Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia maadhimisho kulia ni Bi. Mindi Kasiga na Bw. Arnold Mchemwa.
==================================================
WAZIRI WA MAMBO YA NJE ASHIRIKI KUMBUKUMBU YA MAUAJI YA KIMBARI DHIDI YA WATUTSI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) ameshiriki maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda dhidi ya Watutsi, yaliyoandaliwa na kuratibiwa na Ubalozi wa Rwanda nchini chini ya Mhe. Balozi Eugene Kayihura yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Waziri akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya kumbukumbu hiyo alieleza namna mauaji hayo ya Kimbari yaliyotokea mwaka 1994 yalivyoleta simanzi na majonzi kwa wananchi wa Rwanda, nchi majirani wa Rwanda ambao sehemu yao ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Afrika nzima na Duniani kwa ujumla kwakuwa mauaji hayo yalipoteza maisha ya Wanyarwanda wasio na hatia zaidi ya laki nane (800,000) ndani ya siku mia moja (100).
"Nilishuhudia madhara ya mauaji hayo mwezi Agosti 1994, wakati huo nikiwa Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nikisimamia masuala ya Wakimbizi nchini Rwanda, hali niliyoikuta siku chache baada ya mauaji hayo ilikuwa ya kusikitisha na inayotisha kwakua ardhi ilikuwa imejaa miili ya watu waliouawa wa rika zote sambamba na mito iliyokuwa imefurika miili hiyo" alisema Waziri Mahiga.
Pia alitumia nafasi hiyo kueleza kuwa ni wakati sasa mataifa ya Afrika yakaangalia namna ya kuendesha masuala ya kisiasa na ulinzi katika hali ya amani pasipo kuharibu utulivu wa Taifa husika ili kuepuka kuharibu maisha ya watu wasio na hatia pamoja na nguvu kazi kubwa ambayo ndio tegemeo la kuleta maendeleo sambamba na kukuza uchumi.
Aidha Mhe. Mahiga alieleza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais wa awamu ya tano Mhe. John Pombe Magufuli itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Rwanda katika jitihada za kupigania na kukemea mauaji kama hayo na kuhakikisha hayajirudii tena nchini Rwanda wala kutokea tena katika Taifa lolote barani Afrika na Duniani kwa ujumla. Alisema katika mahusiano ya kidiplomasia, yanapotokea machafuko yanayo hatarisha amani yanaharibu shughuli za kidiplomasia zinazoendelea baina ya mataifa husika.
Balozi wa Rwanda nchini Tanzania Mhe. Eugene Kayihura naye alitoa pole kwa wahanga wote walionusurika na mauaji hayo na pia akatoa wito kwa Wanyarwanda wote popote walipo kuzidi kuwafariji na kuwa karibu na wahanga hao ili waweze kujisikia wapo na ndugu zao na kuwa na matumaini na maisha ya sasa na ya baadae ili waweze kuendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuinua uchumi wa Rwanda.
"Jumuiya zote za Kinyarwanda popote zilipo zihakikishe zinakuwa ndugu kwa wahanga walionusurika na mauaji hayo na kuzidi kuwapa matumaini ya maisha ya baadae ili kuondoa kisasi dhidi ya jamii iliyosababisha mauaji ya ndugu zao" Balozi Kayihura alisema.
Vilevile Mhe. Kayihura alitumia fursa hiyo kumshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kwa kufanya ziara nchini Rwanda na kushiriki maadhimisho ya kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari pamoja na kutembelea maeneo ya kihistoria ya mauaji hayo akiwa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame mapema mwezi April mwaka huu.
Maadhimisho ya kumbukumbu hiyo hapa nchini yalihudhuriwa na mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa, Jumuiya ya Kinyarwanda iliyopo nchini na Watanzania wengine walioalikwa kushiriki maadhimisho hayo wakiwemo wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wa Sekondari ya Wasichana ya Jangwani.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 10 Juni 2016.
|
No comments:
Post a Comment