenzi huo utatagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 133.

“Mpaka sasa Mkandarasi ameweza kukamilisha kujenga makalvati makubwa 11 kati ya 13, na makalvati ya kawaida 169 kati ya 241”, amesema Eng Mkina.

Waziri Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kukagua miradi ya miundombinu na kuangalia utendaji kazi wa taasisi zilizopo katika Mkoa wa Rukwa.

No comments: