Thursday, July 14, 2016

KALEMANI AWATAKA WAKANDARASI MIRADI YA UMEME KUACHA VISINGIZIO

Msimamizi Mkuu wa Mradi wa usafirishaji wa umeme mkubwa, maarufu kama ‘Backbone’, Mhandisi Khalid James (aliyenyoosha mkono), akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka kulia-mbele), kuhusu upanuzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Iringa ili kuwezesha Kituo hicho kupokea umeme mkubwa wa Backbone.
Msimamizi Mkuu wa Kituo cha kupoza umeme cha Iringa, Theopist Semanini akimweleza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (wa tatu kutoka kushoto), utendaji kazi wa Kituo hicho, wakati wa ziara yake kukagua miundombinu ya umeme hivi karibuni.
Ofisa anayeshughulikia uangalizi wa Gridi katika Kituo cha kupoza umeme cha Iringa, John Havie, akimwonesha Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (kulia kwa John) namna anavyoongoza mitambo kupitia chumba maalum cha uangalizi (control room).
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (kulia) akimweleza jambo Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto (kushoto) walipokutana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa wakati wa ziara ya Naibu Waziri kukagua miradi ya umeme mkoani humo hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (wa tatu kutoka kushoto), akitoa maagizo kwa baadhi ya maofisa wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wanaosimamia Bwawa la Maji la Mtera mkoani Iringa, alipotembelea Bwawa hilo ambalo maji yake hutumika kuzalisha umeme, akiwa katika ziara kukagua miradi ya umeme hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (mwenye Suti ya Bluu – Kulia), akizungumza na waandishi wa habari wa Iringa kuhusu utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya umeme mkoani humo, alipopitia katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, akiwa katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya umeme hivi karibuni.

Na Veronica Simba - Njombe

Serikali imewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali ya umeme hapa nchini kuachana na visingizio vya uchelewaji wa fedha kutoka kwa wafadhili na badala yake watumie fedha zao kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani aliyasema hayo hivi karibuni mkoani Njombe akiwa katika ziara kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme.

Dkt Kalemani alisema kuwa, kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wakandarasi kuchelewesha utekelezaji wa miradi wanayoisimamia kwa kisingizio kuwa hawajapokea fedha kutoka kwa wafadhili na hivyo aliwataka kuachana na tabia hiyo mara moja.

Alisema, mojawapo ya sifa katika kuchagua Mkandarasi ni pamoja na uwezo wake wa kifedha katika kutekeleza mradi husika hivyo hakuna sababu ya Mkandarasi kuchelewesha kazi kwa kisingizio cha fedha.

“Serikali haitavumilia wakandarasi wanaosuasua katika utekelezaji wa miradi wanayoisimamia kwa kisingizio cha fedha. Fedha kutoka kwa wafadhili inapochelewa, wao watumie fedha zao kwani uhakika wa kulipwa upo,” alisisitiza.

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa Makambako – Songea, Dkt Kalemani aliwataka Maofisa wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wanaosimamia miradi mbalimbali ya umeme nchini kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi ipasavyo ili kukamilisha miradi husika kwa wakati na viwango vinavyotakiwa.

Alisema, Mradi wa Makambako – Songea ni mojawapo ya Miradi muhimu kwa Taifa, hususan kwa wananchi wa maeneo husika hivyo ni lazima ukamilike kwa wakati uliopangwa ambao siyo zaidi ya mapema 2018.

Naibu Waziri alisema kuwa, matarajio ya Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025, vijiji vyote vya Tanzania vinakuwa na umeme hivyo ni lazima kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo hayo.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo, Meneja wa Mradi husika, Mhandisi Didas Lyamuya alisema kuwa Mradi wa Makambako – Songea unatekelezwa chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now-BRN) na unalenga kuunganisha umeme kutoka makambako hadi songea na kunufaisha wananchi katika maeneo husika yaani mikoa ya Njombe na Ruvuma.

Aidha, Mhandisi Lyamuya aliongeza kuwa, Mradi huo ni wa umeme wa kilovolti 220 kwa umbali wa kilomita 250 na umelenga kuwanufaisha watu 22,700 katika vijiji 120 vya maeneo husika.

Naibu Waziri Kalemani yupo katika ziara kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme katika mikoa ya Iringa, Njombe, Katavi na Rukwa. Ziara hiyo inatarajiwa kuhitimishwa mwishoni mwa mwezi huu.

No comments: