TAWI la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya
(TUGHE) la Makao Makuu ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA-HQ),
limepata viongozi wake wapya katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni kwenye
ukumbi wa Transit uliopo katika jengo la Kiwanja cha Ndege cha Zamani (TBI).
TAA ni wakala wa Serikali iliyoanzishwa tarehe 29
Novemba 1999 kwa Tangazo la Serikali Na.404 la mwaka 1999 chini ya kifungu cha
3 cha Sheria Na. 30 ya mwaka 1997 ya Wakala wa Serikali. Wakala hii ilirithi
majukumu ya iliyokuwa Idara ya Viwanja vya Ndege (Directorate of Aerodromes)
chini ya Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, ulizinduliwa rasmi mnamo tarehe 3
Desemba 1999.
Viongozi hao wamepatikana baada ya uliokuwepo
kumaliza muda wao, na waliochaguliwa katika
uchaguzi huo uliosimamiwa na Katibu Mkuu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Gaudence
Kadyango, ni pamoja na Mwenyekiti Bw. Nasib
Elias aliyezoa kura zote 28, baada ya kutokuwa na mpinzani, huku katibu mkuu akichaguliwa
Bi. Aziza Kipande aliyepata kura 15 akimshinda Bi. Caroline Mntambo aliyepata
kura 13.
Wajumbe watatu ambao ni Bi. Mwanaisha Omari, Bw. Joel
Mwakamele na Bi. Frida Omari walipitishwa bila kupingwa na wajumbe waliotoka
idara mbalimbali za TAA HQ.
Naye Bi. Irene Sikumbili alipata kura zote 14 za
wanawake na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake na Katibu Mkuu
wake ni Bi. Mwanahawa Mdee aliyepata kura 11 akimshinda Bi. Kipande aliyepata
kura tatu.
Walioshinda katika nafasi ya ujumbe katika kamati hiyo ni Bi. Glory Mollel
na Bi. Pendo Pascal; wakati Bi. Mntambo ameukwaa uweka hazina na Bi. Magreth
Mushi ni mwakilishi wa vijana, huku hakukuwa na mwakilishi wa walemavu kutokana
na kutokuwa na mlemavu.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA SHERIA NA MAHUSIANO TAA
No comments:
Post a Comment