Wednesday, June 1, 2016

SERIKALI YATOA UFAFANUZI UBORESHAJI WA MASLAHI YA POLISI NA MAFUNZO YA JKT



 Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson akiongoza kikao cha 34 cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo mjini Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akifurahia jambo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye ndani ya Ukumbi wa Bunge kabla ya kuanza kwa kikao cha 34 cha Mkutano wa 3 wa Bunge mjini Dodoma.

 Wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari Moga iliyoko jijini Dar es salaam wakifuatilia shughuli za kikao cha 34 cha Bunge mjini Dodoma. Wanafunzi 90 wa shule hiyo wamelitembelea Bunge hilio kujifunza namna linavyoendeshwa.
 Baadhi ya Mawaziri na Wabunge wakiwa ndani ya Ukumbi wa Bunge wakati wa kikao cha 34 mjini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Malisili na Utalii Mhe. Ramo Makani akijibu maswali ya Wabunge yaliyoelekezwa kwenye wizara hiyo wakati wa kipindi cha Maswali na majibu leo, Dodoma.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Muhagama akitoa ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya utendaji wa Serikali ndani ya ukumbi wa Bunge leo mjini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa Fedha 2016/2017 leo mjini Dodoma. Wizara hiyo inaliomba Bunge lipitishe kiasi cha shilingi Trilioni 8.7 kwa ajiri ya matumizi ya kawaida na matumizi mengine.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (kushoto) na Naibu wake Dkt. Ashatu Kijaji wakiandika maoni ya Wabunge waliokuwa wakichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara Fedha na Mipango kwa mwaka wa Fedha 2016/2017 leo mjini Dodoma.
 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa(kulia) akimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina nje ya Ukumbi wa Bunge leo.
 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa(kushoto) akisalimiana na Mbunge wa Kilolo Mhe. Venance Mwamoto nje ya Ukumbi wa Bunge, Dodoma.
 Baadhi ya Walimu na Wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari Moga iliyoko jijini Dar es salaam wakiwa katika picha ya pamoja nje ya Ukumbi wa Bunge mara baada ya kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge kufuatilia shughuli za kikao cha 34.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (kushoto) akizungumza jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Suzan Kolimba (kulia) kwenye viwanja vya Bunge, Dodoma. 

Na. Aron Msigwa- DODOMA.
SERIKALI imesema kuwa itaendelea kuboresha maslahi ya askari wa Jeshi la Polisi na kuwajengea nyumba za kisasa za kuishi ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina wakati akijibu maswali ya wabunge kuhusu mkakati wa Serikali wa kuboresha maslahi ya Askari wa Jeshi hilo kwa niaba ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Bungeni mjini Dodoma leo
Amesema kuwa Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017 itatekeleza Mpango kabambe wa ujenzi wa nyumba za Polisi 4136 ambao utakwenda sambamba na ujenzi wa vituo vya Polisi.

Amesema Serikali imechukua hatua za haraka kulishughulikia suala la ukosefu wa nyumba za askari hao katika maeneo mbalimbali nchini ili kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yenye ukosefu wa nyumba hizo.

Amelieleza Bunge kuwa Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa maslahi ya Askari Polisi yanaimarishwa ikiwemo malipo ya Posho ya pango kwa askari wasio na nyumba ambayo ni asilimia 15 ya mishahara yao ili waweze kulipia gharama hizo.

Ameongeza kuwa  askari wenye utalaam maalum wakiwemo madereva na madaktari wamekuwa wakilipwa posho ya asilimia 15 ya mishahara yao na kuongeza kuwa askari wanaoajiriwa katika ajira mpya kama madaktari wamekuwa wakilipwa mishahara sawa na madaktari wengine bila kujali vyeo vyao.

“Serikali tumefanya jitihada kubwa sana kuboresha maslahi ya askari wetu, kama Serikali tumetoa posho za nyumba, posho za utalaam maalum kwa askari wote ambayo ni asilimia 15 ya mshahara wa kila Polisi hii yote ni kuwafanya askari wetu waweze kumudu gharama za maisha” Amesisitiza Mhe. Mpina.
Ameeleza kuwa kwa askari wanaofanya kazi katika mazingira magumu wakiwemo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wamekuwa wakipewa posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu (Hardship allowance) kiasi cha shilingi laki moja (100,000) kila mwezi.
Mhe. Mpina amebainisha kuwa askari wote wanaohitimu mafunzo yao wamekuwa wakikatiwa Bima ya Afya kwa asilimia 100 na Serikali pamoja na udhamini wa mikopo mbalimbali katika taasisi za kifedha ili waweze kupewa mikopo na taasisi hizo.
Aidha, amesisitiza kuwa serikali imewapandishia kiwango cha Posho ya katikati ya mwezi (Ration Allowance) kutoka shilingi 180,000 za awali hadi 300,000 ambazo wanalipwa kwa sasa nchi nzima.
Katika hatua nyingine Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imetoa ufafanuzi kuhusu vijana wa kidato cha nne kutochukuliwa kujiunga na  Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi  amesema kuwa hatua ya kuwachukua vijana wote wanaomaliza kidato cha nne kwa sasa haiwezekani kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wa Serikali.
Amesema kuwa uwezo wa JKT kuchukua vijana wa kujitolea kwa sasa ni 5000 hadi 7000 kwa mwaka kulingana na bajeti inayotolewa na kuongeza kuwa mpango wa Serikali ni kuendelea kutenga fedha na kujenga kambi zaidi za mafunzo ili kuwawezesha vijana wengi kujiunga  na mafunzo hayo kulingana na upatikanaji wa fedha.
Kwa upande wa wahitimu wa kidato cha sita wanaotakiwa kujiunga na JKT kwa mujibu wa Sheria Mhe. Mwinyi amesema Serikali imewachukua vijana 14,000 na inaendelea kujenga uwezo wa ndani wa kuchukua vijana wengi zaidi.
Amesema Serikali inakusudia kujenga majengo ndani ya makambi ili kuwezesha vijana wote wanaohitimu kidato cha sita kupitia JKT kabla ya kujiunga na vyuo mbalimbali hapa nchini.
Aidha, Amefafanua kuwa kwa wale wanaojiunga na JKT kwa kujitolea ambao idadi yao inafikia 5000 sio wote wanaopata nafasi ya kuajiriwa katika vyombo vya Ulinzi na Usalama na kuongeza kuwa ni asilimia 71 ndio hupata ajira kwenye vyombo hivyo huku waliobaki wakilazimika kurudi nyumbani.
Amebainisha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inaangalia utaratibu wa kuwawezesha vijana hao ili wanaporudi uraiani waweze kupatiwa mitaji ya kuwawezesha kujiajiri wenyewe.

No comments: