Tuesday, May 17, 2016

Wakulima wawe makini na mvua hizi za masika.

Na Raymond Mushumbusi MAELEZO

Kwa miaka mingi hapa nchini Tanzania, Kilimo kimetajwa kuwa uti wa mgongo wa Taifa. Ikumbukwe kuwa miaka ya Sabini za mwanzoni kuliwahi kuwepo kauli kuhusu kilimo iliyosema “Kilimo cha Kufa na Kupona”. Kauli hii ililenga kuondoa njaa iliyokuwa inalikabili Taifa. Kwa miaka  ya hivi karibuni, serikali ikaja na Kauli Mbiu ya “Kilimo Kwanza”. Hizi zote ni jitihada za kuinua kilimo ambacho kinategemewa na walio wengi hapa kwetu.

Kilimo ni eneo la kipaumbele katika uchumi wa Tanzania licha ya kuwa  kilimo nchini bado kinategemea kwa kiasi kikubwa mvua na hali ya hewa kwa ujumla .
 
Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka ya hali ya hewa iliyotolewa na  Mkurugenzi Mkuu Dkt. Agnes Kijazi zinasema mvua za masika zimeshaanza katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi. Hata hivyo maeneo machache yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
 
Hali ya unyevunyevu wa udongo inatarajiwa kuwa ya kutosheleza shughuli za kilimo katika maeneo mengi.Hata hivyo, mvua za juu ya wastani zinazoendelea kunyesha zinaweza kusababisha hali ya unyevunyevu wa udongo kupita kiasi hivyo kuathiri mazao na hata kusababisha mafuriko na kuharibu mazao.
 
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, msimu wa mvua za Masika katika kipindi cha miezi ya Machi hadi Mei, 2016 ni mahususi katika maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara), Pwani ya Kaskazini, (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-Kaskazini pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba), Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga) na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani kwa maeneo mengi ya ukanda huo isipokuwa maeneo ya Kusini mwa ukanda huo yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani.
 
Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha tahadhari imetolewa kwa wakulima wote kuwa makini na mvua hizi za masika zinazoendelea kwani zinatarajiwa kunyesha kwa wingi katika baadhi ya maeneo kulingana na uelekeo wa upepo katika maeneo mengi ambayo yanayopata mvua za msimu wa masika.
 
Mwelekeo wa mvua uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa hivi karibuni umezingatia zaidi kipindi cha msimu(miezi mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi.
 
Wakulima wanashauriwa kuendelea na shughuli za kawaida za kilimo katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kutumia mbinu za kuongeza uzalishaji, kupanda mazao na miti kuzuia mmomonyoko wa udongo pamoja na kuzingatia ushauri wa wataalam wa kilimo katika matumizi sahihi ya ardhi na mbegu. Hata hivyo, katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za  chini ya wastani,upungufu wa unyevunyevu wa udongo unaweza kujitokea hususan katika vipindi vya kukosekana kwa mvua. Wakulima waendelee kutafuta, kupata na kuzingatia ushauri wa maafisa ugani katika kutekeleza shughuli zao.
 
Aidha wataalamu wa kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine(SUA) katika tafiti zao wametoa ushauri kuhusu namna bora ya kilimo cha baadhi ya mazao kwa kuzingatia taratibu sahihi za kilimo za mazao hayo wakati huu wa mvua za masika.
 
 
Ushauri kuhusu mtama
 
Mtama unatarajiwa kukua vizuri wakati wa masika. Wakati wa kupanda mtama, wakulima wanashauriwa kuanza utayarishaji wa mashamba kabla ya mvua. Upandaji kavu (yaani upandaji kabla ya mvua) unapendekezwa sana kwa mtama na ni bora wakulima wapande katika wiki za tatu na nne za Machi. Wakulima wanaweza kuanza kupanda mtama katika mwezi wa pili (Februari) kabla ya kupanda mimea mingine. Katika upandaji kavu, kina cha udongo (yaani urefu wa shimo kwenda chini) kinahitajika kuwa sentimeta tano ikilinganishwa na upandaji unyevu (yaani upandaji wakati udongo una maji) ambapo kina kinahitajika kuwa kama sentimita mbili nukta tano (2.5) hadi sentimita nne.
 
Wakulima wanashauriwa kuweka mbolea vizuri kwa kuchanganya na udongo.Wakulima wanashauriwa pia kupalilia angalau mara mbili wakati wa kukua kwa mimea.
 
Ushauri kuhusu Maharagwe
 
Ili kupata  mazao bora ya maharage, umwagiliaji wa maji ni muhimu. Kwa ajili ya mvua ya kawaida au nyingi inayotarajiwa, uhifadhi wa maji ya mvua unahitajika ili maji haya yatumike wakati wa mvua chache. Wakulima wanashauriwa kutumia mbinu za umwagiliaji wa mifereji ya juu au chini wakati wa ukavu kwa milimita 50 kwa wiki hadi mwisho wa msimu. Kwa kawaida, joto huwa haina athari mbaya kwa maharage, kama kiwango kizuri cha maji kimo mchangani.
 
Ushauri kuhusu Mahindi
 
Wakulima wanashauriwa waanze kupanda mahindi kabla ya mwanzo wa mvua katika wiki ya tatu au nne ya Machi. Mahindi yanafaa kupandwa punde tu hali ya udongo na joto lake linapofaa kwani kuchelewesha upandaji kunaweza kusababisha upungufu wa mavuno,kwa sababu mahindi yanahitaji unyevu bora zaidi wa udongo wakati wa upandaji, wakulima wanashauriwa kutumia hatua zinazofaa za kuhifadhi udongo.
 
Kutumia mbinu za ukulima bora ni pamoja na upandaji miti na ukulima wa mseto ambao unaweza kupunguza mmomonyoko wa udongo na kuongeza ubora wa maji na udongo. Wakulima wanahimizwa wawe na mbinu ya kuondoa maji katika maeneo yanayopata mvua nyingi ili kuzuia uharibifu wa mimea. Uchimbaji wa mitaro ya kuondoa maji haya unaweza kuzuia mafuriko na pia mmomonyoko unaopoteza udongo wa juu wenye rutuba. Kuchanganya mchanga na mbolea ya shamba kunaweza kutayarisha udongo kwa unyonyaji wa maji.
 
Mamlaka ya Hali ya Hewa imetoa wito kwa wakulima wote nchini kuzingatia ushauri kutoka kwa wataalamu wa kilimo ili kuondokana na usumbufu utakajitokeza katika msimu huu wa masika unaoendela nchini.
 
Mamlaka ya hali ya hewa imewaomba watanzania kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 pamoja na mwezi kama unavyotolewa na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania ili kujua hali inayotarajiwa kuwepo kwa kipindi chote hiki cha msimu wa mvua za masika.

No comments: