Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Taasisi ya Wanawake ya Mbalawala inayojishughulisha na uzalishaji wa braketi za makaa ya mawe ijulikanayo kama Mbalawala Women Organization yanye makazi yake katika kijiji cha Ruanda wilayani Mbinga mkoani Ruvuma imeipongeza Wizara ya Nishati na Madini kupitia Kitengo cha Mawasiliano Serikali kwa kutangaza shughuli zake hali iliyopelekea wateja wa makaa ya mawe katika taasisi hiyo kuongezeka kadri siku zinazokwenda.
Taasisi hiyo inayofanya shughuli zake karibu na Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka inajishughulisha na utengenezaji wa briketi bora za makaa ya mawe kwa ajili ya kupikia.
Pongezi hizo zilitolewa na Meneja Uendeshaji wa Taasisi hiyo Hajiri Kapinga aliyekutana na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasilano Serikalini Wizara ya Nishati na Madini, Asteria Muhozya jijini Dar es Salaam na kusema kuwa tangu Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kianze kuchapisha habari zinazohusu taasisi hiyo kupitia Jarida lake linalochapishwa kila wiki lijulikanano kama MEM Newsbulletin wameshuhudia idadi kubwa ya wateja ikiongezeka na kuzidi uzalishaji wa taasisi hiyo.
Alisema kabla ya habari zake kuchapishwa na Jarida la Wizara, taasisi hiyo ilikuwa ikiwauzia briketi za makaa ya mawe wateja wake walioko katika vijiji vinavyozunguka mgodi wao wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
“Mara baada ya taarifa zetu kuanza kuchapishwa na Jarida la Wizara ya Nishati na Madini tumeshuhudia mabadiliko makubwa kwani tumekuwa tukipokea simu kutoka mikoa mbalimbali hususan Dar es Salaam, Mbeya, Iringa wateja wakihitaji bidhaa, hali inayopelekea mahitaji kuwa makubwa kuliko kiasi tunachozalisha,.” alisema Kapinga.
“Jarida limetufanya tujulikane, hata wahisani wetu wameahidi kuongeza nguvu na misaada katika kuwezesha mradi huu kuendelea vizuri; Jamii inasoma habari zetu na sisi tumesoma masuala mengi kuhusu nishati na madini,” aliongeza.
Kapinga aliendelea kusema kuwa ili kukabiliana na mahitaji makubwa ya wateja taasisi hiyo imeweka mkakati wa kununua mtambo mwingine kutoka nje ya nchi ili kuongeza uzalishaji utakaoendana na mahitaji ya wateja.
Alisema mikakati mingine ni pamoja na ujenzi wa ghala la kuhifadhia makaa ya mawe, ununuzi wa magari kwa ajili ya usambazaji wa bidhaa ya briketi za makaa ya mawe katika vituo vya uwakala vitakavyoanzishwa nchini karibu kila mkoa.
“Mara baada ya kuanzisha vituo hivyo, wateja wetu watakuwa wanapata bidhaa kutoka kwa mawakala badala ya kukutana na sisi moja kwa moja,” alisema Kapinga.
Alisema kuwa pia wamejipanga kutoa elimu ya matumizi ya briketi za matumizi ya makaa ya mawe na utafutaji wa masoko kwa kushirikiana na wadau wa utengenezaji wa majiko sanifu yanayotumia briketi za makaa ya mawe kwa matumizi ya majumbani.
Akielezea uanzishwaji wa taasisi hiyo, Kapinga alisema kuwa taasisi hiyo ilianzishwa chini ya ufadhili wa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka (Tancoal Energy Limited) unaomilikiwa na kampuni ya Intra Energy ya Australia kwa asilimia 70 na Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kwa asilimia 30 ambao wanafurahishwa na hatua iliyofikiwa na taasisi hii katika uzalishaji ya briketi za makaa ya mawe.
Aliongeza sambamba na uzalishaji wa briketi za makaa ya mawe, taasisi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo juu ya utumiaji wa briketi ya makaa ya mawe katika vijiji na miji jirani na mgodi wake pamoja na ushiriki katika maonesho mbalimbali ndani ya mkoa wa Ruvuma.
“Lengo letu ni kuhakikisha briketi za makaa ya mawe zinazoendelea kuzalishwa katika mgodi wetu zinatumika majumbani, shuleni , vyuoni na taasisi mbalimbali na kupunguza uharibifu wa mazingira kwa kutumia kuni” alisema Kapinga.
Aliendelea kusema kuwa lengo la uanzishwaji wa taasisi hiyo lilikuwa ni kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kupitia briketi za makaa ya mawe na kuachana na matumizi ya kuni ambayo ni chanzo cha uharibifu wa mazingira.
Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Asteria Muhozya alisema kuwa lengo la Jarida la Wizara ni kutangaza shughuli za nishati na madini ikiwa ni pamoja na taasisi zake.
Muhozya aliongeza kuwa jarida la Wizara lipo tayari kutangaza shughuli za wadau wa Madini na Nishati ili kuhakikisha kuwa sekta hizo zinakuwa na kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi
No comments:
Post a Comment