Wednesday, May 25, 2016

WAHANGA WA MAJANGA YA MOTO WILAYANI KIBAHA WAPATIWA MSAADA NA MBUNGE KOKA.

 Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka akimkabidhi mmoja wa wahanga waliounguliwa maduka yao eneo la maili moja kiasi cha shilingi laki tano ikiwa ni kuwapa msaada wa kuanzia mtaji mwingine alipofanya ziara ya siku moja ya kuwapa pole.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka akikagua moja ya sehemu ya  vibanda vya biashara vilivyopo katika eneo la maili moja baada ya kuteketea kwa moto na kuweza  kuunguza  maduka matano  moto huo ulizuka hivi karibu.(PICHA NA VICTOR MASANGU)

NA VICTOR MASANGU, KIBAHA.
WIMBI la kutokea kwa majanga ya moto bado limeonekana bado kuwa ni tatizo sugu kutokana na kuwepo kwa uelewa mdogo kwa wananchi kuhusiana na namna ya kuweza kuzuia majanga ya moto  pindi yananapojitokeza pamoja na kutokuwa na vifaa vya kuzimia.

Hayo yamebainishwa na Afisa uhusiano wa Jeshi la zima moto na uokoaji Mkoa wa Pwani Harryson Mkonyi   wakati akizungumza katika mkutano maalumu  wa kuwafariji na baadhi ya  wahanga ambao ni wafanyabiashara  waliounguliwa maduka yao na kuteketeza mali zao zote  kwa moto katika eneo la maili moja Wilayani Kibaha.

Mkonyi amebainsiha kuwa  wamebaini kuna baaadhi ya wananchi pindi wanapokumbwa na ajali ya moto  wanajikuta wanashindwa kuuzima  na kuuzuia usiendelee kusambaa katika maeneo mengine kutokana kutokuwa na vifaa, kuwa na uelewa mdogo juu ya uzimaji wa moto pamoja na kuchelewa kutoa taarifa katika vyombo vinavyohusika.

“Kwa sasa kutokana na baadhi ya wananchi kutokuwa na uelewa juu ya kupambana na majanga ya moto pindi yanapotokea, tumeanza kutoa elimu katika sehemu mbali mbali ili kuweza kuwafundisha jinsi ya kuzuaia moto kwani wakati mwingine wanachelewa kutoa taarifa kutokana na kuamua kuuzima wenyewe na unaposambaa ndipo wanatoa taarifa,”alisema Mkonyi.

Akisoma risala kwa niaba ya wahanga hao wa moto Tatu Jamaly pamoja na mmoja wa wafanyabishara waliokumbwa na majanga hayo ya moto Marietha Massaji wamesema kwamba kwa sasa wamejikuta katika wakati mgumu sana kutokana na biashara  ambazo walikuwa wanazitegemea  kwa ajii ya kujipatia kipato cha kila siku imeteketea yote kwa moto huo.

“Tulikuwa na tunafanya biashara zetu na zilikuwa zinatusaidia sana katika kujipatia kipato lakini ndio hivyo tena tumepata majanga ya moto na mali zetu zote zimeteketea, lakini tunamshukuru sana mbunge wetu wa jimbo la Kibaha mjini Silvesty Koka kwa kwa moyo wake wa  dhati kwa kutuchangia fedha amabazo zitatusaidia kuanza tena biashara zetu,”alisema Wahanga hao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa maili moja Athumani Chichi alisema kwamba kutokana na wafanyabishara hao kupatwa na matatizo wamerudishwa nyuma kimaendeleo na kuongeza kwamba ataendelea kushirikiana na mbunge wa jimbo la Kibaha kwa hali na mali kutokana na kupenda maendeleo na kuwasaidai wananachi wake pindi wanapopata matatizo.

Naye Mbunge wa jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka ambaye alifanya ziara ya kuwatembelea wahanga hao wa moto ambapo amewaasa  amewachangia  kiasi cha shilingi laki tano kwa  kila mfanyabiashara ambaye duka lake limeungua  na moto na kuwaasa kutokukata  tamaa na badala yake mtaji mwingine  huo aliowapatia wautumie vizuri katika kukuza biashara zao na sio vinginevyo.

Koka  alisema kwamba anatambua uchungu walionao wahanga hao ambapo ameahidi kuendeea  kuwasaidia na kushirikiana nao bega kwa bega katika kuhakikisha wanatimiza malengo yao kupitia shughuli zao za ujasiliamali wanazozifanya.

MOTO huo ambao ulizuka  katika eneo la maili moja Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani  umeweza kuteketeza maduka matano pamoja na mali za wafanyabiashara,wa aina mbali mbali lakini haukuweza kuleta madhara yoyote kwa  binadamu.

No comments: