WADAU HABARI ZA SAA HIZI, TAFADHALI POKEENI CODES:
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) akiwa na kinyago cha mwanamke baada ya kuzindua mradi wa Green Voices Tanzania. Katikati ni mfadhili wa mradi huo, Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, Maria Tereza Fernandes de la Vega, na kushoto ni Mkuu wa Wilaya Ilala, Sophia Mjema.
MAKAMU wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema
serikali itahakikisha mradi wa kutunza mazingira nchini wa Green Voices unakuwa
endelevu na kwamba ni vyema akinamama wote nchini kushirikishwa katika
mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza wakati
wa uzinduzi wa mradi huo wa Green Voices Tanzania katika ukumbi wa Hotel ya
Serena jijini Dar es Salaam, Mhe. Samia amesema kipindi cha miezi mitatu
ambacho mradi huo umeanza kutekelezwa nchini kimeonyesha mafanikio makubwa na
kutia hamasa kwa jamii na serikali kuona umuhimu wa kuuendeleza licha ya kwamba
ufadhili wa mradi huo ulikuwa wa mwaka mmoja tu.
Mradi huo wa
Green Voices umefadhiliwa na taasisi ya Women for Africa Foundation inayoongozwa
na makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Maria Tereza Fernandes de la Vega Sanz
(67).
“Mimi kama
kiranja wa mazingira, ninaahidi kwamba serikali itahakikisha mradi huu unakuwa
endelevu, usiishie hapa tu, na tunataka kila mkoa na hata wilaya zote nchini
wanawake washiriki kwa sababu wao ndio wanaobeba mzigo mkubwa wa jamii huku
mazingira yakiwa yanaharibiwa,” alisema.
“Tumeuzindua
mradi huu kuashiria kwamba kazi imeanza, lakini ni lazima tuhakikishe unakuwa
endelevu na usiishie hapa,” aliongeza.
Makamu wa
Rais amesema kwamba amefarijika na ongezeko la wanawake wanaojihusisha na
miradi ya utunzaji mazingira katika kipindi kifupi tu tangu wapatiwe mafunzo
nchini Hispania.
“Kutoka
wanawake 15 waliopatiwa mafunzo miezi mitatu iliyopita, leo nimefarijika
kusikia kwamba tayari hawa wamekwishawafundisha wanawake wengine 250, haya ni
mafanikio makubwa na lazima serikali iyaunge mkono,” alisema.
Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania Mama Maria Tereza, wakisikiliza maelezo ya ukaushaji wa mboga mboga kutoka kwa Esther Muffui wa Morogoro.
Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania Mama Maria Tereza, wakisikiliza maelezo ya ufugaji nyuki kutoka kwa akinamama wa Dakawa, Morogoro.
Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania Mama Maria Tereza, wakisikiliza maelezo kutoka kwa wanahabari wanawake wanaofanya mradi wa Green Voices Tanzania.
Awali,
Mratibu wa mradi wa Green Voices Tanzania, Secelela Balisidya, alisema kwamba,
baada ya kurejea kutoka Hispania, wanawake 10 wanaofanya miradi mbalimbali
inayolenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi katika mikoa sita ya Tanzania
Bara, wameweza kuwafundisha wenzao wengine 250 na kasi yaw engine kujifunza
inaendelea.
Alisema lengo
la Green Voices ni kuhakikisha wanapanua uelewa kwa wanawake na jamii kwa
ujumla kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira pamoja na kukabiliana na mabadiliko
ya tabianchi, lakini wakati huo huo kuona kwamba wanawake wanafanya miradi
inayoendana na dhima hiyo pamoja na kuwaongezea kipato.
Naye Balozi
Getrude Mongella, amesema kwamba mradi wa Green Voices na miradi mingine ambayo
inashughulikiwa katika Bara la Afrika inaonyesha ushirikiano wa kimataifa siyo
tu kwa serikali bali kwa wanawake.
Amesema ni
vyema ushirikiano wa maendeleo usiachiwe tu kwa serikali, bali unaweza
ukafanywa hata kwa watu binafsi.
Bidhaa mbalimbali zinazotokana na mazao ya muhogo.
Kuhusiana na
ushirikishwaji wa wanawake, Balozi Mongella ambaye ndiye Mwafrika wa kwanza
kuwa mwenyekiti wa Mkutano wa Dunia wa Wanawake uliofanyika Beijing, China
mwaka 1995, amesema jitihada za kwanza zilianza katika Mkutano wa Rio de
Janeiro, Brazil mwaka 1992 kuhusu mazingira na mkutano wa maendeleo wa Cairo,
Misri 1993 pamoja na ule wa Beijing, ambapo maazimio yaliyofikiwa ni
kuhakikisha wanawake wanahusishwa katika maendeleo.
“Jambo
muhimu ni kwamba, miradi hii yote inawahusisha wanawake, na kwa hakika wanawake
ndio wenye nafasi kubwa ya kuleta maendeleo,” alisema.
Naye Makamu
wa Rais mstaafu wa Hispania, Maria Tereza Fernandes de la Vega, amewapongeza
wanawake hao wa Tanzania kwa jitihada kubwa walizozionyesha kuhusu mradi huo na
kuahidi kuendelea kuwasaidia.
Alisema kwamba,
mradi huo ni wa majaribio, lakini umeweza kuleta matumaini makubwa tofauti na
walivyofikiria awali.
“Julai mwaka
jana wakati nilipokuja hapa Tanzania ndipo nilipata wazo la kuleta mradi huu
kwa majaribio, lakini inatia imani kubwa kuona wazo lile tulilotaka kulijaribu
leo hii limepata mwitikio mkubwa namna hii,” alisema Maria Tereza, ambaye ndye
Rais wa taasisi ya Women for Africa Foundation.
Mama Maria
Tereza alikuwa makamu wa rais wa Hispania kati ya Aprili 18, 2004 hadi Oktoba
20, 2010, na ndiye alikuwa msemaji wa serikali ya Waziri Mkuu Jose Luis
Rodriguez Zapatero. Yeye ni mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo katika
historia ya Hispania.
No comments:
Post a Comment