Thursday, August 11, 2016

Watanzania watakiwa kuunga mkono jitihada za Serikali kupambana na wizi wa kazi za sanaa nchini

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye( kushoto) akiangalia bidhaa za filamu na muziki zilizokamatwa katika zoezi la kushtukiza la ukamataji wa bidhaa hizo katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam zilizoingizwa nchini kinyume na sheria, kulia ni Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bi. Joyce Fissoo.
Mitambo ya kuzalishia bidhaa za filamu na muziki kama zilivyokutwa katika kampuni ya Aguster kariakoo jijini Dar es Salaam katika zoezi la kushtukiza la ukamataji wa bidhaa hizo zilizoingizwa sokoni kinyume na sheria na hivyo kuikosesha serikali mapato kupitia kodi. Picha zote na Lorietha Laurence WHUSM.

Na Raymond Mushumbusi WHUSM

Kilio cha wizi wa kazi za sanaa nchini kimekuwa cha siku nyingi hali inayosababisha wasanii wengi kukosoa haki ya kazi zao kwani baadhi ya watu wamekuwa wakitumia kazi zao kujinufaisha wenyewe na wasanii kubaki wakiwa hawana maendeleo yoyote kutokana na kazi zao ukilinganisha na wasanii wa nchi jirani za Afrika ya Mashariki na duniani kwa ujumla.

Ikumbukwe katika halfa iliyoandaliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli kwa kuwashukuru makundi ya watu mbalimbali wakiwemo wana habari, wasanii na wanamichezo kwa ujumla Mhe. DKt Magufuli aliagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kusimamia kazi za wasanii na kuhakikisha wanakamata kazi zote ambazo hazina stika ya TRA.

Katika kutekeleza agizo hilo hivi karibuni Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alifanya zoezi la kushtukiza la kukagua kazi za wasanii ambazo hazina stika ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo zinakwepa kulipa kodi katika soko la Kariakoo Jijini Dar es Salaam na kuahidi  kwamba zoezi hilo litafanyika nchi nzima.
Katika zoezi hilo Serikali ilifanikwa kukamata jumla ya  bidhaa za filamu na muziki 111,802 ambapo 111,529 ni za wasanii wa nje zilizoingia nchini kinyume na sheria huku bidhaa 273 za wasanii wa ndani zikiwa hazina stika ya ushuru wa bidhaa kutoka Mamlaka ya  Mapato Tanzania(TRA).

Aidha mpaka sasa takribani  maduka 42 yamekaguliwa na kukamata  mitambo 19 ya kufyatua kazi za wasanii (duplicators),printer 8 za Cd/Dvd,dvd writers 31,komputa 3,ups 7 kutoka kampuni ya Aguster.

Katika zoezi hilo Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alisema hatua hii ni ya mwanzo kwa kuwaonesha watanzania kuwa agizo la Rais wa awamu ya Tano Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli la kulipa kodi na kununua bidhaa halisi kwa kutoa risiti na kupambana na wizi wa kazi za sanaa nchini linasimamiwa ipasavyo.

Mhe.Nnauye aliongeza kuwa wauzaji wengi wa bidhaa za filamu na muziki wamekuwa wakikiuka Sheria  zinazosimamia tasnia ya Filamu na muziki ikiwemo sheria ya Filamu na Michezo ya kuigiza na.4 ya mwaka 1976 inayosimamiwa na Bodi ya Filamu Tanzania.

Waziri Nape Nnauye alizitaja sheria nyingine kuwa ni Sheria ya Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na.23 ya mwaka 1984, Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki  na.7 ya mwaka 1999 inayosimamiwa na Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki ( COSOTA) pamoja na Sheria ya Ushuru wa Bidhaa sura ya 147 chini ya kanuni za stampu kwa bidhaa za Filamu na Muziki ya mwaka 2013 inayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA).

Mhe. Nnauye ameongeza kuwa Serikali itaendelea kujenga misingi mizuri kwa wasanii na tasnia ya filamu Tanzania na kuhakikisha wasanii na watayarishaji wanapata mitaji itakayowawezesha  kuzalisha filamu bora na kupata masoko mazuri.

Uchumi wa nchi na wasanii umehujumiwa sana kwa muda mrefu  kufuatia kuwepo kwa bidhaa za filamu za kitanzania nchini kuuzwa kwa njia zisizo halali  na kuikosesha Serikali mabilioni ya fedha kupitia kodi.

Kwa upande wake katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bibi. Joyce Fissoo amesema wasanii sasa wanatakiwa kutengenza kazi zenye ubora zaidi ili kuvutia watanzania kununua kazi zao na kuleta ushindani katika soko la filamu nchini na nje ya nchi.

“ Nawapongeza watayarishaji wa filamu wanaotemgeneza filamu zenye ubora kwa kuzingatia maadili na wazidi kutengeneza filamu zenye ubora zaidi ili kukuza tasnia ya filamu nchini na kuongeza pato la wasanii na taifa” Alisema Bi Joyce.

