Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Neema Rusibimayila (kushoto) akiongea na Waandishi wa Habari leo 6 Mei, 2016 Jijini Dar es Salaam kuhusu msaada walioupokea toka Shirika la Afya Duniani (WHO) wenye thamani ya shilingi bilioni 1.4.
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga,Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Neema Rusibimayila (kushoto) pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania Dkt. Rufaro Chatoro wakisaini hati za makabidhiano ya vifaa tiba leo 6 Mei, 2016 jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Neema Rusibimayila (kushoto) pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania Dkt. Rufaro Chatoro wakikabidhiana hati za makabidhiano ya vifaa tiba leo 6 Mei, 2016 jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania Dkt. Rufaro Chatoro (kulia) akikabidhi jokofu kwa kwa jaili ya huduma za chanjo kwa Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Neema Rusibimayila leo 6 Mei, 2016 jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia taarifa juu ya makabdhiano ya vifaa tiba toka Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto leo 6 Mei, 2016 Jijini Dar es Salaam. Picha zote na Benedict Liwenga)
Na Benedict Liwenga-MAELEZO.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.4 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kutoa chanjo kwa akina mama na watoto dhidi ya magonjwa mbalimbali nchini.
Akiongea na waandishi wa habari Wizarani hapo, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Dkt. Neema Rusibimayila ameeleza kuwa vifaa tiba hivyo vitasaidia uhifadhi wa chanjo katika mikoa mbalimbali pamoja halmashauri nchini.
‘’Ni msaada mkubwa tulioupata toka WHO na nina amini kuwa utatusaidia sana katika kufanikisha suala la chanjo kwa akina mama na watoto nchini na pia tunaamini wataendela kushirikiana na Wizara ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea’’, alisema Dkt. Rusibimayila.
Ameongeza kuwa, kwa sasa vituo vipya vinavyofunguliwa nchini vikiwemo vile ambavyo havikuwa na majokofu vitakuwa na uwezo wa kupata vifaa hivyo kama vile majokofu na vifaa vingine vya tiba ili huduma za chanjo ziweze kutolewa katika kila kituo nchini.
Akikabidhi vifaa hivyo Wizarani hapo, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania Dkt. Rufaro Chatoro amesema kuwa vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.4 ni pamoja na majokofu 200 pamoja na vifaa vitumikavyo kwa ajili ya kutolea chanjo.
Kwa upande wake Mratibu Chanjo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bwana Emmanuel Yohana ameeleza kuwa, majokofu hayo pia yatapelekewa katika wilaya ambayo yana upungufu wa majokofu pamoja na vituo vipya kwa ajili ya kupunguza umbali kwa wagonjwa wa chanjo na pia ni moja ya kuweka huduma karibu na wananchi nchini.
Aidha, ameongeza kuwa spesimeni za polio na surua zilizotolewa na WHO zitapalekwa pia katika vituo kwa jili ya kuchukua damu kwa ajili ya vipimo na kuletwa Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi wa maabara.‘’Wanufaika wa huu msaada kutoka WHO ni wananchi wote wa Tanzania kwani utaenda katika vituo vyote vya chini zikiwemo Zahanati’’, alisema Yohana.
Kupitia wadau mbalimbali Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea kushirikiana na wadau hao katika kutafuta vifaa tiba mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kuwa sekta ya afya nchini inaimarika kwani Tanzania kwa sasa imeweza kudhibiti polio kwa kiasi kikubwa.
No comments:
Post a Comment