Tuesday, June 21, 2016

Wananchi wa Chasimba waaswa kuwa wavumilivu.

Na Jacquiline Mrisho-MAELEZO.
Baada ya mtafaruku mkubwa kutokea katika Kijiji cha Chasimba kilichopo katika Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam na kuwaacha wakazi wa eneo hilo katika hali ya sintofahamu juu ya maisha yao ya siku zijazo, wakazi wa eneo hilo wamepata ahueni baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Willium Lukuvi kuingilia kati na kutoa suluhu ya mtafaruku huo.

Mgogoro huu baina ya wananchi wa Kijiji cha Chasimba na mwekezaji wa Kiwanda cha Saruji cha Twiga, Bw. Alfonso Rodriguez kilichopo Wazo Hill ambao ulianza takribani miaka 15 iliyopita baada ya Mkurugenzi huyo kugundua kuwa wananchi wamevamia eneo lake na kujenga makazi yao.

Hayo yalitokea baada ya kiwanda hicho kushindwa kuilinda mipaka yake kwa muda mrefu na kusababisha wananchi kujenga maeneo hayo na kukaa kwa muda mrefu sana hali iliyowapelekea kujiona kama wana haki na eneo hilo na kukataa kuhama.

Mkurugenzi Msaidizi Usanifu wa Miji na Uendelezaji Upya Maeneo wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Immaculata Senje alisema kuwa eneo hilo ni mali ya mwekezaji wa Kiwanda hicho.

"Ni ukweli usiofichika kuwa eneo hili la Chasimba ni mali ya mwekezaji na ana hati ya mwaka 1957 aliyopewa na Wizara yetu inayoonyesha ukubwa na mipaka ya eneo lake kwahiyo wananchi ndio wavamizi wa eneo hilo".anakiri Bi. Senje.

Mgogoro huo ulileta tafrani kubwa baada ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kutoa agizo kuwa wananchi waliojenga katika eneo hilo wahame mara moja na kwenda eneo ambalo wamepangiwa na Wizara ambapo takribani wakazi 30 waligoma kuondoka katika eneo hilo na kuamua kwenda mahakamani kudai haki yao, hatua ambayo haiukupata suluhu ya mgogoro.

Ili kuwasaidia wakazi wa Chasimba, Waziri Lukuvi aliamua kuingilia kati kwa kufanya mazungumzo ya amani na muwekezaji wa kiwanda hicho ambapo alimuomba Mkurugenzi huyo kuwaachia wakazi wa Chasimba sehemu hiyo kwa makubaliano maalumu watakayoafikiana.

Hatimaye mazungumzo baina ya wawili hao yalileta picha mpya kwa wakazi wa Chasimba baada ya Muwekezaji kukubali kuachia sehemu ya eneo lake kwa ajili ya makazi ya wananchi hao.

Mnamo Mei 13 mwaka 2015 ulifanyika Mkutano wa hadhara wa kutangaza kurudisha eneo hilo kwa wananchi, mkutano huo uliokutanisha uongozi wa wizara, uongozi wa kiwanda cha saruji, uongozi wa Manispaa ya Kinondoni, Shirika la Umeme Tanzania, Idara ya Maji, Polisi, Mbunge wa Kawe Halima Mdee ambao walipewa maagizo mbele ya wakazi wa Chasimba ya kupanga eneo hilo kuwa la makazi.

"Sasa natamka rasmi kuwa ardhi hii imerudishwa kwa wananchi na imeshabadilishwa kutoka kuwa ardhi ya biashara na kuwa ardhi ya makazi kwahiyo nimeongozana na wahusika ambao watalipanga eneo hili kwa kuzingatia dhana ya mpango shirikishi ambapo kamati ya wananchi itashirikiana na wataalamu wa wizara yetu katika upangaji wa eneo hilo ili kuwezesha uwekaji wa huduma za jamii",alisema Lukuvi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bw. Rodriguez anakiri kuwa mgogoro huo ulikuwa ni wa mda mrefu na umekuwa ukiwanyima usingizi kwahiyo, alimpongeza  Waziri Lukuvi kwa kumaliza mgogoro huo na kuwaahidi wakazi hao kushiriki katika ujenzi wa miundombinu.

Hatimaye eneo la Chasimba sasa limekuwa rasmi la wakazi wa Chasimba, eneo hilo lina takribani Kaya 4,096, wastani wa watu watano kila kaya  na jumla ya takribani watu 20,480.

Akizungumzia hatua hiyo, Mkazi mmoja wa Chasimba Juma Athumani alieleza kufurahi baada ya mgogoro huo kuisha.

"Nimeishi hapa kwa miaka 30, sasa nina watoto 11 na wajukuu kadhaa katia eneo hili, hapo awali mwekezaji aliposema tutoke kuwa eneo hili ni lake nilikua sielewi kabisa lakini nimefurahi sana kwa hatua hii iliyofikiwa". Alisema Athumani.

Tangu kuisha kwa mgogoro huu Mwezi Mei mwaka 2015, wizara inajitahidi kuendana na kasi ya "hapa kazi tu" iliyotolewa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuanza kupima viwanja kwa ajili ya wananchi hao ambapo hadi kufikia Mei 31 mwaka 2016 jumla ya viwanja 491 vimeshapimwa kati ya viwanja 2180 vinavyotarajiwa kupimwa katika eneo hilo.

Wizara ina malengo ya kumaliza kupima viwanja hivyo ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu na baada ya hapo wananchi hao wataletewa huduma za kijamii zikiwemo za Afya, shule,sehemu za kuabudu,viwanja vya michezo,miundombinu ya umeme, maji  pamoja na barabara.

Wizara inawataka wananchi kuwa wavumilivu na kuacha kulalamika kwa kuwa wizara inaendelea na kazi katika eneo hilo na  kila kitu kinaenda kwa wakati kwamba baada ya upimaji wa maeneo kuisha ndipo huduma za kijamii zitafuata.

Mkurugenzi Immaculata alisema "wakazi wa Chasimba mnatakiwa kuelewa kuwa kila kitu kinatakiwa kufanywa kwa kufuata sheria kwahiyo lazima twende taratibu ili kuepuka migogoro mingine kutokea, tunawasihi wakazi wa kijiji hicho kusubiri upimaji uishe ndipo huduma za kijamii zifuate".

Kila Mtanzania anahitaji kuishi kwa amani na utulivu katika sehemu aliyoichagua na kuiridhia lakini kutokana na nchi kuongozwa na sheria katika kila jambo basi hakuna budi kufuata sheria za ardhi zilizowekwa ili kuepuka usumbufu pamoja na migogoro inayopelekea kuwa na ugomvi na mauaji yanayosababisha amani kutoweka na kurudi nyuma kwa maendeleo ya mtu mmoja au Taifa zima.

Wahenga wanasema,"heshimu wenzio ili nawe uheshimiwe", shukrani kwa wakazi wa Chasimba kuwa wavumilivu wakati Serikali inakamilisha taratibu za kuendeleza eneo hilo  kwa kupima viwanja halali na baadae kuwekewa miundombinu ya kijamii .

Lakini pia ni vyema wakazi hao wakafuata sheria ili kuhakikisha kwamba hakuna mtu au mamlaka yoyote itakayowasumbua kwenye eneo lao ambalo watakuwa wakilimiki kihalali.

No comments: