Thursday, June 23, 2016

KAMATI YA ICGLR-RINR YAZINDULIWA, KUIMARISHA USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA MADINI NCHINI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe akimkabidhi Mratibu Mkuu wa ICGLR, Balozi Samuel Shilukindo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje (Mwenyekiti) vitendea kazi wakati akizindua Kamati ya Kimataifa ya Kusimamia Utekelezaji wa Mpango wa ICGLR Tanzania jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (mbele) na kulia kwake aliyesimama ni Mratibu Mkuu wa ICGLR, Balozi Samuel Shilukindo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje akisoma hotuba wakati wa uzinduzi na wengine katika picha ni wanakamati.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (mbele) na wajumbe wa kamati hiyo wakimsikiliza Kaimu Kamishna wa Madini Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ally Samaje (aliyesimama) akitoa mada katika uzinduzi uliofanyika katika Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe wa nne kutoka kulia akiwa pamoja na Kamati ya Kimataifa ya Kusimamia Utekelezaji wa Mpango wa ICGLR Tanzania na Wajumbe kutoka Wizara ya Nishati na Madini wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumaliza uzinduzi wa Kamati hiyo.

Na Rhoda James

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia madini Profesa James Mdoe kwa Niaba ya Katibu Mkuu, Profesa Justin Ntalikwa tarehe 22 Juni, 2016 alizindua Kamati ya Kimataifa ya Kutekeleza Mpango ujulikanao kama International Conference on the Great Lakes Regional Initiative Against Illegal Exploration of Natural Resources (ICGLK- RINR) katika Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam.

Profesa Mdoe alisema kuwa lengo la Mpango wa ICGLR- RINR ni kuweka mfumo wa usimamizi wa uchimbaji, uchenjuaji, usafirishaji na uuzaji wa madini ili kuhakikisha kuwa shughuli hizo zinafanywa kihalali na hazitumiwi na vikundi au watu wanaohusika katika kuendeleza migogoro na vita.

Aliongeza kuwa Mpango wa ICGLR-RINR ulianzishwa kutokana na juhudi za Kimataifa za kukabiliana na vita na machafuko katika eneo la maziwa makuu. Ushirikiano wa awali wa Kimataifa katika nchi za maziwa makuu ulianzishwa mwaka 1999, mwaka 2003 nchi hizo zilikutana kwa ushawishi wa umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) na Asasi ya Kiraia ijulikanayo kama Group of Friends (GoF) ili kutafuta suluhisho la migogoro katika eneo la nchi za Maziwa Makuu.

Vilevile alisema kuwa juhudi hizo zilifanywa kwa msaada wa Washirika wa Maendeleo ya nchi za Maziwa Makuu ambazo zilipitisha Azimio la Dar es Salaam mwaka 2004, ikifatiwa na Tanzania kusaini Mkataba wa Usalama, Utengamano na Ustawi (Pact on Security, Stability and Development mnamo tarehe 15 Desemba 2006 jijini Dar es Salaam.

Aidha, Prof. Mdoe alifafanua kuwa, nchi zilizosaini Mkataba huo jijini Nairobi nchini Kenya zilikuwa ni pamoja na Tanzania, Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati-CAR, Jamhuri ya Congo- DRC, Kenya, Rwanda, Sudan, Uganda na Zambia.

Mkataba huo uliosainiwa Nairobi ulikuwa na Itifaki kumi zikiwa ni Ushirikiano wa Kiulinzi; Demokrasia na Utawala bora; Ushiriki wa Kimahakama; kudhibiti makosa ya mauaji ya kimbari; kujijenga na kujenga Ukanda wa Maendeleo.

Itifaki nyingine ni pamoja na Msaada kwa Washirika wa Maendeleo wa Kimataifa (International Development Partners (IDP); kuzuia unyanyasaji wa Kijinsia; Kulinda haki za Wanyonge; Upashaji Habari na Mawasiliano pamoja na Mapambano dhidi ya uvunaji haramu wa Rasilimali.

Pia alisema mwaka 2010, nchi za Maziwa Makuu zilisaini Azimio la Lusaka kuhusu Itifaki ya Mapambano dhidi ya Uvunaji Haramu wa Rasilimali – RINR na kuongeza kuwa Itifaki hii ilizingatia ukweli kwamba nchi za Maziwa Makuu ni wazalishaji wakubwa wa madini ya Tantalum na Niobium, Bati (Tin) tungsten na Dhahabu.

Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Madini Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ally Samaje alisema Utekelezaji wa Mpango wa ICGLR nchini Tanzania unaratibiwa na Wizara ya Nishati na Madini.

Alibainisha kwamba vipo Vipengele vya ICGLR – RINR, ambavyo tayari vimekamilika ikiwa ni pamoja na mpango wa uwazi katika Tasnia ya Uziduaji – EITI, kurasimisha uchimbaji mdogo (ASM formalization) na utumiaji wa kanzidata ambayo tayari inatumika.

Aidha, Kamishna Samaje alisema kuwa rasimu ya kanuni za Madini kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa ICGLR-RINR imetayarishwa na hatua za kuzikamilisha kanuni hizo zinaendelea.

“Ukamilishaji huu wa Kanuni za ICGLR utawezesha nchi yetu kuanza kutoa hati za ICGLR ifikapo Desemba 2018 wakati wa kusafirisha madini (ICGLR Reginal Certification) na kubadilishana taarifa za usafirishaji madini kupitia  Kanzidata ya madini,” alisema Mhandisi Samaje.

Naye Mratibu Mkuu wa ICGLR, Balozi Samuel Shilukindo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje aliishukuru Wizara kwa uundwaji na utekeleza wa Mpango huo ambao utasaidia Tanzania kufaidika na Rasilimali za Madini na kwamba Kamati hiyo sasa inalo jukumu kubwa la Kusimamia Utekelezaji wa Sheria na Kanuni za mpango huo.

No comments: