Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto imesikitishwa na tukio la ubakaji na udhalilishwaji lililofanywa na wanaume
wawili dhidi ya mwanamke mmoja, ambaye alishurutishwa kuwa mtupu, kufanya ngono bila ridhaa yake, kupigwa picha na kusambazwa
katika mitandao ya kijamii hapa nchini.
Wizara inalaani
vikali kitendo hiki cha ukatili na udhalilishaji kilichofanywa na wanaume wawili,
ambao wamekamatwa na Polisi kwa kuhusishwa na udhalilishaji huo. Mazingira ya ukatili
huo yanahuzunisha, kwani inaelezwa kuwa wanaume hao kwa wakati mmoja walihusika
kumwingilia kimwili pasipo ridhaa yake, ilihali,wakimpiga picha za tukio zima
la ubakaji huo. Kitendo hiki, ni ukatili usio na kifani, maana kimefedhehesha utu wake binafsi na kudhalilisha familia
yake, na wanawake kwa ujumla. Aidha, kitendo hiki kinaweza kusababisha madhara
makubwa kwa mwanamke huyu kimwili,kisaikolojia,
kijamii na kihisia.
Wizara inaamini kuwa, vitendo
hivi vya ubakaji na udhalilishaji havistahili kuvumiliwa hata kidogo, maana vinaashiria
kuwepo kwa matumizi ya nguvu, vitisho, kulazimishwa kuingiliwa,
na kuna uwezekano mkubwa wa mwanawake huyu kuwa katika hali ya hatari zaidi
ambayo inagusa maisha yake binafsi, jambo ambalo ni haki yake ya msingi.
Naomba ieleweke kuwa, Wizara haitetei ukosefu wa uaminifu miongoni mwa
wanandoa au watu wenye mahusiano ya kimapenzi, bali tunasisitiza kwamba mwanawake
sawa na binadamu wengine anastahili na ana haki ya kuthamaniwa utu wake kwa
mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ikumbukwe kuwa uhuru na
haki ya kufanya mapenzi ni hiari na kamwe hayafanyiki kwa kulazimishwa.
Navipongeza vyombo vya usalama kwa weledi wa kazi yao ambavyo
vimewasaka na na kufanikisha kupatikana kwa watuhumiwa wa ukatili huo. Serikali
itahakikisha mkondo wa sheria unafuatwa kuhakikisha haki inatendeka.
Natoa wito kwa wananchi wote kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha
vitendo hivi vinakoma kabisa katika jamii zetu za Kitanzania. Hakika huu sio utamaduni
wetu! ni lazima tuhakikishe tunapambana kukomesha tabia za udhalilishaji wa
wanamke na watoto wa kike kwa nguvu zote. Tujenge tabia ya kutoa taarifa kwa
haraka matukio yote ya ukatili dhidi ya wanawake yanapotokea katika jamii zetu.
Aidha, natoa rai kwa mamlaka zinazohusika na ulinzi na haki za wanawake
zihakikishe zinaelimisha jamii kubadilika na kuhakikisha wanawake wanalindwa
maana hawa ni mama zetu, dada, zetu, na binti zetu. Pia, natoa wito kwa
viongozi mbalimbali katika jamii kutofumbia macho matukio ya udhalilishaji wa
wanawake yanayo kiuka maadili ya jamii yetu.
Naomba kutoa
rai kwa wawakilishi wa kisiasa, watendaji, na wadau wa haki za watoto kutumia
nafasi zetu katika kuelimisha wananchi kuondokana na tabia za ukatili dhidi ya
wanawake, hususan suala zima la udhalilishaji wa picha za utupu kupitia
mitandao ya kijamii, tabia ambayo imeibuka kwa kasi kubwa katika siku za hivi
karibuni. Kamwe Taifa haliwezi kuhesabika kuwa limeendelea kama utu wa mwanamke
utwezwa na kudhalilishwa usoni mwa mataifa mengine duniani.
Erasto T. Ching’oro
Mkuu wa Kitengo cha Mawasilino
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
16/5/2016
No comments:
Post a Comment