Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akiongoza kikao kilichoshirikisha Watendaji kutoka Benki ya Dunia pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake ikiwa ni pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) na Wakala wa Serikali wa Uagizaji wa Mafuta ya Pamoja (PBPA).
Mtendaji Kutoka Benki ya Dunia anayeshughulikia mazingira Vladislav Vucetic, akielezea mikakati ya benki hiyo katika ushirikiano wake na Serikali ili kupanua sekta za nishati na madini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Profesa Justin Ntalikwa (kushoto waliokaa mbele) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya Nishati Dkt. Juliana Pallangyo ( wa pili kutoka kushoto waliokaa mbele) wakifuatilia kwa makini maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo( hayupo pichani) katika kikao hicho.
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ameelezea mikakati ya Serikali katika uboreshaji wa sekta za nishati na madini na kuongeza kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) katika uboreshaji wa sekta hizo ili ziwe na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Profesa Muhongo aliyasema hayo alipokutana na Watendaji kutoka Benki ya Dunia pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake ikiwa ni pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) na Wakala wa Serikali wa Uagizaji wa Mafuta ya Pamoja (PBPA).
Akizungumzia Sekta ya Nishati nchini Profesa Muhongo alisema kuwa serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa Sekta ya nishati inakuwa na mchngo mkubwa katika ukuaji wa uchumi na kutoka katika kundi la nchi masikini duniani na kuingia katika kundi la nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 kama Dira ya Maendeleo ya Taifa ifanvyofafanua.
Aliongeza kuwa, Serikali kwa mara ya kwanza imetenga asilimia 40 ya bajeti yake katika miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ya umeme na kuendelea kufafanua kuwa katika bajeti ya Wizara ya mwaka wa fedha 2016/17, Wizara imetenga asilimia 94 ya bajeti yake katika miradi ya maendeleo, ambapo katika Idara ya Nishati asilimia 98 itakwenda kwenye miradi ya umeme.
Waziri Muhongo alisema kuwa ili kuimarisha Sekta ya Nishati, Wizara imepanga kupanua sekta ya nishati kwa kukaribisha wawekezaji binafsi kuwekeza katika sekta ya uzalishaji na uuzaji wa umeme pamoja na kuwapo kwa mwongozo utakaowawezesha kuzalisha umeme.
Alindelea kusema kuwa Wizara inatarajia kuimarisha usambazaji wa umeme vijijini kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na TANESCO.
Profesa Muhongo aliendelea kutaja mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuimarisha mradi wa usambazaji wa umeme wenye msongo wa kilovolti 400 kupitia Iringa, Mbeya, Tunduma hadi katika eneo la Kabwe nchini Zambia na kusisitiza kuwa upembuzi yakinifu unatarajia kukamilika mapema Desemba mwaka huu kabla ya kuanza kwa mradi.
Aliendelea kutaja miradi mingine kuwa ni pamoja na mradi wa usambazaji umeme kupitia Mbeya, Sumbawanga, Mpanda, Kigoma, Nyakanazi na kuiomba Benki ya Dunia kushirikiana na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) ili kufanikisha mradi huo.
“Kuna mradi wa kuunganisha Tanzania na Uganda ujulikanao kwa jila la Tanzania – Uganda inter-connector unaounganisha Mwanza, Geita, Nyakanazi, Kyaka- Bukoba hadi Masaka nchini Uganda.
Akizungumzia Sekta ya Gesi Profesa Muhongo alieleza kuwa serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha nishati ya gesi inatumika ipasavyo katika uzalishaji umeme pamoja na kusambazwa katika matumizi ya majumbani.
Aliongeza kuwa serikali imeweka mikakati ya kusambaza gesi majumbani kwa ajili ya matumizi ya kupikia katika mikoa ya Dar es salaam, Lindi, Mtwara na katika maeneo mengine ya Pwani.
Akielezea Sekta ya Madini Profesa Muhongo aliiomba Benki ya Dunia kusaidia katika ununuzi wa vifaa vya madini kwa wachimbaji wadogo pamoja na katika kuwapatia elimu kuhusu mazingira, uchenjuaji wa madini na kuongeza ajira hususan katika maeneo ya madini yaliyopo vijijini.
Naye Mtendaji Kutoka Benki ya Dunia anayeshughulikia mazingira Vladislav Vucetic alisema Benki ya Dunia ipo tayari kushirikiana na Serikali katika uendelezaji wa sekta za nishati na madini ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment