Uongozi wa Shamba la Kuku Maruhubi { Zanchick } umejipanga
kushirikiana na Wizara ya Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi katika kuwasaidia wafugaji na wakulima wadogo
wadogo Nchini ili waendeshe miradi yao ya uzalishaji katika misingi ya
kitaaluma.
Mkuu na muanzilishi wa Shamba hilo Dr. David Elua
akiuongoza ujumbe wa Viongozi watatu wa shamba hilo alieleza hayo wakati
akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini
kwake vuga Mjini Zanzibar.
Dr. David Elua alisema mpango huo uliolenga
kutekelezwa pande zote mbili za Muungano, Tanzania Bara na Zanzibar
utawanufaisha wanachi wa kipato cha chini zaidi ya 45,000 kwa kupata ajira
katika uendeshaji wa miradi ya ufugaji kuku kwa kutumia njia ya kisasa.Alisema katika hatua ya awali shamba hilo tayari
limeshatoa ajira zipatazo 300 katika kiwanda chake cha kutotoa vifaranga vya
Kuku kiliopo Maruhubi juhudi zikiwekwa zaidi katika kuunga mkono azma ya Serikali
Kuu katika uwekezaji wa viwanda vidogo vidogo.
Dr. David alimfahamisha Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar kwamba Sera hiyo iliyoanzishwa na Serikali na kuanza kukubalika kwa
baadhi ya mashirika na taasisi za uwekezaji ndani na nje ya nchi itawasaidia
zaidi vijana kupata ajira badala ya kusubiri ajira za serikali ambazo ni finyu
kwa miaka ya sasa.
Akizungumzia ugonjwa wa kuambukiza wa kipindupindu
ulioikumba Zanzibar katika Kipindi hichi Mkuu na Muanzilishi wa Shamba hilo la
Kuku Maruhubi Dr. David alisema Uongozi wake umepata mshtuko kutokana na janga
hilo linaloendelea kusumbua wananchi hasa Watoto wadogo.
Dr. David alisema Zanchick imeahidi kutoa mchango wa
shilingi Milioni 10,000,000/- ili zisaidie nguvu ya Serikali katika mapambano
yake dhidi ya maradhi hayo yaliyopoteza maisha ya watu wasiopungua 53 tokea
yavikumbe Visiwa vya Zanzibar mwezi septemba mwaka uliopita.
Akitoa shukrani zake kwa Uongozi wa Shamba hilo la
Kuku Maruhubi {Zanchick} Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kuzifanyia kazi
changamoto zote zinazoikumba Taasisi hiyo katika kuendesha miradi yake ya
uwekezaji hapa Nchini.
Balozi Seif alisema Serikali imeamua kuimarisha
miundombinu katika sekta mbali mbali za Uwekezaji ili kujenga mazingira bora
yatakayotoa fursa kwa Taasisi na Makampuni ndani na nje kuwekeza miradi yao ya
kiuchumi ili hatimae isaidie uchumi wa Taifa.
Shamba la Kuku Maruhubi ni miongoni mwa Taasisi za
uwekezaji zilizohamasika kuja kuwekeza miradi yao Nchini kufuatia ziara ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyoifanya Nchini Marekani mwezi
Oktoba mwaka 2011 kwa mualiko wa shirika la uwekezaji vitega uchumi Barani
Afrika la Nchini Marekani.
Ziara hiyo ya Balozi Seif ililenga kuitangaza
Zanzibar kwa taasisi na mashirika ya Marekani kuangalia uwezekano wa kuwekeza
miradi yao katika maeneo yaliyomo ndani ya Sekta za Utalii, Biashara, Elimu,
Kilimo, Afya, Miundombinu pamoja na Mazingira.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
6/5/2016.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif akisalimiana na Ujumbe wa Viongozi wa Shamba la Kuku
Maruhubi { Zanzchick } uliofika ofisini kwake kubadilishana mawazo juu ya sekta
ya uwekezaji.Aliyempa mkono ni Mkuu na muanzilishi wa shamba hilo
Dr. David Elua, wa kwanza kutoka kulia ni Meneja operesheni wa Shamba hilo Bw.
Christopher Kontonasios na wa kwanza kutoka kushoto ni Nd. Issa Kassim.
Balozi Seif akizungumza na Ujumbe
wa Viongozi wa Shamba la Kuku Maruhubi { Zanzchick } ukiongozwa na Mkuu na
muanzilishi wa Shamba hilo Dr. David Elua.
Balozi Seif akiwa katika picha ya
pamoja na Ujumbe wa Viongozi wa Shamba la Kuku Maruhubi { Zanzchick } mara
baada ya mazungumzo yao.Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu na muanzilishi wa
Shamba hilo Dr. David Elua, Bwana Michael Mantheakis, Nd. Issa Kassim na kushoto
ya Balozi Seif ni Meneja operesheni wa Shamba hilo Bw. Christopher Kontonasios.Picha na – OMPR – ZNZ.
No comments:
Post a Comment