Bibi. Joyce Fisso ameongeza kuwa Bodi yake  inapokea filamu na maigizo mbalimbali kwa ajili ya kupata kibali cha kusambazwa hivyo basi jamii inatahadharishwa kuzingatia kununa filamu zenye stika za TRA katika filamu na maigizo hayo ili kuepukana wizi wa kazi za sanaa unaozidi kuongezeka siku hadi siku.

Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. George Haule amewaomba wananchi waunge mkono jitihada za Serikali kwa kununua bidhaa za filamu  zenye stika ya TRA ili kusaidia kuongeza pato kupitia kodi na kukomesha wale wote wanaokwepa kulipa kodi.

“Nawaomba wananchi waunge mkono serikali wanunue bidhaa za filamu za ndani na nje zenye stika ya TRA ili kusaidia kuongeza pato la kodi na la wasanii ili  kukomesha wale wote wanaokwepa kulipa kodi” alisema Bw.Haule.

Baada ya ziara ya kushtukiza ya Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye,Chama cha Wasambazaji wa  Filamu Tanzania  na Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) wamepongeza hatua iliyochukuliwa na Wizara huyo katika kuhakikisha wanatokomeza waharamia na uuzaji wa kazi za wasanii bila kufuata utaratibu za kisheria zilizowekwa.

Aidha Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF),Simon Mwakifamba,amesema kuwa anaunga mkono zoezi linaloendelea kwa wadau wa kazi za wasanii chini wakishirikiana na Serikali katika kuhakikisha wanatokomeza uharamia wa kazi za wasanii wote nchini ili walau kuwapa motisha ya maisha mazuri waigizaji hao ili waendelee kutengeneza kazi nzuri za kuelimisha na kuburudisha jamii.

Naye  Mwenyekiti wa chama cha wasambazaji wa filamu nchini,Moses Mwanyilu, hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari na kupongeza hatua ya Serikali imekuja katika muda muafaka kufuatia kilio cha muda mrefu kutokana na baadhi ya wafanyabiashara na wasambaji wa filamu na muziki kutoka nje ya nchi wamekuwa wakiingiza na kuuza bidhaa hizo bila ya kufuata utaratibu ikiwemo kulipa kodi.

Amesema kuwa wafanyabiashara hao pia wamekuwa wakidurufu filamu za ndani ya nchi na kuziingiza sokoni bila ya wasanii kunufaika na kazi zao ikiwemo kazi hizo kutolipiwa kodi hivyo kupelekea kuziuza kwa bei ya chini ukilinganisha na filamu hapa nchini jambo ambalo linasababisha soko la filamu za ndani kudidimia.

Aidha Mwanyilu ameongeza kuwa  baada ya kilio cha muda mrefu hatimaye wameona jitihada za Serikali kupitia kwa Wizara inayohusika na masuala ya sanaa kuanza kuchukua hatua za makusudi kufanya oparesheni ya nguvu ya kukamata walanguzi wa kazi za wasanii nchini katika maeneo ya kariakoo.

Naye Katibu Mkuu wa chama cha Wasambaji wa Filamu Tanzania,Suleiman Ling’ande alisema kuwa tatizo la uharamia katika kazi za wasanii nchini ni changamoto ya muda mrefu kufuatia kuwepo na sheria ambayo imeshindwa kukidhi na kusimamia utaratibu unaofaa hasa katika kuhakikisha kazi za wasanii zinawanufaisha wasanii pamoja na kuliongezea kipato taifa pamoja na kulipa kodi.

Kwa niaba ya chama cha wasambazaji wa filamu na shirikisho la filamu Tanzania na vyama vyote vya shirikisho wanapenda kutoa shukrani za dhati kwa wizara ya habari kupitia waziri wake,Nape Nnauye kwa kushirikiana na mamlaka ya mapato Tanzania (TRA),Bodi ya filamu,Cosota na Baraza la Sanaa Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kazi za wasanii nchini zinauzwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa na unaotambulika.

Serikali imeahidi  kuendeleza zoezi la kukamata bidhaa feki zinazoingia nchini kinyume na sheria pamoja na zile zinazokwepa kulipa kodi ili kuinua uchumi wa nchi na wasanii.
Serikali imewahakikishia wasanii na watengenezaji wa  filamu Tanzania kuwa kazi hii ya kusaka wezi wa kazi za sanaa nchini  itaendelea na haitoshindwa itashinda na imewaonya wanaofanya kazi ya kuiba kazi za wasanii waache mara moja na yoyote atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Wadau wa sanaa na filamu kwa ujumla wameaswa kukaa na Serikali na kuangalia namna bora yakuboresha jinsi ya kusambaza kazi za sanaaa kwa kuzingatia Sheria za nchi na  kurasimisha vibanda vinavyoonesha filamu za kitanzania kuwa kumbi maalum kwa ajili ya kuonesha filamu hizo ili kuongeza soko la filamu hizo kupitia kumbi hizo.

No comments: