Baadhi ya wazalishaji, wanunuzi na wafanyabiashara wa
madini ya jasi na makaa ya mawe wakijisajili kabla ya kuanza
kwa mkutano ulioongozwa na Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, Dkt Medard Kalemani hivi karibuni katika Ofisi za
Wizara jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani
(katikati) akizungumza na wazalishaji, wanunuzi na
wafanyabiashara wa madini ya jasi na makaa ya mawe hivi
karibuni katika Ofisi za Wizara jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani
akizungumza mbele ya waandishi wa habari, katika mkutano
uliowakutanisha wazalishaji, wanunuzi na wafanyabiashara
wa madini ya jasi na makaa ya mawe (hawapo pichani) hivi
karibuni katika Ofisi za Wizara jijini Dar es Salaam. Kulia ni
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Madini, Profesa James
Mdoe.
Na Veronica Simba
Serikali imepiga marufuku wawekezaji nchini kuagiza makaa
ya mawe na madini ya jasi kutoka nje kwa ajili ya matumizi ya
viwanda badala yake imewataka wanunue madini hayo
kutoka kwa wazalishaji wa ndani.
Akizungumza hivi karibuni mbele ya waandishi wa habari
katika mkutano uliowajumuisha wazalishaji, wanunuzi na
wafanyabiashara wa madini ya jasi na makaa ya mawe;
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani
alisema hakuna sababu ya madini hayo kuagizwa kutoka nje
ya nchi kwani ipo hazina ya kutosha nchini.
Katika Mkutano huo uliofanyika Makao Makuu ya Wizara ya
Nishati na Madini jijini Dar es Salaam, Dkt Kalemani
alibainisha kuwa kwa upande wa makaa ya mawe, hazina
iliyopo nchini kwa sasa ni zaidi ya tani milioni 5.
“Madini hayo hayajachimbwa na tunataka wachimbaji
wadogo na wakubwa waje wayachimbe.”
Akifafanua zaidi kuhusu hazina ya makaa ya mawe iliyopo
nchini, Dkt Kalemani alieleza kuwa, hadi sasa, viwanda
vinavyozalisha madini hayo vimezalisha takribani tani 50,000
kwa ujumla wake wakati mahitaji ni tani 37,000 tu.
“Kwa hivyo hatuwezi kuelewa kwamba mahitaji ni makubwa
kuliko uzalishaji, si kweli hata kidogo. Makaa ya mawe yapo
ya kutosha, haturuhusu kuagiza kutoka nje na huo ndiyo
msimamo wa Serikali,” alisisitiza.
Halkadhalika, kwa upande wa madini ya jasi, Naibu Waziri
Kalemani alieleza kuwa hazina iliyopo nchini kwa sasa ni
zaidi ya tani 300,000 na kwamba Viwanda vya ndani bado
vinahitaji madini hayo ili kutosheleza mahitaji yao.
“Zipo kampuni za kizalendo zinazozalisha jasi na makaa ya
mawe. Niwapongeze Magamba sana, mnazalisha vizuri na
mwongeze uzalishaji. Lakini watanzania wengine waige,
wazalishe ili wenye viwanda vyote waweze kununua hapa
nchini.”
Dkt Kalemani pia aliwataka Maafisa Madini wa Kanda zote
nchini hususan maeneo kulipo na Viwanda, wasimamie
utekelezaji wa maagizo hayo ya Serikali.
Aidha, agizo jingine alilotoa Dkt Kalemani ni kwa wazalishaji
na wanunuzi wa makaa ya mawe kuingia mikataba rasmi,
ambapo aliagiza mikataba husika ieleze bayana bei ya
kununua na bei hiyo itenganishwe na gharama ya usafirishaji.
“Hatutaki kuambiwa kwamba bei kutoka Afrika Kusini ni rahisi
kuliko bei ya kutoka pale Mchuchuma kwenda Mtwara.”
Kuhusu suala la thamani ya makaa ya mawe pamoja na jasi,
Dkt Kalemani aliwaagiza Shirika la Umma linalojishughulisha
na tafiti mbalimbali pamoja na kutoa ushauri wa kitaalam
kuhusu Viwanda (Tanzania Industrial Research and
Development Organization – TIRDO) kwa kushirikiana na
Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), kufanya kazi ya
kutathmini ubora wa madini husika ili kuondoa malalamiko
yaliyopo kwamba madini hayo yanayozalishwa hapa nchini
yana thamani ya chini yakilinganishwa na yanayozalishwa na
nchi nyingine ikiwemo Afrika ya Kusini.
Kuhusu suala la kuwepo bei elekezi za madini hayo, kama
walivyoomba wadau kwenye mkutano husika, Naibu Waziri
alisema kuwa, Serikali itatathmini umuhimu wake wakati
biashara ikiendelea.
Katika hatua nyingine, Dkt Kalemani aliwaagiza Maafisa
Madini wa Kanda zote, kuandaa orodha ya maeneo yenye
leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini ya jasi ambayo
hayafanyiwi kazi na kuwasilisha orodha hiyo wizarani ili
zifutwe na kuwapatia watanzania wenye uwezo wawekeze.
“Nimepata taarifa kuwa kuna jumla ya leseni 1230 za madini
ya jasi lakini zinazozalisha ni 472 tu hivyo, nimewapa siku 30
Maafisa Madini kuanzia leo, mtayarishe orodha mlete tufute
leseni ambazo hazisimamiwi vizuri,” alisisitiza.
Dkt Kalemani aliwataka wazalishaji pamoja na wanunuzi
wote wa makaa ya mawe pamoja na jasi, kuingia mikataba
ya kuuziana ifikapo tarehe 20 mwezi huu.
Pia, alielekeza kuwa, kuanzia sasa mahitaji ya madini husika
(oda) yawe yanatolewa ndani ya siku 20. “Lisiwe jambo la
kushtukiza kwamba mnahitaji leo tani 30 mnatoa oda
zizalishwe siku hiyohiyo. Hilo haliwezekani.”
Naibu Waziri pia alisisitiza kwamba ni marufuku kununua
madini ya jasi na makaa ya mawe kwa madalali (middlemen)
na kuagiza madini hayo yanunuliwe kutoka wazalishaji, kwani
husababisha kupanda kwa bei pasipo sababu za msingi.
Aidha, katika mkutano huo, Naibu Waziri Kalemani alimteua
rasmi Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Madini, Profesa
James Mdoe kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kuratibu
changamoto zinazojitokeza katika masuala husika.
Alieleza kuwa Kamati hiyo itakuwa na wajumbe wengine 12
kutoka kwenye taasisi za wazalishaji na wanunuzi na kutoka
ofisi za madini za kanda, ambapo wadau wote watatakiwa
kuripoti katika Kamati hiyo endapo watakuwa na tatizo lolote.
Alisema kuwa majina ya wajumbe wa Kamati yatatolewa
ndani ya siku Tano (5).
Mkutano huo umefanyika kufuatia maazimio yaliyofikiwa
katika mkutano uliofanyika mapema mwezi huu (Agosti 3),
uliowakutanisha wadau husika chini ya uenyekiti wa Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
No comments:
Post a Comment