Friday, June 17, 2016

TANZANIA NA SWEDEN ZATILIANA SAINI KUSHIRIKIANA KIMAENDELEO, MJINI DODOMA

Benny Mwaipaja, WFM -DODOMA


SERIKALI za Tanzania na Sweden zimetiliana saini mkataba wa ushirikiano wa miaka 4 kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2019 utakaojikita kuimarisha uchumi wa nchi na maendeleo ya watu katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, utafiti, nishati jadidifu na kupambana na umasikini.

Tukio hilo limefanyika leo Juni 16, 2016, mjini Dodoma kati ya Katibu Mkuu na mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Servacius Likwelile kwa upande wa Tanzania na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Kimaendeleo wa Sweden, Mhe. Ulrika Modeer.

Dkt. Likwelile ameeleza kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka 2019, Serikali ya Sweden itatoa ruzuku ya fedha za Kiswidi, SEK 5.5 Biln, sawa na shilingi Trilioni 1.42 za Kitanzania.

Amesema kuwa kutiwa saini kwa mkataba wa ushirikiano huo kutafuatiwa na utiwaji saini wa mikataba ya kifedha ambapo fedha hizo zitaelekezwa katika miradi kadhaa ikiwemo kusaidia Elimu, Maendeleo ya Jamii-TASAF, Utafiti, Nishati, Demokrasia, Haki za Binadamu, na Sekta Binafsi.

"Ushirikiano huu umelenga kusaidia kujenga mazingira ya maendeleo endelevu na kuwapatia Watanzania maskini fursa za kujikwamua katika umaskini kwa kujipatia ajira na kuweza kuanzisha biashara za kujipatia kipato ambapo vikundi vinavyolengwa zaidi ni wanawake, watoto na vijana" Alisema Dkt. Likwelile

Dkt. Servacius Likwelile ametoa wito kwa Serikali ya Sweden na nchi nyingine duniani kuwekeza katika biashara na vitega uchumi ili ziweze kunufaika na rasimali kubwa ambazo nchi imejaaliwa ikiwemo maliasili, ardhi yenye rutuba na jiografia ya kimkakati inayochochea uwekezaji na biashara

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ushirikianno na Maendeleo ya Kimataifa wa Sweden Mhe. Ulrika Modeer, amepongeza uongozi mahili wa Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kupambana na vitendo vya kifisadi ikiwemo rushwa.

"Sweden inaunga mkono kwa nguvu zote hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli kupambana na mauvu nchini na tunaamini nchi itapiga hatua kubwa kimaendeleo" Alisistiza Modeer.

Mhe. Ulrika Modeer ameahidi kuwa serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa kutoa fedha kupitia mfuko mkuu wa Bajeti ili kuwezesha kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo inayogusa hifadhi ya mazingira, kilimo endelevu, kuwawezesha wananawake kiuchumi na kumsaidia mtoto wa kike na kiume kielimu.

"Tunataka kuona kuwa maendeleo ya nchi yanakwenda sambamba na maendeleo ya wananchi wake ambapo tunaamini kuwa utafiti utasaidia kupata njia bora za kupambana na umasikini"Alisisitiza Mhe. Modeer

Amesema kuwa pamoja na nchi yake kutaka kuyasaidia makundi mbalimbali wakiwemo watu wenye ulemavu, wanataka kuona suala la demokrasia na utawala bora vinapewa kipaumbele katika mipango mbalimbali ya maendeleo

"Vilevile uwekezaji wetu mkubwa wa fedha katika maendeleo ya Taifa hautakuwa na maana sana kama suala la hifadhi ya mazingira halitapewa kipaumbele kwa kuanzisha miradi ya nishati jadidifu "Renewable energy" ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi: aliongeza Mhe. Ulrika Modeer

Uhusiano wa Tanzania na Sweden umedumu tangu mwaka 1960 ambapo katika kipindi chote cha miaka 50, serikali hizi mbili zimeshirikiana katika kubuni na kutekeleza miradi kadhaa ya maendeleo

Programu na miradi itakayotekelezwa katika ushirikiano uliosainiwa leo unaendena pia na Mpango wa Taifa wa Pili wa Miaka Mitano unaoanzia mwaka 2016/17 hadi 2020/21 na unalenga kuondoa utegemezi wa misaada kwa Tanzania. 


Katibu Mkuu Wizara ra Fedha na Mipango, Dkt. Servacius Likwelile (kushoto), na mgeni wake, Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Kimataifa wa Sweden Mhe. Ulrika Modeer (kulia), wakipeana mikono na kubadilishana hati za mkataba baada ya kutiliana saini mkataba wa ushirikiano wa maendeleo wa miaka minne kuanzia mwaka 2016 hadi 2019, tukio lililofanyika katika Ofisi za Hazina Mjini Dodoma leo, Juni 16, 2016.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Servacius Likwelile (kushoto), akizungumza jambo wakati wa hafla fupi ya Tanzania na Sweden, kutiliana saini mkataba wa ushirikiano wa kimaendeleo, wa miaka minne kuanzia 2016 hadi 2019, tukio lililofanyika katika Ofisi za Hazina Mjini Dodoma leo, Juni 16, 2016.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Servacius Likwelile (kushoto), na mgeni wake, Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Kimataifa wa Sweden Mhe. Ulrika Modeer (kulia), wakipeana mikono na kubadilishana hati za mkataba baada ya kutiliana saini mkataba wa ushirikiano wa kimaendeleo wa miaka mine kuanzia mwaka 2016 hadi 2019, tukio lililofanyika katika Ofisi za Hazina Mjini Dodoma leo, Juni 16, 2016
Baadhi ya Maofisa wa serikali ya Tanzania wakifuatilia kwa makini tukio la kutiliana saini mkataba wa ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na Sweden, utakao chukua miaka minne kuanzia 2016 hadi 2019, tukio lililofanyika katika Ofisi za Hazina Mjini Dodoma leo, Juni 16, 2016
Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Kimataifa wa Sweden Mhe. Ulrika Modeer (kulia), akizungumza jambo wakati wa hafla fupi ya Tanzania na Sweden, kutiliana saini mkataba wa ushirikiano wa kimaendeleo wa miaka minne kuanzia 2016 hadi 2019, tukio lililofanyika katika Ofisi za Hazina Mjini Dodoma leo Juni 16, 2016. 
Ujumbe wa Sweden ukiongozwa na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Kimataifa wa Sweden Mhe. Ulrika Modeer (Katikati), wakifuatilia kwa makini tukio la kutiliana saini mkataba wa ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na Sweden, utakao chukua miaka mine kuanzia 2016 hadi 2019, tukio lililofanyika katika Ofisi za Hazina Mjini Dodoma leo, Juni 16, 2016
Baadhi ya Maofisa wa serikali ya Tanzania akiwemo Mkurugenzi wa Tasaf Ladislaus Mwamanga (kushoto) wakifuatilia kwa makini tukio la kutiliana saini mkataba wa ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na Sweden, utakao chukua miaka minne kuanzia 2016 hadi 2019, tukio lililofanyika katika Ofisi za Hazina Mjini Dodoma leo, Juni 16, 2016.

No comments: