Monday, June 20, 2016

PSPF YAJA NA MPANGO WA KUKUTANA NA WANACHAMA WAKE NA KUPOKEA MAONI

Mfuko wa Pensheni wa PSPF leo hii umeanzisha rasmi mpango wa kukutana na wanachama wake na baadhi ya wajasiriamali jijini ili kupokea maoni na kuwahamasisha kujiunga na Mpango wa Uchangiaji wa Hiari (PSS) ili kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na mpango huo.

Akizungumza katika mkutano na wanachama na wajasiriamali kutoka soko la samaki la Feri Jijini Dar, Afisa Uendeshaji wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Hadji Jamadary alisema kuwa mbali na kupokea maoni wanaendelea kutoa elimu ya juu ya mpango huo wa hiari ambapo mwanachama atakuwa huru kuchagua muda wa kuchangia kutegemea kipato chake huku kiwango cha chini kikianzia Shilingi 10,000 ambayo mwanachama anaweza kulipia kupitia benki na huduma za simu.

Bwana Hadji alisema kuwa mpango huo wa hiari unakaribisha raia na mtu asiye raia bila kusahau mjasiriamali na mfanyakazi wa serikali na kuongeza kuwa mwanachama anayejiunga katika mfuko huo huweza kupata mafao ya aina sita ambayo ni; Fao la Elimu, Fao la Ujasiriamali, Fao la Uzeeni, Fao la Kifo, Fao la Ugonjwa/Ulemavu, Fao la Kujitoa, na Fao la Matibabu.

Akifafanua kuhusu Fao la Matibabu, Bwana Hadji alisema kuwa kupitia mpango wake wa uchangiaji wa hiari wanashirikiana na mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambapo mwanachama ataweza kupatiwa huduma bure katika hospitali na maduka ya madawa yaliyosajiliwa na NHIF kote nchini.

“Mwanachama anaweza kuwasajili pia wategemezi wake watano na kuendelea kupata mafao yetu bila shida yoyote,” alisema Hadji.

Wakizungumza kwa nyakati mbalimbali wajasiriamali hao walionesha kufurahia unafuu wa mfuko huo na kuwataka PSPF kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili wananchi wengi wajiunge kwa kuwa hupoteza fedha nyingi ambazo wangeweza kuziokoa kwa kujiunga na mfuko huo.

Aidha Hadji aliwaambia wanachama hao kuwa PSPF ina mpango wa kuwawezesha wanachama wake na jamii kwa ujumla kumiliki nyumba zilizopo Dar , Morogoro, Tabora, Mtwara, Shinyanga na Iringa ambapo wataweza kununua kwa mkopo au malipo ya mara moja pamoja na mikopo ya viwanja vilivyo sehemu mbalimbali nchini.
Afisa Mwendeshaji kutoka Mfuko wa Pensheni wa PSPF Hadji Jamadary akiongea na wavuvi,Wafanyabiashara ya samaki pamoja na wajasiliamali waliopo katika soko la Samaki la Feri.
Katibu Kamati ndogo ya Utawala na Biashara Soko la Samaki la Feri Bw. Daudi Chiwinga akizungumza jambo wakati wa mkutano huo wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF na wadau wake.
Afisa Mwendeshaji Msaidizi kutoka Mfuko wa Pensheni wa PSPF Nahshon Mshabaa akigawa fomu za kujiunga n NHIF kwa wadau wake wakati wa mkutano huo wa kupokea maoni na kuwaelimisha zaidi juu ya bidhaa za mfuko wa pensheni wa PSPF.
Afisa Mwendeshaji Msaidizi kutoka Mfuko wa Pensheni wa PSPF Nahshon Mshabaa akiwasaidia kujaza fomu wanachama wapya ambao ni wajasiliamali kutoka soko la Samaki la Feri waliojiunga na Mpango wa hiari wa PSPF.
Afisa Mwendeshaji kutoka Mfuko wa Pensheni wa PSPF Hadji Jamadary akiwaonesha wajasiriamali kutoka Soko la Samaki la Feri(Hawapo pichani) mafao yatolewayo na Mpango wa Uchangiaji wa Hiari wa PSPF.
Baadhi ya wajasiliamali kutoka soko la Samaki la Feri wakitoa maoni yao na kuuliza maswali mbalimbali kwa ma afisa wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF wakati wa Mkutano huo.
Wajasiliamali na wadau wa PSPF wakitazama moja ya kipeperushi ambacho ni cha Mkopo wa viwanja.
Mmoja wa wajasiliamali kutoka Soko la Samaki la Feri akipokea kadi yake ya Mpango wa uchangiaji wa hiari (PSS) kutoka Mfuko wa Pensheni wa PSPF bwana Hadji Jamadary.
Baadhi ya ya wajasiliamali kutoka katika Soko la Samaki la Feri wakisikiliza kwa makini wakati Mfuko wa Pensheni wa PSPF ulipokwenda kuwatembelea kwa lengo la kupata maoni kwa wadau wake na kuwapa elimu zaidi juu ya mfuko huo.

No comments: