Fainali za Kombe la Shirikisho maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) zinatarajiwa kufanyika kesho Mei 25, 2016 kwa kuzikutanisha timu za Young Africans na Azam FC; zote za Dar es Salaam katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Taifa jijini.
Sherehe za mchezo huo zitaanza rasmi saa 8.00 mchana kwa mchezo wa awali wa kuburudisha kuzikutanisha timu za soka za kituo cha Televisheni cha Azam ‘Azam Tv’ na wafanyakazi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kurushwa live na kituo hicho kilichotokea watazamaji wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Viingilio katika mchezo huo itakuwa ni Sh 25,000 kwa VIP A wakati VIP B na C ni Sh 20,000 wakati majukwaa yenye viti vya rangi ya chungwa, mzunguko wenye viti vya rangi ya bluu na kijani ni Sh 5,000.
TFF inajivunia nyota wake kama Jemedari Said, Wilfred Kidao, Salum Madadi, Alfred Lucas, Danny Msangi, Michael Ngogo na Jonas Kiwia, lakini Meneja wa timu ya Wafanyakazi wa TFF, Eliud Mvella anasikitika kumkosa nyota wake Mwesigwa Selestine.
Azam Tv wanatamba na nyota wao waliopata kufanya kazi nje ya nchi katika vyombo vya kimataifa kama vile Charles Hilary, Tido Mhando, Yahaya Mohammed, Baruan Muhuza na Rhys aliyetajwa kwa jina moja.
Mbali ya burudani hiyo, pia Mwakilishi wa Azam Tv, Baruan Muhuza alisema kwamba mara baada ya mchezo huo utakaomalizika saa 9.00 alasiri, itafuata burudani ya wasanii mbalimbali ambao pia wataburudisha wakati wa mapumziko ya mchezo huo.
Alisema kwamba burudani hiyo itakuwa ni ya nusu saa kabla ya kuziacha timu kufanya maozezi ya kupasha moto viungo kabla ya mchezo huo kuanza saa 10.30 jioni na wakati wa mapumziko burudani itaendelea kabla ya kutolewa taji ambalo timu zitakuwa zikiliwania.
Kwa mujibu wa kanuni bingwa wa michuano hiyo atatwaa kombe, medali na fedha Sh 50,000,000 wakati mshindi wa pili atazawadiwa tuzo na medali. Kadhalika kutakuwa na tuzo kwa mchezaji bora, mfungaji bora na mchezaji bora wa michuano hiyo ambayo waaandaaji wamepanga kuiboresha mwakani.
Mwamuzi wa mchezo huo atakuwa Israel Mujuni Nkongo wa Dar es Salaam kwa mujibu wa Kamati ya Waamuzi ya TFF huku akisaidiwa na Ferdinand Chancha wa Mwanza upande wa kulia (line 1) na upande wa pili ni Soud Lila wa Dar es Salaam (line 2) na mwamuzi wa akiba mezani ni Frank Komba wa Dar es Salaam pia. Kamishna wa mchezo huo anatakuwa Juma Mgunda wa Tanga.
Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu msimu 2015/16, mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu 2015/16 wataiwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2016/17. Nafasi hiyo imechukuliwa na Young Africans.
Kadhalika Azam ina tiketi tayari ya kushiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kufika fainali za ASFC ingawa kanuni zinataka bingwa ambako kwa upande wa Yanga wana tiketi ya michuano ya juu zaidi ya shirikisho. Mvuto wa mchezo wa Jumatano ni ushindani wa soka na zawadi kwa bingwa.
Fainali za Kombe la Shirikisho zinakuja baada ya mchuano ulioshindanisha timu 64 za Ligi Kuu Tanzania Bara - VPL (16); Ligi Daraja la Kwanza -FDL (24), Ligi Daraja la Pili – SDL (24).
No comments:
Post a Comment